Wednesday, February 18, 2015

NDUGU ZANGU NIFAHAMISHENI NIMWOKOE NANI.
Na Baraka Mfunguo,

Hodi hodi waungwana, pamoja nanyi watwana
Nina swala pana, tuulizane na kujadiliana
Niwaulizeni  mabwana,  bila kutofautiana
Ndugu zangu nifahamisheni nimwokoe nani.Katikati safarini, mimi na familia yangu
Tukiwa mtumbwini, mke  na mwanangu
Baba  mama safarini,  tukielekea  mwangu
Ndugu zangu nifahamisheni nimwokoe nani.
Ghafla ikajitokeza ,dhoruba kali na mawimbi
Baba  mama ikawokoteza, mke  mithili ya vumbi
Mwanangu ikampoteza , bahari ikavuma wimbi
Ndugu zangu nifahamisheni nimwokoe nani. Baba  mama yangu, mke naye mwanangu
Wote ni damu yangu,  wastahiki msaada wangu
Mama  kimbilio langu, penye taabu na shida zangu
Ndugu zangu nifahamisheni, nimwokoe nani.Mke  mwanangu walia, baba  mama wakihemea
Bahari haitowavumilia,  wimbi lawachekea
Nafsi  yaumia,   upepo  wawapepetea
Ndugu zangu nifahamisheni, nimwokoe nani.Ndugu zangu nisaidieni,  nikate shauri,
Bahari hazifanani,  kwa  wajuvi   mahiri
Baba mama wa thamani, mke   mwanangu najishauri
Ndugu zangu nifahamisheni nimwokoe nani.Wenye hekima na busara, mfanye maamuzi
Walio msimamo imara, kutoa utatuzi
Baba  mama ni bora, mke  mwanangu   vipenzi
Ndugu zangu nifahamisheni , nimwokoe nani.Kalamu niiweke, nasubiri yenu majayabu
Busara  nizipokee, nizitafakari kwa  adabu
Uamuzi nitolee , kwa hekima za mababu
Ndugu zangu nifahamisheni, nimwokoe nani.


-Shairi limebuniwa kutoka wimbo wa Bendi ya  NUTA JAZZ (1970) “  Ndugu zangu nifahamisheni ,Nimwokoe nani?” Ni fumbo ambalo lanitatiza  tangia udogo wangu mpaka sasa. Latufundisha dhahiri shahiri katika vipaumbele vyetu vya maisha na maamuzi yetu. Ni hekima ambayo imejificha.

No comments: