Thursday, May 12, 2016

USISUMBUKIE KICHAA
Kichaa kusumbukia, sumbuko usisumbuke
Jambo hilo zingatia, maoni yangu ushike,
Kichaa ana udhia, utajuta mwisho wake,
Sumbuko usisumbuke, kusumbukia kichaa.

Kichaa hana sheria, katika maisha yake,
Kila litomzukia, hilo ndilo sawa kwake,
Hata kama akasema, jukumu limuepuke,
Sumbuko usisumbuke, kusumbukia kichaa.

Hajui alo murua, mbaya na mwema wake,
Wote atawasumbua, hatimaye awacheke,
Japokuwa waumia, atoke aende zake,
Sumbuko usisumbuke, kusumbukia kichaa.

Daktari maradhia, hutibu maradhi yake,
Yeye akamwendea, humrushia mateke,
Majeraha kumtia, na heshima iondoke,
Sumbuko usisumbuke, kusumbukia kichaa.

Yeye kwake ni tabia, hili lile aropoke,
Siasa kuhubiria, na dini ichanganyike,
Lengo lake kukutia, makosani upotoke,
Sumbuko usisumbuke, kusumbukia kichaa.

Vichaa nakusudia, wa nyingi aina zake,
Ni wale wakulimbia, na nyumbani wasitoke,
Nyumbani kuwafungia, ni makubwa dhara yake,
Sumbuko usisumbuke, kusumbukia kichaa.

Vichaa utakutia, waume na wanawake, 
Mjini wanatembea, kwa vishindo na makeke,
Wao wanafurahia, mashamba wakuondoke,
Sumbuko usisumbuke, kusumbukia kichaa.

Wengine wajisumbua, kwa kutaka wasikike,
Majununi kujitia, kwa kutaka wasumbuke,
Sumbuko usisumbuke, kusumbukia kichaa.

Hatua ikifikia, lazima ubabaike,
Yupi alotimilia, katika vitendo vyake,
Mizani isotimia, mgongoni tuwaweke,
Sumbuko usisumbuke, kusumbukia kichaa.

Kaditamati natua, kituoni mwisho wake, 
Lakini nashadadia, kwa kichaa sisumbuke
Aisifiaye mvua, kaloa mwili wake,
Sumbuko usisumbuke, kusumbukia Kichaa

No comments: