Thursday, May 19, 2016

SUKARI TAMU JAMANI, ANGALIA ITAKULEVYA.
Sukari kitu kitamu, kaumu tunaisifia,
Huwa tuna nyingi hamu, wengi wetu kutumia,
Tukosapo hulaumu, shutuma nyingi kutoa,
Inafaa kutambua, sukari jama ni dhara.

Sukari ina mashaka, athari hutuletea,
Hatari tazitamka, zile ninazozijua,
Kwanza meno kung'oka, mengine hujiozea,
Sukari ina udhia, ukila tahadhari.

Taumbuka ujue, sukari ukiisoea,
Hukufunga utambue, utamu ukikukaa,
Lazima usijijue, kishailafukia,
Haifai kubugia, sukari uiogope.

Hukupatisha hasara, kila mara kitumia,
Hukutia safura, kila leo kijitia,
Tumbo laweza fura, halafu akajutia,
Japo tamu balaa, sukari iogope.

Maradhi yake thakili, usingizi yanatia,
Sijue yako hali, fikra kukujalia,
Hukufanya idhihali, kibidi kujutia,
Sukari naisemea, siri yake tambue

Wengi wafedheheka, sukari kipapia,
Wengine kuadhirika, wasijie pakwendea,
Vichwa moto kuwawaka, kila wakifikiria,
Kama hujatambua, ni chungu kuila sukari.

Wengine naokula, vibaya kwa mazoea,
Sasa wameanza lala, mshangao wawaingia,
Humaliza zao hila, taabu kuiondoa,
Lishalo kujigandia, kupapatua ni mambo.

Jambo moja ninapenda, sukari ninowambia,
Sio ile ya Makonda, na nje kuagizia,
Hii siwezi iponda, wala ila kuitia, 
Yafaa itambua, sukari niisemayo.

Si mapenzi asilani, haifai fikiria, 
Takuwa nabuni, hilo kiliwazia,
Iko mafichoni, kazi yako ng'amua,
Kitendawili tegua, kishindwa nipe mji.

Wasalaam, namaliza, sitaki endelea,
Jibu lako kiliwaza, fumbo hilo tegua,
Elimu tumia kwanza, fasihi kiijua,
Wengi ishawalevya, sukari tamu ya ila.

No comments: