Sunday, May 1, 2016

SI LEO TOKA ZAMANI MKULIMA MTU DUNI.Si leo toka zamani, mkulima mtu duni,
Ana tabu maishani, tena hana thamani,
Yafaa tutizameni, kisha tuyachunguzeni,
Si leo toka zamani, mkulima mtu duni.


Jogoo linapowika, kokoriko mitaani,
Mkulima huamka, jembe lake mkononi,
Bila ya kupumzika, hufika kwake shambani,
Si leo toka zamani, mkulima mtu duni.


Na tena mvua na jua, humwangukia mwilini,
Mkulima huungua, kwa kazi kuithamini,
Mimea kupalilia, kukwepa umaskini,
Si leo toka zamani mkulima mtu duni.


Mkulima lengo lake, mazao kujipatia,
Kuwaamini wenzake, maisha kufurahia,
Kwa hakika kazi yake, thamani yahitajia,
Si leo toka zamani, mkulima mtu duni.


Wakaazi wa mijini, na wafanyakazi pia,
Na viongozi nchini, huduma  awapatia,
Sijui kakosa nini?, Thamani kutomtia,
Si leo toka zamani, mkulima mtu duni.


Maisha ya mkulima, humalizika taabuni,
Haonji malazi mema, kila siku vibandani,
Wenye baba na yatima, wote wako mashakani
Si leo toka zamani, mkulima mtu duni.


Upungufu wa chakula, utokeapo nchini,
Hukumbana na swala, shambani wafanya nini?
Kazi yako unalala, watia njaa nchini,
Si leo toka zamani, mkulima mtu duni.


Starehe kwa ujumla, zinaishia mijini,
Maji safi ya muala, njia na umeme ndani,
Aliyezichuma hela, ni mkulima shambani,
Si leo toka zamani, mkulima mtu duni.


Dharau wakielewa, kuna hatari mbeleni,
Mkulima ang'amuwa, naye akae mjini,
Hapo ndipo tutajua, mkulima naye nani,
Si leo toka zamani, mkulima mtu duni.

No comments: