Monday, February 9, 2015

MNYUKANO KWENYE TWITTER BAINA YA WANASIASA WA TANZANIA NA KENYA


Na Baraka Mfunguo,

Sakata la magari ya watalii kutoka Tanzania kuzuiliwa Kenya yameleta sura mpya, baada ya baadhi ya wanasiasa kuonyesha hisia zao za wazi wazi mtandaoni. Inavyoelekea wenzetu Wakenya wame-capitalize kwenye udhaifu fulani ambao ni  miundombinu hususan viwanja vya ndege, na usafiri wa anga kama vile kuwa na kampuni imara ya usafiri wa ndege. Binafsi kama mtanzania linaniumiza kwa sababu linagusa maslahi ya nchi yangu. 

Lakini ninaamini ikiwa tutajiimarisha vizuri kimkakati na kuwa na dira yakinifu kiushindani tutafika.  Suala hili sio la mtu mmoja mmoja ni suala linalogusa maslahi ya nchi zote mbili Kenya na Tanzania majadiliano ni bora zaidi na yakishindikana, itafutwe njia nyingine kama vile kuuimarisha uwanja wa KIA pamoja na viwanja vingine vya ndege mfano kuweka viwanja vikubwa vya ndege Tanga, Dodoma, Mwanza na Arusha. Kuanzisha ama kuifumua upya ATCL na kuifanya iwe ya kiushindani zaidi bila ya kutegemea ruzuku serikalini wala kuingiliwa na serikali, kuwa na mkakati wa kuhamasisha watanzania kuitangaza na kujifunza juu ya vivutio mbalimbali vya nchi yao na kuweka uzalendo wao mbele kwa maslahi ya nchi yetu ya Tanzania.  Siamini katika mkakati wa kufaidisha makampuni ya ndege ya kiarabu ninaamini katika mkakati wa biashara ya ushindani na kuwa na kitu chetu tutakachokitumia na kukithamini sote. Naamini pia kadhia hii na wenzetu Wakenya itakwisha kwani kuna mambo mengi ya maendeleo yanayohitaji ushirikiano wao nasi kama nchi za Afrika Mashariki. Nachukua hatua hii kumpongeza ndg. Zitto Kabwe na wengineo walioonyesha uzalendo katika kutetea  maslahi ya nchi yao. KIINI CHA TATIZO  • Mkataba wa mwaka 1985 unaozuia magari ya utalii kutoka Tanzania  kuhudumu katika hifadhi za Taifa na viwanja vya ndege. Mkataba huo unaeleza kwamba magari ya kampuni yanayojihusisha na biashara ya utalii katika nchi zote yanatakiwa kuwashusha abiria wake mipakani mathalan Lunga Lunga, Taveta, Namanga na Nyakiyakaye kwa upande wa  Kenya na   magari ya Tanzania kushusha watalii katika mipaka ya  Horohoro, Himo, Namanga na Sirare. 

  • Wakenya wanadai magari ya shughuli za utalii kutoka Kenya yanazuiliwa katika baadhi ya mikoa na miji ama majiji isipokuwa Tanga, Arusha, Moshi na Musoma wakati wao wanaruhusu magari ya utalii kutoka Tanzania katika miji  ama majiji yote nchini Kenya.

  • Gati la Bologonja linalotenganishwa na mto wa Mara dhidi ya Mbuga ya Masai Mara Kenya  na Serengeti upande wa Tanzania kufungwa na kuwafanya  wale wanaohitaji kuingia na kuona wanyama upande wa Tanzania  kutokea Kenya kutokuwa na mwanya huo.

  • Upande wa Tanzania kupinga kupitia Waziri wake kuwa makubaliano ya mwaka 1985 baina ya Kenya na Tanzania hayahusishi viwanja vya ndege (Kwa mujibu wa gazeti la Standard la Kenya la January 25th 2015 lililoandikwa na  Luke Anami na Nicholas Waithathu )

  • Mgogoro wa kimaslahi baina ya makampuni ya utalii ya Kenya na Tanzania kuhusiana na msimamo wa Tanzania katika pembetatu ya mbuga maarufu za Kenya zinazopakana pia na Tanzania za Mara, Serengeti na Tsavo. Msimamo wa Tanzania  ndio unaowatia hofu kubwa Wakenya. Wakenya wanaamini kwamba wao walilegeza kamba katika mkataba wa kiitifaki wa 1985 na kwamba mkataba huo umetumika kama fimbo ya kuyaadhibu makampuni yanayofanya shughuli za utalii Tanzania kuingia uwanja wa kimataifa wa Jomo Kenyatta. Hata hivyo imeelezwa kwamba mkataba huu wa 1985 unatarajiwa kufanyiwa tathmini na marekebisho miezi sita ijayo.

2 comments:

Mbele said...

Tanzania tulipaswa tuwe na ndege zetu, tangu miaka iliyopita, zinaruka hadi ughaibuni kuleta na kupeleka watalii. Nini kilituzuia. Au ni ufisadi? Ukipanda ndege ya Ethiopian Airlines, kwa mfano, unajionea jinsi wanavyoitangaza nchi yao humo ndani ya ndege.

Pamoja na rasilimali zetu nyingi hizi, imekuwaje tusiwe na ndege angalau mbili zinazofika Ulaya au Marekani, wakati mafisadi wanachota mabilioni na kwenda kuyaficha kusikojulikana na kunakojulikana? Yaani mpaka tukumbane na mgogoro na Kenya ndipo tupate akili?

A. Massawe said...

Nilitarajia wanasiasa na viongozi wa serikali pande mbili husika kwenye mgogoro wangebakia kuwa mstari wa mbele kwenye kutafuta suluhu itakayokubalika na pande mbili husika na siyo miongoni mwa walalamikaji na wanaonyosheana vidole mitandaoni. Wanasia na viongozi wa serikali kuwa miongoni miongoni mwa wanaolalamika na kuwanyoshea vidole wenzao wa nchi jirani husika ni ukiukwaji wa maadili ya uongozi na kujidhalilisha mbele ya macho ya walimwengu. Jukumu la viongozi ni kutatua migogoro na sio kuikuza kwa njia ya malalamiko dhidi ya wenzao wa nchi jirani husika.