Thursday, May 19, 2016

GADO TOON: AFRICAN LEADERS AND CHINA


SUKARI TAMU JAMANI, ANGALIA ITAKULEVYA.
Sukari kitu kitamu, kaumu tunaisifia,
Huwa tuna nyingi hamu, wengi wetu kutumia,
Tukosapo hulaumu, shutuma nyingi kutoa,
Inafaa kutambua, sukari jama ni dhara.

Sukari ina mashaka, athari hutuletea,
Hatari tazitamka, zile ninazozijua,
Kwanza meno kung'oka, mengine hujiozea,
Sukari ina udhia, ukila tahadhari.

Taumbuka ujue, sukari ukiisoea,
Hukufunga utambue, utamu ukikukaa,
Lazima usijijue, kishailafukia,
Haifai kubugia, sukari uiogope.

Hukupatisha hasara, kila mara kitumia,
Hukutia safura, kila leo kijitia,
Tumbo laweza fura, halafu akajutia,
Japo tamu balaa, sukari iogope.

Maradhi yake thakili, usingizi yanatia,
Sijue yako hali, fikra kukujalia,
Hukufanya idhihali, kibidi kujutia,
Sukari naisemea, siri yake tambue

Wengi wafedheheka, sukari kipapia,
Wengine kuadhirika, wasijie pakwendea,
Vichwa moto kuwawaka, kila wakifikiria,
Kama hujatambua, ni chungu kuila sukari.

Wengine naokula, vibaya kwa mazoea,
Sasa wameanza lala, mshangao wawaingia,
Humaliza zao hila, taabu kuiondoa,
Lishalo kujigandia, kupapatua ni mambo.

Jambo moja ninapenda, sukari ninowambia,
Sio ile ya Makonda, na nje kuagizia,
Hii siwezi iponda, wala ila kuitia, 
Yafaa itambua, sukari niisemayo.

Si mapenzi asilani, haifai fikiria, 
Takuwa nabuni, hilo kiliwazia,
Iko mafichoni, kazi yako ng'amua,
Kitendawili tegua, kishindwa nipe mji.

Wasalaam, namaliza, sitaki endelea,
Jibu lako kiliwaza, fumbo hilo tegua,
Elimu tumia kwanza, fasihi kiijua,
Wengi ishawalevya, sukari tamu ya ila.

Thursday, May 12, 2016

USISUMBUKIE KICHAA
Kichaa kusumbukia, sumbuko usisumbuke
Jambo hilo zingatia, maoni yangu ushike,
Kichaa ana udhia, utajuta mwisho wake,
Sumbuko usisumbuke, kusumbukia kichaa.

Kichaa hana sheria, katika maisha yake,
Kila litomzukia, hilo ndilo sawa kwake,
Hata kama akasema, jukumu limuepuke,
Sumbuko usisumbuke, kusumbukia kichaa.

Hajui alo murua, mbaya na mwema wake,
Wote atawasumbua, hatimaye awacheke,
Japokuwa waumia, atoke aende zake,
Sumbuko usisumbuke, kusumbukia kichaa.

Daktari maradhia, hutibu maradhi yake,
Yeye akamwendea, humrushia mateke,
Majeraha kumtia, na heshima iondoke,
Sumbuko usisumbuke, kusumbukia kichaa.

Yeye kwake ni tabia, hili lile aropoke,
Siasa kuhubiria, na dini ichanganyike,
Lengo lake kukutia, makosani upotoke,
Sumbuko usisumbuke, kusumbukia kichaa.

Vichaa nakusudia, wa nyingi aina zake,
Ni wale wakulimbia, na nyumbani wasitoke,
Nyumbani kuwafungia, ni makubwa dhara yake,
Sumbuko usisumbuke, kusumbukia kichaa.

Vichaa utakutia, waume na wanawake, 
Mjini wanatembea, kwa vishindo na makeke,
Wao wanafurahia, mashamba wakuondoke,
Sumbuko usisumbuke, kusumbukia kichaa.

Wengine wajisumbua, kwa kutaka wasikike,
Majununi kujitia, kwa kutaka wasumbuke,
Sumbuko usisumbuke, kusumbukia kichaa.

Hatua ikifikia, lazima ubabaike,
Yupi alotimilia, katika vitendo vyake,
Mizani isotimia, mgongoni tuwaweke,
Sumbuko usisumbuke, kusumbukia kichaa.

Kaditamati natua, kituoni mwisho wake, 
Lakini nashadadia, kwa kichaa sisumbuke
Aisifiaye mvua, kaloa mwili wake,
Sumbuko usisumbuke, kusumbukia Kichaa

Monday, May 9, 2016

NANI KAMA MAMA, NAAMINI HAKUNA!


Tafakari kwa kina, marefu na mapana, Maisha alotupa muamana, atuhimizaye kila adhana, Ndipo utapoona, wanadamu twafanana, Yupo alobeba dhamana, katika maisha na amana, Nani kama mama, naamini hakuna.

Mama ndio kila kitu, katika maisha jamani, Miezi tisa si kitu, kutuvumilia amini, Watundu kwa watukutu, katupenda yamini, Mama kabeba uthubutu, kutufariji nafsini, Nani kama mama, naamini hakuna. Mama alivumilia, zuri nalo baya, Kila alosikia, kukuhusu kwa wanaizaya, Subira alisubiria, hadi majira yalipowadiya, Kwa upole akuulizia, akukemea ukigwaya, Nani kama mama, naamini hakuna. Mama rafiki wa kweli, maishani na kifoni,
Kutuvumilia hakujali, miezi tisa duniani, Maumivu makali, mateso yaso kifani, Mama atakabali, malezi yetu ujanani,
Nani kama mama, naamini hakuna.

Atayemkana mama, huyo hayawani,
Atayebeba lawama, maishaye bila hisani,
Hana usalama, dini wala imani,
Si kwa maulamaa, wahafadhini hata wafiadini,
Nani kama mama, naamini hakuna.

Saturday, May 7, 2016

TUYAZINGATIE HAYA WALA TUSIRUDI NYUMA.
Wazalendo hima hima, uchumi kuufufua,
Tena tusimame wima, hatua kuzichukua,
Jambo lililolazima, mbinu bora kutumia,
Tuyazingatie haya, wala tusirudi nyuma.

Uchumi kuufufa, si hotuba refu sana,
Moja litosaidia, ni kwa kuhamasishana,
Jengine lafuatia, sote kushirikiana,
Tuyazingatie haya, wala tusirudi nyuma.

Malengo kuyafikia, jamani si maongezi,
Hasa litotuinua, ni kuwa wachapa kazi,
Jukumu kutumikia, raia, na viongozi,
Tuyazingatie haya wala tusirudi nyuma.

Kufanya kazi lazima, tuacheni utegezi,
Na jingine la kukoma, kuwepo kwa ubaguzi,
Kutupiana lawama, ni mambo ya kipuuzi,
Tuyazingatie haya wala tusirudi nyuma.

Uliyepewa dhamana, uache kupora mali,
Acha kutia fitna, jungu si kitu amali,
Ni bora kukosoana, uonapo idhihali,
Tuyazingatie haya, wala tusirudi nyuma.

Kile tunokipitisha, vikaoni na bungeni,
Isiwe kukikwamisha, tukawa hatukioni,
Au kukikadilisha, tusikione machoni,
Tuyazingatie haya, wala tusirudi nyuma.

Tamaa ya utajiri, tuiacheni jamani,
Mbona hii ni hatari, inatutia shidani,
Mnaacha desturi, twafata njia gani?
Tuyazingatie haya, wala tusirudi nyuma.

Jama zigo la makuti, katu tusijejitwika,
Sijefika kati kati, mambo yaja panguka,
Tukafika mauti, ahadi haijafika,
Tuyazingatie haya, wala tusirudi nyuma.

Tuwekeni mwongozi, tusijitie vikwazo'
Tupime wetu uwezo, tusibebe matatizo,
Yapokewapo mawazo, sijetokea mizozo'
Tuyazingatie haya wala tusirudi nyuma.

Ya kupanga yenye kheri, yalo fanaka njema,
Tusiitafute shari, ikajazuka dhahama,
Mambo yende vizuri, kama tulivyoyapima,
Tuyazingatie haya, wala tusirudi nyuma.

GADOTOON: MAGUFULI AT WORKSunday, May 1, 2016

SI LEO TOKA ZAMANI MKULIMA MTU DUNI.Si leo toka zamani, mkulima mtu duni,
Ana tabu maishani, tena hana thamani,
Yafaa tutizameni, kisha tuyachunguzeni,
Si leo toka zamani, mkulima mtu duni.


Jogoo linapowika, kokoriko mitaani,
Mkulima huamka, jembe lake mkononi,
Bila ya kupumzika, hufika kwake shambani,
Si leo toka zamani, mkulima mtu duni.


Na tena mvua na jua, humwangukia mwilini,
Mkulima huungua, kwa kazi kuithamini,
Mimea kupalilia, kukwepa umaskini,
Si leo toka zamani mkulima mtu duni.


Mkulima lengo lake, mazao kujipatia,
Kuwaamini wenzake, maisha kufurahia,
Kwa hakika kazi yake, thamani yahitajia,
Si leo toka zamani, mkulima mtu duni.


Wakaazi wa mijini, na wafanyakazi pia,
Na viongozi nchini, huduma  awapatia,
Sijui kakosa nini?, Thamani kutomtia,
Si leo toka zamani, mkulima mtu duni.


Maisha ya mkulima, humalizika taabuni,
Haonji malazi mema, kila siku vibandani,
Wenye baba na yatima, wote wako mashakani
Si leo toka zamani, mkulima mtu duni.


Upungufu wa chakula, utokeapo nchini,
Hukumbana na swala, shambani wafanya nini?
Kazi yako unalala, watia njaa nchini,
Si leo toka zamani, mkulima mtu duni.


Starehe kwa ujumla, zinaishia mijini,
Maji safi ya muala, njia na umeme ndani,
Aliyezichuma hela, ni mkulima shambani,
Si leo toka zamani, mkulima mtu duni.


Dharau wakielewa, kuna hatari mbeleni,
Mkulima ang'amuwa, naye akae mjini,
Hapo ndipo tutajua, mkulima naye nani,
Si leo toka zamani, mkulima mtu duni.