Saturday, May 7, 2016

TUYAZINGATIE HAYA WALA TUSIRUDI NYUMA.
Wazalendo hima hima, uchumi kuufufua,
Tena tusimame wima, hatua kuzichukua,
Jambo lililolazima, mbinu bora kutumia,
Tuyazingatie haya, wala tusirudi nyuma.

Uchumi kuufufa, si hotuba refu sana,
Moja litosaidia, ni kwa kuhamasishana,
Jengine lafuatia, sote kushirikiana,
Tuyazingatie haya, wala tusirudi nyuma.

Malengo kuyafikia, jamani si maongezi,
Hasa litotuinua, ni kuwa wachapa kazi,
Jukumu kutumikia, raia, na viongozi,
Tuyazingatie haya wala tusirudi nyuma.

Kufanya kazi lazima, tuacheni utegezi,
Na jingine la kukoma, kuwepo kwa ubaguzi,
Kutupiana lawama, ni mambo ya kipuuzi,
Tuyazingatie haya wala tusirudi nyuma.

Uliyepewa dhamana, uache kupora mali,
Acha kutia fitna, jungu si kitu amali,
Ni bora kukosoana, uonapo idhihali,
Tuyazingatie haya, wala tusirudi nyuma.

Kile tunokipitisha, vikaoni na bungeni,
Isiwe kukikwamisha, tukawa hatukioni,
Au kukikadilisha, tusikione machoni,
Tuyazingatie haya, wala tusirudi nyuma.

Tamaa ya utajiri, tuiacheni jamani,
Mbona hii ni hatari, inatutia shidani,
Mnaacha desturi, twafata njia gani?
Tuyazingatie haya, wala tusirudi nyuma.

Jama zigo la makuti, katu tusijejitwika,
Sijefika kati kati, mambo yaja panguka,
Tukafika mauti, ahadi haijafika,
Tuyazingatie haya, wala tusirudi nyuma.

Tuwekeni mwongozi, tusijitie vikwazo'
Tupime wetu uwezo, tusibebe matatizo,
Yapokewapo mawazo, sijetokea mizozo'
Tuyazingatie haya wala tusirudi nyuma.

Ya kupanga yenye kheri, yalo fanaka njema,
Tusiitafute shari, ikajazuka dhahama,
Mambo yende vizuri, kama tulivyoyapima,
Tuyazingatie haya, wala tusirudi nyuma.

No comments: