Saturday, February 21, 2015

MAUAJI YA YOHANA BAHATI NA KILELE CHA UNAFIKI WA SERIKALI.Na Baraka Mfunguo,

MABAKI ya mwili wa mtoto mwenye ulemavu wa ngozi, Yohana Bahati  ambaye alitekwa Februari 16, mwaka huu na kuuawa kwa kukatwa mikono na miguu,  yalizikwa kaburini chini ya ulinzi mkali wa polisi.

Mazishi ya mtoto huyo yalifanyika saa tisa alasiri katika Kijiji cha Ilelema, Wilaya ya Chato, mkoani Geita, huku polisi wakiwa wameimarisha ulinzi.

Mabaki ya mwili wa mtoto huyo yalipelekwa kwanza nyumbani kwa babu yake, Misalaba Manyamche, saa sita mchana kabla ya kuanza kwa msafara wa kuelekea makaburini ulioongozwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Geita, Joseph Konyo. Katika msafara huo pia walikuwepo viongozi wa mashirika mbalimbali yasiyo ya kiserikali.

Licha ya Kijiji hicho kuwa porini na kutokuwapo na idadi kubwa ya watu, vilio vya ndugu na jamaa wa mtoto huyo na shughuli ya maziko ya mwili wake ilifanywa na askari polisi walioongozwa na Konyo.

Kama tujuavyo, na kama ilivyo silika kwa watanzania wote na utamaduni wao/wetu. Tumekuwa na utamaduni wa kushiriki katika misiba mbalimbali. Lakini ni lazima ikumbukwe kwamba sio wote wanaoshiriki kwenye misiba ni waombolezaji. Wapo wale ambao wanataka kujionyesha ili umma uone namna gani walivyoguswa na msiba na pia wapo hata wauaji ambao kwa namna moja ama nyingine ni kutafuta taarifa ili kujua kitu gani kinaendelea ili waweze na wao kubuni mbinu na mikakati ya kujikwamua.

Serikali kupitia jeshi la Polisi, Wanasiasa na Wanaharakati wameonyesha unafiki mkubwa na wanachotaka kutuonyesha watanzania ni kama machozi ya Mamba yale ambayo mtu anaonyesha anaomboleza lakini moyoni anachekelea. Kinachofanyika kupitia jeshi la polisi na wanasiasa, ni kujaribu kutafuta njia ya kuepa upepo mbaya utakaoweza kutokea haswa ikizingatiwa hisia za wananchi ziko juu. Na serikali haitaki msuguano wowote kwa  maana ya ukweli wowote uwekwe wazi kwa kigezo cha amani na utulivu.

Hii amani mnayoizungumzia iko wapi wakati watu wanawindana kila kukicha. Hatuwezi kukubaliana na hadithi za Alinacha ambazo zinataka kuficha na kupotosha ukweli. Ni lazima tuamini kwamba mtandao huu wa wahusika wa mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi yaani Albino, ni mkubwa sana. Unawahusisha hata hao polisi wenyewe huwezi ukautenga mtandao kwa njia nyepesi njia madhubuti zinahitajika kufanyika. Na njia hizo ni kwa wananchi kusema IMETOSHA.

IMETOSHA, ni kauli ambayo si Polisi wana wanasiasa wetu wangependa kusikia masikioni mwao. Ni kauli ambayo inawatisha na kuwaogopesha lakini ndio ukweli na ukweli hauwezi kukwepeka. Kwa kipindi kirefu sana wananchi wamekuwa walilalamika hususan walemavu wa ngozi na wengi wetu tumekuwa kama tumetia pamba masikioni ni kana kwamba yale ambayo wanakumbana nayo hayatuhusu na wala hayatugusi. Sasa IMETOSHA, kwa kigezo cha kila mtu anastahili uhai, heshima na haki ya kuishi popote pasipo kujali hali yake. Serikali imekuwa ikitoa matamko, Wanasiasa matamko, Wanaharakati matamko, na watu wa vijiweni matamko. Tutaendelea kutoa matamko juu ya matukio kama haya mpaka lini?

Ni suala lisilokubalika na haiyumkiniki wapo wale ambao wameona picha ya mtoto Yohana Bahati mtoto asiyekuwa na hatia alivyokatwa kwa mapanga na kuona ni jambo la kawaida kabisa. Na kujifanya wameguswa na kutaka wajionyeshe katika mitandao namna walivyoguswa na kulizungumzia kwa hisia kali ili waonekane wameguswa. Wengine wameenda mbali kabisa haswa wanaharakati na kwenda kwa mama mzazi wa Yohane na kupiga naye picha. Haikatazwi na sio dhambi, lakini matatizo ya hawa wenzetu yasigeuzwe mradi wa watu kujitajirisha na kuvimbisha matumbo yao.

Mwingine akiona Albino kakatwa panga anapatwa kama na wazimu fulani maana anajua kwamba ndio wakati muafaka wa ile "proposal" yake kuiandikia ili apate posho ya kuendeshea ka asasi kake uchwara.  Kwa nje anaonekana kama ni mtu mnyofu na mwaminifu kweli kweli lakini moyoni ameoza. Na ndivyo wanasiasa wetu walivyo na wanavyotufanya. Tunageuzana mitaji hivi hivi huku tunajiona. IMETOSHA


Hii serikali sio sikivu kama wengine tunavyodhani. Hii changamoto ya mauaji ya ndugu zetu wa ulemavu wa ngozi inawashinda je hayo mengine tusemeje? Kutwa kucha wako katika meza za siri wakijadiliana na kuwahonga na kuwanunua wale  ambao wataonekana ni vinara wa kudai suala hili. Wao hawataki kuwajibika wanataka suala  hili lipite kwa ajili ya kulinda maslahi yao kwa kigezo cha usalama na amani ya nchi. Haiwezekani hapa lazima kieleweke. IMETOSHA


Mwisho nimalize kwa kusema. Leo analengwa Albino, kesho inawezekana ikawa wewe, mimi na yule. Na kama unadhani huu unaosemwa ni uongo ama uchochezi puuzia na usichukue hatua siku si nyingi utakuja kujutia. Mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi Albino yanatuhusu sote. Mimi , wewe na yule . Serikali inajenga utamaduni wa kikafiri wa kutojali na kuwabagua wengine na kuwaona kama sio sehemu ya jamii. Albino ni wewe na mimi na wapo ambao wamefanya na wanafanya makubwa zaidi ya wewe unayejitia kwamba mauaji haya si sehemu yako. Wanasiasa wamegeuka kuwa manyang'au wao wanawatumia kama mtaji wao wa kisiasa na kama njia yao ya kisiasa na wakati huo huo wanajifanya kuguswa na vitendo vibaya vya kihalifu. Sio kweli. Tuache tabia ya kuwatumia wenzetu kama mitaji ya kisiasa. IMETOSHA


1 comment:

Mbele said...

Umesema ukweli mtupu. Ni uwongo kudai kwamba Tanzania ni nchi ya Amani, wakati hao wa-Tanzania wenzetu albino wanaishi katika kihoro muda wote, kama vile wamo katika msitu wa wanyama wakali.

Na serikali inahusika moja kwa moja na uhayawani huu. Miaka michache iliyopita, Vicky Mtetema alifanya utafiti kidogo tu na akaweza kuwanasa baadhi ya waganga wanaoendesha uhayawani huu.

Vicky Mtetema ni raia tu, wala hana vyombo vya dola. Iweje serikali, yenye macho na masikio katika kila kona ya nchi, na vyombo vya dola kila mahali, idai kwamba inashindwa kukomesha uhayawani huu?

Inajulikana kuwa baadhi au wengi wa hao tunaowaita viongozi ndio ngome ya ushirikina. Kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi ni kipindi ambacho vitendo vya kishirikina vinashamiri, kwa mujibu wa wachunguzi wengi.

Serikali hii ya CCM inazembea suala hilo. Na mtafiti Vicky Mtetema amenukuliwa akisema kuwa serikali inalegalega katika suala hilo. Kama serikali haiwezi au haitaki kuwajibika, ni muhimu na wajibu kwa wapiga kura kuitosa jalalani.