Monday, March 2, 2015

MAONI YA WANANCHI KUHUSU TAASISI ZA USIMAMIZI WA RASILIMALI ZA PAC, LAAC NA CAG.


1. Utangulizi
Je, ni kwa njia gani wananchi na wabunge wanaweza kujua kama serikali yao inatumia fedha zao ipasavyo? Kama ilivyo kwenye demokrasia nyingine, Bunge la Tanzania huunda kamati maalumu za kudumisha usimamizi wa fedha na kuhakikisha kuwa uwajibikaji kwenye uendeshaji wa shughuli za serikali unakuwepo. Kamati ya Hesabu za Serikali (Public Accounts Committee, PAC) inawajibu wa kusimamia hesabu za serikali kuu na mashirika ya umma.

Kamati ya Hesabu za Mamlaka za Serikali za Mitaa (Local Authorities’ Accounts Committee, LAAC) inawajibu wa kusimamia fedha za serikali za mitaa. PAC na LAAC zinahitaji kupewa taarifa ili ziweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

Taarifa hizi kwa kawaida hutolewa na Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu Tanzania (National Audit Office of Tanzania, NAOT), inayoongozwa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (Controller and Auditor General, CAG).

Dhamira kuu ya NAOT inasema: “Kutoa huduma bora za ukaguzi ili kuimarisha uwajibikaji na thamani ya fedha kwenye kukusanya na kutumia rasilimali za umma.”1 Ili kutekeleza jukumu
hili, CAG hutoa ripoti ya kila mwaka ya ukaguzi wa hesabu za taasisi/idara mbalimbali za serikali, ikiwa ni pamoja na wizara, mashirika ya kiserikali na mamlaka za serikali za mitaa.

Ni wazi kuwa, uhusiano wa pembetatu kati ya Bunge, Serikali na taasisi za ukaguzi ni msingi muhimu katika usimamizi wa fedha za umma. Lakini je, wananchi wa Tanzania wanafahamu kazi hizi muhimu zinazofanywa na taasisi hizi? Na je, wanaamini masuala ya fedha za umma ni mambo yanayowahusu?

Muhtasari huu unaripoti takwimu za hivi karibuni zenye uwakilishi wa kitaifa kuhusu maoni ya wananchi juu ya kazi za taasisi tatu za kitaifa za usimamizi wa fedha: PAC, LAAC na NAOT.

Takiwmu zimetokana na awamu ya 25 ya Sauti za Wananchi, utafiti wa kwanza barani Afrika wenye uwakilishi wa kitaifa unaofanyika mara kwa mara kwa njia ya simu za mkononi (Sauti za Wananchi :: Uwazi :: Twaweza.org).

Jumla ya wahojiwa 1,474 walipigiwa simu kati ya Septemba 23 na Oktoba 6, mwaka 2014. Ikumbukwe kuwa ukusanyaji wa takwimu ulianza baada yakutangazwa kustaafu kwa aliyekuwa CAG, Ndugu Ludovick Utuoh (Septemba 15, 2014) na ulikamilika kabla ya kuwasilishwa kwa ripoti ya Escrow Bungeni (26 Novemba 2014) na kabla ya uteuzi wa CAG mpya, Profesa Mussa Juma Assad.

Matokeo muhimu ni:

• Zaidi ya mwananchi mmoja kati ya kumi anatambua au anaweza kuelezea kwa usahihi kazi za taasisi mbalimbali za usimamizi.

• Wananchi tisa kati ya kumi wanaamini rushwa ipo serikalini.

• Wananchi wawili kati ya watatu wanaamini kuwa taasisi za ukaguzi na usimamizi haziko huru kama inavyotakiwa.

• Wananchi saba kati ya kumi wanafikiri kuwa rushwa ni upotevu wa fedha “zao wenyewe”.

• Mtanzania mmoja kati ya watatu angependa matokeo ya ukaguzi yajadiliwe moja kwa
moja kwenye vipindi vya redio kila wiki.

2. Mambo saba kuhusu ufahamu wa wananchi juu ya taasisi za serikali za ukaguzi wa hesabu na usimamizi


Jambo la 1: Mtu mmoja kati ya watatu anafahamu mifumo ya uwajibikaji

Watu wengi hawajawahi kusikia kuhusu Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali
(CAG), Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), na Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali
za Mitaa (LAAC).

Mwananchi mmoja kati ya watatu ameshawahi kusikia kuhusu CAG, lakini ni mmoja tu kati ya sita anayeweza kuelezea shughuli za CAG (Kielelezo cha 1). Vile vile, takriban mwananchi mmoja tu kati ya wanne amewahi kusikia kuhusu PAC na LAAC, na mmoja kati ya kumi anaweza kuzielezea vyema taasisi hizi (Kielelezo cha 1).


Pia wahojiwa kwa kiasi kikubwa hawakuweza kutaja kwa usahihi majina ya wakuu wa taasisi hizi: asilimia 12 walitaja kwa usahihi jina la Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu, Ludovick UtouhKwa ujumla, makundi ya wasomi, watu wenye kipato kikubwa na wanaume waliohojiwa walionekana kuwa na taarifa zaidi kuhusu ofisi hizi tatu (takwimu hazijaoneshwa).


Jambo la 2: Wananchi wengi hawakumbuki mafanikio ya ofisi hizi

Vile vile, wananchi wengi ambao wanazifahamu taasisi hizi hawakuweza kukumbuka mafanikio yoyote yaliyopatikana ndani ya ofisi hizo tatu kati ya kipindi cha miaka mitatu iliyopita. Wahojiwa wengi hawakuweza kubainisha mafanikio yoyote.

Hata hivyo, wananchi wachache sana (kati ya 5% na 6%) waliamini kuwa ofisi hizi hazina mafanikio kabisa (Kielelezo cha 2). Hili linashabihiana na viwango vya chini vya ufahamu wa kashfa za rushwa – nyingi kati ya hizo zimeibuliwa na kuandikwa na Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu na taasisi za usimamamizi - kama ilivyooneshwa kwenye takwimu za muhtasari uliopita kuhusu rushwa.

Ikumbukwe kuwa takwimu za muhtasari huu zilikusanywa kabla ya kuwasilishwa kwa ripoti ya Escrow Bungeni (ambayo ilianza Novemba 2014). Ripoti ya Escrow ingeweza kuathiri matokeo yaliyowasilishwa hapa.Jambo la 3: Wananchi wawili kati ya watatu hawaamini kuwa taasisi za ukaguzi wa hesabu ziko huru

Moja ya sifa muhimu ya taasisi yoyote ya ukaguzi ni uhuru wake kamili kwa vyombo na taasisi za dola ambazo inazikagua. Bila uhuru kamili, ubora na mbinu za mchakato wa ukaguzi hauwezi kuwa wa uhakika.

Watanzania kwa kiasi fulani wana wasiwasi juu ya uhuru wa CAG, PAC na LAAC. Karibu mtu mmoja kati ya watatu anaamini CAG yuko huru “kwa kiasi kidogo”, na mwananchi mmoja kati ya watatu anaamini CAG yuko huru kwa”kiasi fulani”, na mtu mmoja kati ya wanne anaamini kuwa CAG yuko huru kwa kiasi kikubwa (Kielelezo cha 4).

Mgawanyiko huu wa maoni unafanana pia kwa PAC na LAAC. Hii ina maana kuwa wananchi wawili kati ya watatu wanaamini kuwa taasisi za ukaguzi wa hesabu hazina uhuru kamilifu.
Jambo la 4: Wananchi tisa kati ya kumi wanaamini rushwa ipo serikalini

Walipopewa orodha ya mazingira ya kubuni yanayohusiana na aina mbalimbali za rushwa serikalini, idadi kubwa ya wananchi (zaidi ya 50% katika kila suala) inaamini masuala haya hufanyika kiuhalisia serikalini.

Hata hivyo,wananchi wachache sana wanafikiri kuwa masuala haya yatajitokeza kwenye ripoti ya CAG. Hivyo basi, Watanzania wengi wanaamini kuwa rushwa hairipotiwi kikamilifu kwa kiwango inachotendeka.

Kwa mfano, takriban wananchi tisa kati ya kumi wanaamini kuwa makampuni hutoa rushwa kwa viongozi wa serikali ili kushinda zabuni/mikataba - lakini ni wananchi 34% tu wanaoamini kuwa aina hii ya rushwa huandikwa na kuonekana kwenye ripoti ya CAG (Kielelezo cha 5). Tunaweza kubashiri kuwa hili limetokana na wananchi kupata ugumu wa kugundua aina hii ya rushwa.

Vile vile, wananchi nane kati ya kumi wanaamini kuwa kuna mishahara inalipwa kwa wafanyakazi hewa, na karibu 50% wanaamini taarifa hii huandikwa kwenye ripoti ya CAG (Kielelezo cha 5).

Jambo la 5: Wananchi saba kati ya kumi wanatambua kuwa rushwa ni upotevu wa fedha zao

Masuala matatu mahususi yalielezwa kwenye ripoti ya CAG ya mwaka 2012/2013. Masuala haya ni:

1. Mwezi Septemba 2012, magari 11 ya ofisi yalinunuliwa na Wizara ya Viwanda na Biashara kwa ajili ya mradi wa TradeTan. Magari haya hayakununuliwa kabisa.

2. Makusanyo ya mapato kutoka Halmashauri 31 za Serikali za Mitaa (LGAs) yanayofikia kiasi cha shilingi za Kitanzania 585,500,000 (takriban dola za Kimarekani 351,000) hayakupelekwa benki wala kupelekwa katika mamlaka za Serikali za Mitaa.

3. Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) ilitumia shilingi bilioni 2.5 (takriban dola za marekeni milioni 1.5) kununua mita nane za pampu za mafuta. Mita hizi zilikataliwa mara tu baada ya kununuliwa maana zilikuwa hazifai.

Tuliyaelezea matukio haya matatu kwa wahojiwa. Kisha tukauliza swali: katika matukio haya matatu, kwa maoni yako, ni fedha za nani zilizopotea? Wananchi saba kati ya kumi (69%) wanaamini ni fedha zao ndizo zimepotea (Kielelezo cha 6).

Zaidi ya hayo, wananchi nane kati ya kumi wanaamini kuwa matukio haya yanawaathiri wao kwa “kiwango fulani” au “kiwango kikubwa” (Kielelezo cha 7).

Pia tuliwauliza wahojiwa ni suala gani kati ya haya matatu wangependa kupata taarifa zakezaidi. Idadi kubwa ya wahojiwa (41%) walitamani sana kusikia zaidi kuhusu upotevu kwenye halmashauri (takwimu hazijaoneshwa). Hii inaweza kuonesha matukio ya papo kwa papo kuwa kodi za Serikali za Mitaa, kwa wananchi wengi, huathiri moja kwa moja jamii zao.Jambo la 6: Wananchi sita kati ya kumi wanatarajia Rais achukue hatua dhidi ya vitendo vya rushwa

Takwimu za muhtasari wa utafiti wa Sauti za Wananchi uliochapishwa huko nyuma unaonesha kuwa Watanzania 71% wana imani na Rais kwa kiwango “fulani” au “kikubwa”.

Sambamba na hilo, karibu wananchi sita kati ya kumi (57%) wanaamini kuwa Rais anapaswa kuchukua hatua kutokana na matokeo ya ubadhilifu yaliyoripotiwa kwenye ripoti ya CAG ya mwaka 2012/2013 (Kielelezo cha 8).

Kwa kulinganisha, mwananchi mmoja kati ya ishirini (5%) anaamini kuwa kamati za usimamizi – PAC na LAAC – zinapaswa kuchukua hatua, ingawa mwananchi mmoja kati ya kumi (13%) anafikiri kuwa wananchi wa kawaida ndiye wangepaswa kuchukua hatua.


Je, ni hatua gani wananchi wanatarajia zichukuliwe dhidi ya wale wanaokutwa na hatia ya rushwa na vitendo vingine kinyume na sheria vilivyoelezwa kwenye ripoti ya CAG? Wananchi watatu kati ya kumi (32%) wanasema wale wanaokutwa na hatia ni lazima wafukuzwe kazi, na watatu kati ya kumi (30%) wanasema mtu anayepatikana na hatia anapaswa kulipa fedha alizoiba (Kielelezo cha 9). Wahojiwa wachache sana ndio walisema wanaokutwa na hatia wafungwe, wapewe onyo kali au waondolewe kwenye ofisi za umma.Jambo la 7: Redio ni chombo maarufu zaidi katika kusambaza Taarifa kuhusu michakato ya ukaguzi wa hesabu za serikali 

Kama tulivyoona kwenye Jambo la 1, Watanzania wengi hawafahamu vizuri taasisi za serikali za ukaguzi na usimamizi wa hesabu za serikali, pamoja na mafanikio ya ofisi hizo.

Hata hivyo, hii haimaanishi kuwa hawana shauku ya kutaka kujua. Kinyume kabisa, zaidi ya nusu wanaamini kuwa matokeo ya ripoti ya CAG yana athari za moja kwa moja kwao (Jambo la 5).

Hivyo, ni kwa jinsi gani Watanzania watajifunza zaidi kuhusu matokeo haya? Walipoulizwa jinsi ya kushughulikia kukosekana kwa ufuatiliaji wa matokeo ya ripoti ya CAG, na jinsi ya kusambaza matokeo ya CAG kwa wananchi wengi, wahojiwa walitaja kuwa redio ndio njia yenye ufanisi zaidi.

Karibu mwananchi mmoja kati ya watatu aliamini kuwa kianzishwe kipindi cha redio ya nusu saa kila wiki kujadili matokeo ya ukaguzi na ufuatiliaji wake (Jedwali la 1).

Vile vile, njia iliyopendelewa zaidi katika kusambaza matokeo ya ripoti ya CAG kwa jamii ni kutangazwa moja kwa moja redioni ripoti ya CAG inaposomwa Bungeni (wananchi 57% walilisema hili).

 Njia nyingine muhimu zaidi iliyopendekezwa ni kuanzishwa kwa chombo kipya kitakachofuatilia ripoti za ukaguzi wa hesabu za serikali - hili lilipendekezwa na wahojiwa 27% (Jedwali la 1).
Vile vile, njia iliyopendelewa zaidi katika kusambaza matokeo ya ripoti ya CAG kwa jamii ni kutangazwa moja kwa moja redioni ripoti ya CAG inaposomwa Bungeni (wananchi 57% walilisema hili).

3. Hitimisho
Muhtasari huu unaripoti matokeo ya hivi karibuni ya ufahamu wa wananchi juu ya mifumo ya usimamizi wa fedha nchini Tanzania na maoni kuhusu rushwa, ukaguzi wa hesabu na uwajibikaji.

Kinachoonekana wazi kabisa ni kwamba taasisi tatu za kitaifa za usimamizi na mafanikio yao hazijulikani vizuri kwa wananchi wengi. Wakati huo huo, vyombo hivi vya usimamizi vinashughulikia masuala ambayo wanayataka wananchi na yanagusa maisha yao.

Karibu mwananchi mmoja kati ya watatu (31%) angependa matokeo ya ukaguzi wa hesabu yajadiliwe kwenye redio kila wiki.

Hususan, wanaposikia kuhusu matukio halisi ya rushwa kama yalivyoelezwa kwenye ripoti ya CAG ya mwaka 2012/2013, wananchi wanasema wanahisi kuathirika na ubadhilifu huo maana fedha zao ndizo hutumiwa vibaya. Je, matumizi mabaya haya yashughulikiwaje? Wananchi wengi (57%) wanaona Rais ndiye anayepaswa kuchukua hatua. Wananchi wachache wanafikiri kuwa taasisi nyingine, kama vile Baraza la Mawaziri (16%) na Mahakama (11%) vinapaswa kuchukua hatua dhidi ya rushwa na ubadhilifu.

Hili halitofautiani sana na wananchi 13% ambao wanaoema wananchi wa kawaida wanapaswa kuwajibika kuchukua hatua kwenye hoja za ukaguzi zisizopatiwa ufumbuzi.

Matokeo mengine muhimu ni kwamba wananchi wanaonekana kwa kiasi fulani kusamehe yale yanayoonekana kuwa makosa ni makubwa ya jinai. Kwa mfano, wananchi wachache sana wanasema kuwa viongozi wala rushwa lazima wafungwe au wafukuzwe kwenye ofisi za umma.

Hili linaibua suala la uwajibikaji na kinga ya kuadhibiwa kisheria: wahojiwa wengi wanakubaliana kuwa bila adhabu kali za kisheria, motisha kwa viongozi kuwa waaminifu inashuka na uwajibikaji utaendelea kuwa jambo la kufikirika tu. Pia kama maoni ya wananchi hayadai adhabu kali kwa vitendo vya rushwa, viongozi wa umma wanauwezekano wa kutokabiliwa na adhabu sahihi na wataweza kuendelea na mtindo wa kutumia vibaya fedha za umma ‘kama walivyozoea’.

Kinyume cha hili, aina hii ya msamaha haitumiki kwenye makosa yanayoibuka ndani ya jamii, kama vile wizi wa mitaani unaofanywa na vibaka. Sauti za Wananchi iliripoti huko nyuma kuwa, wezi ndani ya jamii mara nyingi hukumbana na ukatili/adhabu kali inayotokana na wananchi wenye hasira.

Ingawa ukimya wa kushughulikia rushwa ni vigumu kuuelezea, uwezekano mojawapo ni kwamba wananchi wana imani ndogo na utayari wa taasisi za serikali kushughulikia kesi hizi. Hii inahusu taasisi tatu za ukaguzi wa fedha na vyombo vingine vya usimamizi lakini pia kwa uwazi kabisa inahusiana na imani ndogo kwa polisi na mahakama.

Wananchi wanaziona taasisi ni miongoni mwa taasisi za serikali zilizokithiri kwa vitendo vya rushwa. Ili taasisi yoyote kati ya hizi iwe ya usimamizi wa fedha au sheria, iweze kufanya kazi kwa ufanisi hutegemea utashi wa kisiasa na mwenendo mwema ndani ya taasisi zenyewe.

Isitoshe, wananchi wanaweza kutilia shaka uwezo wa taasisi hizi kwenye suala hili.

Kwa mfano, katika orodha ndefu sana ya hoja za ukaguzi katika ripoti yake ya mwaka 2012 - 13 juu ya taarifa za fedha za Serikali Kuu7, CAG alibaini malipo yaliyozidi kwa ajili manunuzi ya bidhaa katika Ofisi ya Waziri Mkuu, na bidhaa/vifaa vilivyotaifishwa na jeshi la polisi vilikosekana kituo cha polisi . Hivyo, wananchi wako sahihi wanapokuwa na wasiwasi juu ya nani atachukua hatua dhidi ya vitendo vya rushwa.

Aidha, CAG amekuwa akiripoti kuhusu ukiukwaji wa taratibu za matumizi ya fedha za umma kwa miaka mingi, na mara nyingi masuala anayoyaibua hayatatuliwi wala kufanyiwa kazi.

Ripoti ya mwaka 2012-13 inaonesha kuwa kati ya mapendekezo 960 ya CAG mwaka uliopita, ni mapendekezo 401 tu (42%) ndiyo yaliyotekelezwa kikamilifu na Wizara, idara za Serikali na Mashirika ya Kiserikali (MDA), jambo lililosababisha kuendelea kuwepo kwa orodha ndefu ya hoja za CAG zenye jumla ya thamani ya fedha za Kitanzania Sh 636,849,769,109 (karibu dola za Kimarekani 368).

Kiasi hiki, kama kingerudishwa, kingetosha kugharamia 5% ya jumla ya matumizi ya Serikali mwaka wa bajeti 2012-13. Au, kingeweza kulipa mishahara ya walimu wa shule za msingi wapatao 116,294 kwa mwaka mzima.

Tunaweza kuuliza: kama matokeo ya ukaguzi yanapuuzwa, kwa nini tufanye ukaguzi? Lakini ukweli ni kwamba 42% ya mapendekezo CAG yalitekelezwa kikamilifu kama ilivyoelezwa kwenye ripoti ya mwaka 2012-13. Kwa upande mwingine mtu anaweza kusema kuwa, bora nusu shari kuliko shari kamili, bila ripoti ya CAG hali ya matumizi ya fedha ingekuwa mbaya zaidi. Hivyo, kila pendekezo linalotekelezwa linapaswa kutambuliwa na kupongezwa.

Swali muhimu si kama hesabu na matumizi ya rasilimali lazima vipitiwe upya maana hili ndilo sharti la msingi la kuonesha kwamba uwajibikaji upo. Ni muhimu zaidi kuuliza ni jinsi gani ukiukwaji wa taratibu, mapendekezo ya ukaguzi na wizi wa fedha za umma vinaweza ushughulikiwa ili visijirudie tena kama ilivyo sasa.

CAG huandika: “Kwa kutoa uchunguzi wa kiukaguzi na mapendekezo, lengo kuu la CAG ni kuboresha utendaji na kuongeza uwajibikaji wa Wizara, idara na mashirika ya kiserikali. Si jukumu la CAG, na wala CAG hana mamlaka, yakulazimisha utekelezaji wa mapendekezo haya.

Jukumu la msingi la utekelezaji wa mapendekezo ya ukaguzi liko kwa Maafisa Maduhuri wa Wizara, idara na sekretarieti za mikoa.”

Mwisho wa siku, uwajibikaji na uwazi unahitaji zaidi ya maafisa maduhuri. Kinachotakiwa ni maadili ya uongozi katika ngazi zote, na kuwekwa kwa masharti magumu ambayo yatawagharimu wale wanaofuja fedha za umma.

Masharti hayo lazima yawe kwenye mfumo wa adhabu kali kwa mujibu wa sheria, bila kutekeleza adhabu kikamilifu, kazi za taasisi za usimamizi hazitakuwa na manufaa, licha ya bidii kubwa iliyotumika kufanya ukaguzi.


Nani ataonesha mfano?

No comments: