Sunday, March 8, 2015

MTOTO MWENYE ULEMAVU WA NGOZI (ALBINO) AKATWA KIGANJA MKOANI RUKWA
 Na Willy Sumia,

Akithibitisha tukio hilo la kusikitisha Kamanda wa jeshi la polisi mkoani Rukwa, Jacob Mwaruanda alisema tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia Jumapili Machi 8, 2015 saa nane usiku katika kijiji cha Kipeta kata ya Kipeta wilaya ya Sumbawanga mkoani Rukwa

Alisema usiku huo, mtoto mwenye ulemavu wa ngozi, Baraka Cosmas (6) alikuwa amelala na mama yake mzazi Bi Prisca Shabani (26) watu wasiofahamika walivamia nyumba yao na kuanza kuwapiga mama na mtoto wake ambapo mama alijeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili kisha wakamkata kiganja cha mkono wa kulia Baraka na kutokomea kusikojulikana.

Alisema wakati hayo yanatokea baba mzazi wa Mtoto huyo mwenye ulemavu wa ngozi, Cosmas Yoramu (32) alikuwa amelala kwa mke mdogo katika kijiji hicho hicho cha Kipeta.

Kamanda Mwaruanda alisema msako wa kuwatafuta watuhumiwa ulianza usiku huo huo kwa kushirikiana polisi na wananchi ambapo watu watatu walikamatwa tayari wanahojiwa na jeshi la polisi ambapo majina ya watuhumiwa hayajawekwa wazi kwa sababu za kiupelelezi


Alisema mtoto Baraka amelazwa katika kituo kimoja cha afya kwa matibabu na hali yake inaendelea vizuri ambapo juhudi za kutafuta kiganja zinaendelea kwa nguvu.

No comments: