Wednesday, March 4, 2015

SAKATA LA MADAWA YA KULEVYA TANZANIA.
Kliniki maalum ya kuwatibu waathirika wa Madawa ya Kulevya iliyopo Muhimbili. Picha na Erin Bynes wa Aljazeera.


Mwathirika wa madawa ya kulevya akipata dozi ya madawa ya aina ya Methadone yanayotumika kuwatibu waathirika wa madawa ya kulevya inayotolewa katika Kliniki maalum iliyopo Muhimbili. Picha na Erin Bynes wa AljazeeraNa Baraka Mfunguo, 

(Imetokana na mwendelezo wa makala ya Aljazeera ya "Strung Out in Tanzania" iliyoandikwa na Sarika Bansal)

Napenda kuwapa pongezi Aljazeera ambao wamenipa hamasa na kuweza  kuchimba kwa undani kuhusu tatizo la madawa ya kulevya linaloikabili nchi yetu hususan vijana. Aljazeera  wameandika makala nzuri  yenye kuelimisha juu ya tatizo la matumizi ya madawa ya kulevya Tanzania.  Kwa mujibu wa makadirio ya shirika la takwimu kwa mwaka 2015 idadi ya watanzania inakadiriwa kufikia     47,421,786    katika idadi hiyo ya watu asilimia 65% ni vijana. Katika janga la madawa ya kulevya asilimia kubwa ya waathirika ni vijana wa umri kuanzia miaka 8-50. Hali imekuwa mbaya sana na tunakoelekea ndio kubaya Zaidi ikiwa jamii na serikali havitachukua hatua.

Sababu zinazochangia vijana kujihusisha na madawa ya kulevya
 • Ukosefu wa ajira.
 • Umaskini.
 • Kupoteza  tumaini la maisha.
 • Serikali kufumbia macho na kutokuwa na sharia kali dhidi ya wasambazaji na walanguzi wa madawa hayo.
 • Rushwa.
 • Utandawazi.

Kijiwe cha kutumia madawa ya kulevya kinachojulikana kama Sheraton wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam. Picha na Erin Bynes wa Aljazeera

Muuzaji wa madawa ya kulevya akiwa na kete za madawa aina ya Heroin ambayo huuzwa kuanzia 1500 mpaka shilingi 2000. Picha na Erin Bynes wa Aljazeera
Juma Omari,  25 mtumiaji madawa ya kulevya akionyesha michoro katika mwili wake. Picha na Erin Bynes wa Aljazeera.


Hatua ya serikali iliyochukua ni kuanzisha program maalumu za kuwatibu vijana dhidi ya madawa ya kulevya katika kliniki iliyopo Hospitali ya Muhimbili . Baadhi ya asasi za kijamii zimeanzisha miradi maalum kama vile “House of Sober” mahala ambapo mwathirika wa madawa anakwenda kukaa na kutibiwa dhidi ya matumizi ya madawa ya kulevya.  Hata hivyo changamoto bado ni kubwa hususan rasilimali watu, fedha na ushirikiano kutoka serikalini.


Mwandishi Sarika Bansal wa Aljazeera amekwenda kwa undani na kulifuatilia suala hilo. Nami nimejaribu kuchukua baadhi ya machache ambayo ningependa kuwashirikisha. Mwandishi  amemzungumzia mwathirika wa madawa hayo ajulikanaye kama Stamil Hamad mwanamama mwenye umri wa miaka 34 ambaye ameamua kuachana na madaya ya kulevya kupitia program maalum inayoendeshwa na kliniki maalum inayotibu waathirika wa madawa ya kulevya iliyopo Muhimbili. Mwaka 2009 serikali kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa jamii ilianza mkakati wa kuwapata wahisani, wafadhili na watu wenye moyo wa kujitolea ndani na nje ya Tanzania katika kuzuia na kutibu waathirika wa madawa ya kulevya. Hata hivyo ni chini ya asilimia moja ya waathirika wa madawa haya ndio wanaweza kuhimili na kumudu matibabu.
Michoro ya aina ya madawa iliyopo katika kuta za kliniki maalum ya kuwatibu waathirika wa madawa ya Kulevya. Picha na Erin Bynes wa Aljazeera


Dondoo muhimu za  kuongezeka kwa matumizi ya  madawa ya kulevya  Tanzania

 • Kushuka kwa soko la Heroin dhidi ya cocaine kwa nchi za Ulaya na Amerikani na hivyo kufanya wazalishaji na  wasambazaji kutafuta masoko maeneo mengine.

 • Kwa mujibu wa shirika la umoja wa mataifa linalojishughulisha na kupambana na madawa ya kulevya na masuala ya kiharamia  (UNODC) inakadiriwa kwamba idadi ya watu 500,000 ni waathirika wa madawa ya kulevya.

 • Matumizi ya Heroin yalianza miaka ya 1990 na mara zote madawa hayo huingia kama madawa ghafi yenye rangi ya brown ama kahawia na kusambaa katika maeneo mfano wa Temeke, Manzese, Uwanja wa fisi na maeneo mengi jijini Dar es Salaam. Madawa haya yajulikanayo “Brownie” yanauzwa kiasi  cha shilingi 1500 kwa kete. Heroin nyeupe hujulikana kwa jina la “OBAMA”.

 • Asilimia kubwa ya watumiaji ni wapiga debe wa vituo vya mabasi ya daladala.

 • Wanawake kwa waume ambao wanajikuta ni watumiaji na hawana uwezo wa kuyanunua madawa hayo hujiingiza katika uchangudoa ili wafanikiwe adhma  yao. Wanaume wanakubali kulawitiwa mradi wapate  pesa ya kununua madawa na kuwa wadokozi na wezi mitaani.

 • Watumiaji wengi kama Stamil Hamad huanza kutumia madawa ya kulevya  kwa kuanza kuvuta bangi, Kuchanganya bangi na heroin kwa mtindo ujulikanao kama “Cocktail”, kuvuta mvuke wa heroin maarufu kama kupiga mistari ama bati, Kuvuta kwa kutumia pua “Sniffing” na kujichoma kwa kutumia sindano ambapo mtumiaji hujidunga kwa kuyaingiza madawa kupitia mishipa ya damu. Pia mtumiaji huweza kujitoa damu yake na kumdunga mwenzake ilia pate ulevi. Wanaita” kushare stimu”. Njia hii ndio njia ambayo husababisha watumiaji wa madawa ya kulevya kuambukizana virusi vya Ukimwi.


CHANGAMOTO
Asilimia kubwa ya watumiaji wa madawa ya kulevya ambao wameamua kuachana nayo hukumbana na changamoto mbalimbali katika jamii mfano kutengwa, kuitwa majina mbalimbali. Jamii kuwaona kama sio sehemu yao na kupelekea kuathirika kwa kiasi kikubwa kisaikolojia.

Hitimisho.

Jamii inatakiwa ilivalie njuga  suala la madawa ya kulevya na kuchukua hatua kwani vyombo vingi vya sharia na usalama vimelifumbia macho kutokana na ushawishi mkubwa wa fedha walionao wasambazaji, wazalishaji, na wachuuzi. Ni wakati sasa kwa vijana kuchukua hatua kwa kusema “HAPANA MADAWA YA KULEVYA NINATAKA KULITUMIKIA TAIFA LANGU”


Fuatilia undani wa makala hiyo kwa kubofya ALJAZEERA

Tizama na makala ya FRANCE 24 inayoelezea athari za madawa ya kulevya Tanzania
No comments: