Saturday, February 7, 2015

MAHAKAMA YA KADHI: TANZANIA INAANZA KUVUNA MATUNDA YA KUIKATAA HISTORIA YA KWELI.Na Mohamed Said, ( Bandiko Kutoka JAMII FORUMS).

Mtu yoyote hii leo ikiwa ataingia katika mitandao ya kijamii na kusoma mjadala unaofanyika kuhusu Mahakama ya Kadhi ni lazima atapata mshtuko mkubwa kutokana na lugha kali na wakati mwingine matusi kati ya hao wanaojadiliana. Kila upande ukitupa shutuma na maneno makali dhidi ya upande mwingine. Ukipitia majadiliano yote kitu kimoja kinachojitokeza wazi na dhahiri kabisa ni kuwa kuna mpasuko mkubwa kati ya Waislam na Wakristo kuhusu Mahakama ya Kadhi. Chuki na uadui sasa upo wazi bila kificho.

Hili linawezekana vipi wakati viongozi wetu wanatuambia kuwa Baba wa Taifa alituachia misingi imara ya umoja? Wahenga wamesema dalili ya mvua ni mawingu. Suali la kujiuliza ni hili, wapi sisi kama taifa tumejikwaa? Wengi katika hao wanaojadili hiyo Mahakama ya Kadhi ukweli ni kuwa hawaijui vyema historia ya Tanzania au ukipenda Tanganyika. Wengi katika hawa waliojizinga katika malumbano haya baadhi ni watu wazima walio na umri zaidi ya miaka 50 na vijana ambao wamezaliwa baada ya Tanganyika kupata uhuru wake mwaka 1961. Mjadala unafanyika katika mazingira ya ujinga wa kutojua historia. Sasa hapa linakuja swali imekuwaje kuwa watu hawa ambao kwa sasa ndiyo wengi katika jamii yetu hii leo hawaijua historia ya nchi yao?

Vipi tumekuwa na Chuo Kikuu kwa karibu ya nusu karne na sasa vimeongezeka vingine vingi lakini hadi sasa ikawa historia yetu ni ya kubabaisha haijakaa sawa hadi leo? Mimi sitatoa jibu kwa sasa ingawa jibu ninalo. Huko vyuoni ni historia gani inasomeshwa ambayo inawafanya watu wasijijue?

Baadhi ya wachangiaji katika hiyo mitandao ya kijamii na inaelekea hao ni Wakristo wanasema iweje Mahakama ya Kadhi igharimiwe na serikali ilhali serikali hii haina dini? Waislam wanaleta jibu wakisema mbona serikali inatoa mabilioni kila mwaka kwa makanisa kuhudumia taasisi zao kupitia “Memorandum of Understanding (MoU)?” Kwa wale ambao labda hawaujui huu mkataba ni kuwa mwaka wa 1993 Serikali ya Tanzania ilitiliana sahihi mkataba na makanisa, mkataba uliokuja kujulikana kama Memorandum of Understanding.

Makubaliano ambayo serikali iliridhia na kuidhinisha elimu, huduma za jamii na afya ziendeshwe na Christian Council of Tanzania (CCT) na Tanzania Episcopal Conference (TEC) kwa kushirikiana na serikali. Mkataba huu ulitayarishwa na Dr. Costa Mahalu, wa Kitivo cha Sheria Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam na ukatiwa sahihi na Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Edward Lowassa. Kikubwa katika mkataba huu kwanza ni ule usiri uliogubika mpango mzima na pili ni kuwa ulitiwa sahihi bila ya kuwashirikisha au kuwafahamisha Waislam.

Ili makubaliano haya yaweze kutekelezeka, serikali ilibidi ifanye marekebisho kifungu 30 cha Education Act No. 25, 1978. Katika mabadiliko haya kuletwa Bungeni ndipo Waislam wakajua kuhusu hii MoU kati ya Serikali na Makanisa.

Suali lingine la kujiuliza ni inakuwaje jambo zito kama hili lilipitishwa na Bunge letu bila kipingamizi? Suala hili limepita kwa kuwa Waislam Bungeni waliamini kuwa uamuzi huo una maslahi na taifa letu? Au limepita kwa kuwa Waislam katika Bunge ni wachache wameelemewa na ndugu zao Wakristo kupelekea kuwa sasa hawana sauti kwa uchache wao? Ikiwa huu ndiyo ukweli wenyewe, tumefikaje hapa na nini athari ya jambo hili kwa mustakbali wa taifa letu?

Kwa uchache unaweza mtu ukajiuliza kwa nini basi serikali hiyo hiyo haikuja na mpango wowote hata kama si sawa na ule wa Makanisa wakatoa fedha kwa taasisi za Kiislam na wao wajiletee maendeleo kama hayo ya Makanisa? Mimi sitatoa jibu ingawa majibu ninayo. Kwa kuhitimisha hebu tujiulize kwani Mahakama ya Kadhi ni kitu kipya katika nchi hii kiasi cha kusababisha mtafaruku huu ambao hivi sasa tunaushuhudia?

Ukweli ni kuwa ukoloni umeingia Tanganyika umekuta Waislam wakijihukumu kwa kitabu chao. Mmishionari Johan Krapf kaja Tanganyika na alipokelewa na Chifu Kimweri wa Usambaa mwaka 1848. Krapf alipokelewa kwa ukarimu wa hali ya juu na alimkuta Chifu Kimweri Muislam, anajua kusoma na kuandika kwa herufi za Kiarabu akihukumu katika barza yake iliyokuwa Vuga. Ni wazi kuwa Chifu Kimweri hakuwa anahukumu kutoka, “Order in Council,” kutoka India kwani Waingereza walikuwa bado hawajafika.

Chifu Kimweri alikuwa anahukumu kwa sheria kama walivyohukumiana Waislam katika ukanda wa pwani ya Afrika Mashariki kwa miaka mingi. Mimi nimekuwa na kupata fahamu katika Tanganyika ya 1950/60 na nina kumbukumbu za hizi mahakama za kadhi na baadhi ya hawa mahakimu nimewaona kwa macho yangu aidha wakiwa katika mahakama wakihukumu na wengine nimewaona mitaani na wengine nimewaona wakisuhubiana na wazee wangu. Namkumbuka Sheikh Abdallah Simba kutoka Songea. Nikifumba macho ni kama vile namuona Sheikh Abdallah Simba. Alikuwa kija Dar es Salaam na Land Rover yake mwenyewe na siku zote akivaa kanzu, koti na tarbush. Sheikh Abdallah Simba alikuwa na watoto wawili Bi. Habiba na Mwajuma. Bi Habiba alikuwa na umri sawa na mama yangu na alikuwa ‘’nurse’’ Princes Princess Margret Hospital (sasa Muhimbili Hospital) lakini Mwajuma yeye alikuwa makamu ya dada yangu mkubwa. Mwajuma akisoma St. Joseph’s Convent School (sasa Forodhani). Sheikh Abdallah Simba alikuwa akihukumu katika mahakama huko Songea kwa sheria za Kiislam na akifahamiana na babu yangu Salum Abdallah toka ujana wao katika Dar es Salaam ya 1920.

Sheikh Abdallah Simba akiishi Songea lakini alikuwa na nyumba mbili moja Mtaa wa Kipata (sasa Mtaa wa Kleist Sykes) nyingine Mtaa wa Somali (Sasa Mtaa wa Omari Londo). Majina ya mitaa hii ilibadilishwa kuwaenzi wazee hawa Kleist Sykes na Omari Londo walioacha alama katika historia ya uhuru wa Tanganyika.

Kulikuwa na Sheikh Said Chaurembo akihukumu katika Mahakama ya Kariakoo. Sheikh Said Chaurembo alikuwa katika Kamati Ndogo ya Siasa ya TAA (TAA Political Subcommittee) mwaka 1950. Kamati hii chini ya Mufti Sheikh Hassan bin Amir ilifanya makubwa katika kujenga mazingira ya kuunda TANU mwaka 1954 na kumweka Mwalimu Nyerere katika uongozi wa kudai uhuru lakini hapa si mahali pake kuyaeleza hayo. Huyu Sheikh Said Chaurembo alikuwa na nduguye akiitwa Iddi Chaurembo huyu ndiye baba yake Sheikh Abdallah Chaurembo na wakati ule Sheikh Abdallah Chaurembo alikuwa mwanafunzi katika chuo cha Mufti Sheikh Hassan bin Amir.

Sheikh Said Chaurembo ndiyo aliyekuwa na lile ghorofa maarufu Mtaa wa Msimbazi na Congo linalojulikana hadi leo kama Ghorofa la Chaurembo. Kwa kumalizia kuhusu hizi mahakama hapa Dar es Salaam napenda kueleza kuwa katika miaka ya 1960 baada ya uhuru Sheikh Kassim Juma alikuwa akihukumu katika Mahakama ya Kadhi Mkwajuni hadi mahakama hizo zilipovunjwa na serikali mwaka 1963. Sheikh Kassim Juma na yeye ana historia kubwa katika siasa za Waislam, BAKWATA na serikali baada ya uhuru.

Sheikh Abdallah Chaurembo akiwa msomi wa dini ya Kiislam alihusika sana katika harakati za kudai uhuru wa Tanganyika. Sheikh Abdallah Chaurembo alikuwapo katika mkutano wa TANU uliofanyika Mtaa wa Pemba usiku mmoja mwaka 1955 agenda kuu ikiwa vipi TANU itapunguza joto kali la Uislam ndani ya chama ili kupunguza ile taswira kuwa TANU ni chama cha Waislam. Jambo hili lilikuwa muhimu ili kumwezesha Mwalimu Nyerere kuongoza harakati za kudai uhuru kwa utulivu.

Pamoja na Sheikh Abdallah Chaurembo katika mkutano ule alikuwapo Sheikh Nurdin Hussein na Rajab Diwani lakini mzungumzaji mkuu na aliyesukuma agenda hii ikakubaliwa na TANU na kutoa azimio alikuwa Mufti Sheikh Hassan bin Amir. Azimio lenyewe lilikuwa yeyote atakaeleta udini katika TANU “atatoswa.” Ningependa sana kueleza historia hii lakini nachelea itakuwa nje ya maudhui. Lakini mtu unaweza ukajiuliza vipi katika historia ya uhuru wa Tanganyika majina haya hayasikiki kutajwa?

Haiyumkiniki hata kidogo kuwa wazalendo hawa walipigania uhuru wa Tanganyika ili waiweke kwenye madaraka serikali ambayo itakuja kuvunja misingi ya dini yao.

Tanga kulikuwa na Mahakama ya Kadhi na mahakama hii ilikuwa katika jengo la TAA Barabara ya 7 ambako Kadhi, Sheikh Ali bin Hemed Al-Buhry alihukumu jamii ya Waislam kwa kutumia sharia. Huyu Sheikh Ali bin Hemed Al Buhry ndiye baba yake Sheikh Mohamed Ali Al-Buhry na yeye ndiye alikuwa hakimu wa mwisho kwenye mahakama hiyo. Sheikh Mohamed Ali Al-Buhry alikuja baadae katika miaka ya 1968 kuhusika sana katika BAKWATA na kuna kisa cha kusisimua sana kati yake na serikali katika siasa za Waislam na BAKWATA lakini hapa si mahali pake kueleza makasa huu. Hapo Tanga kulikuwa na Liwali Abdallah Rished na mtaa aliokuwa akikaa ulipewa jina la Liwali Street kwa heshima yake. Baada ya uhuru ukaitwa Makoko Street kwa heshima ya mpigania uhuru na mwanachama shupavu wa TANU Rashid Makoko.

Kulikuwa na Sheikh Seif Nassor Alhinawy ambae alikuwa Akida pale Tanga na akihukumu kwa sheria. (Akida Seif ndiye baba ya wachezaji mpira mashuhuri katika miaka ya 1960 hadi 1970, Hemed Seif, Marshed Seif na Rashid Seif ambao ukimtoa Marshed wote ndugu zake waliva jezi ya taifa). Kwa kuthamini taasisi hizi za Kiislam kuna mtaa Waingereza waliupa jina Akida Road (sasa Mkwakwani Road) kwa heshima ya Akida Seif Nassor. Katika Tanganyika Tanga ndiyo moja ya miji iliyokuwa na historia nzuri sana ya Mahakama ya Kadhi. Mwanzo wa miaka ya 1900 kulikuwa na Kadhi Omar Stambuli kisha akaja Kadhi Ali bin Hemed Al-Buhry, Liwali Abdulrahman bin Ali Diwani, Liwali Rished Abdallah, Omar Stambuli, Juma Mwindadi , Said bin Ali Al-Buhry (OBE), Mohamed bin Ali Al-Buhry.

Masheikh hawa baadhi yao walifanya kazi ya ukadhi Tanga na wengine walikuwa Moshi, Arusha, Mwanza na kwengineko Tanganyika.

Tabora Sheikh Bilali Mshorwa alikuwa akihukumu kwa sheria mahakamani. Huyu Sheikh Bilali Mshorwa akifahamiana vizuri sana na babu yangu, Salum Abdallah pale Tabora kwani wao ndiyo walikuwa wanamji na wazee wa mjini wakati wao. Moshi kwa Wachagga alikuwapo Liwali Mussa Minjanga akihukumu Bomani. Liwali Mussa alikuwa akifahamiana na baba yangu na mtaa aliokuwa akiishi Liwali Mussa Minjanga toka enzi hizo za ukoloni ulikuwa ukijulikana kama Liwali Street na jina hili limebaki hivyo hadi hii leo.

Hali ilikuwa hivi Tanganyika nzima na Mahakama ya Kadhi haikupata kuwa katika agenda ya kufutwa uhuru utakapopatikana. Nini kilifanya serikali mwaka 1963 ivunje mahakama hizi? Jibu ninalo lakini sitalitoa kwa sasa.

Kuna watu wanasema ati kuwa na Mahakama ya Kadhi itavunja umoja wa taifa letu. Hapa linakuja swali kwani Tanzania huo umoja unaozungumziwa tunao hivi sasa? Mbona kumekuwa na malalamiko mengi tu kutoka kwa Waislam kuwa serikali ina udini na inawabagua? Hii ilianza kama manung’uniko ya chinichini kwa miaka mingi na mwisho ikaibuka kwa sauti kubwa kuwa nchi yetu inatawaliwa na “Mfumokristo” yaani nchi inaendeshwa kwa maslahi ya Kanisa. Mwaka wa 2012 Waislam walifanya mikutano nchi nzima wakitahadharisha kuhusu hili. Video za mikutano hii imezagaa nchi nzima na kwenye mtandao. Bahati mbaya hadi leo serikali imekuwa kimya.

Labda mtu unaweza kujiuliza kwa nini serikali imekuwa kimya kwa shutuma nzito na za hatari kama hizi? Imekaa kimya kwa kuwa yanayosemwa na Waislam hayana ukweli na ithibati yoyote au iko kimya kwa kuwa inaogopa kulifingua Sanduku la Pandora? Jibu la swali hili vilevile ninalo. Nadhani msomaji wangu angalau kwa mbali umeweza kusoma angalau kwa muhtasari historia ya nchi yetu ilivyokuwa. Vipi tumejikuta katika huu uhasama tunaoushuhudia hivi sasa hii ni mada ya kujitegemea na In Sha Allah tutaizungumza.


JAMII FORUMS

2 comments:

Mbele said...

Hakuna andiko lolote la histiria linaloweza kuitwa ndilo pekee la kweli. Kwanza inabidi mtu ufahamu nadharia au falsafa ya historia. Uandishi wa historia ni mchakato ambao huwezi kuuhitimisha ukasema sasa kazi imeisha.

Kila andiko la historia ambalo limejengeka katika utafiti linatupa ukweli kiasi fulani tu. Mambo mengi huwa hayaonekani katika hilo andiko.

Kwa Hali hiyo, utafiti na uandishi wa historia inabidi use delete. Mohammed Said anaelezea mchango wa baadhi ya wa-Islam, lakini akumbuke kuwa wa-Islam wail kuwa wengi kuliko hao anaowataja, na mchango wao wao haukuwa huu tu anaouelezea. BAKWATA nao walikuwa na bado ni wa-Islam. Walishiriki kikamilifu katika kuanzishwa na kudumu kwa BAKWATA. Huo ni mfano moja tu.

Kuna watafiti wengi wameandika kuhusu historia ya Tanganyika (na Tanzania). Sawa kama Mohammed Said, hakuna ambaye amemaliza suala hili katika andiko lake au maandishi yake.

Profesa Susan Geiger (marehemu) alifanya utafiti kuhusu suala la historia ya harakati za kupigania uhuru lakini alizingatia mchango wa wanawake, mmoja maarufu akiwa Bibi Titi Mohammed. Mfano huu unatosha kuthibitisha kuwa hakuna mtu ambaye ameweza au anaweza kuandika historia akadai kuwa yeye ndiye amesema ukweli na hakuna mwingine.

Mbele said...

Samahani, hiyo IPad imekorofisha hapo juu, mstari wa kwanza wa para ya tatu. Niliandika "uendelee," sio "use delete."