Saturday, February 28, 2015

KAPTENI KOMBA AFARIKI DUNIA


Na Baraka Mfunguo,

Mbunge wa Mbinga na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Kapteni John Damian Komba amefariki dunia katika Hospitali ya TMJ, Dar es Salaam leo saa kumi jioni kutokana na mshtuko wa moyo . 

Binafsi niliweza kumfahamu kapteni John Komba nikiwa mwanafunzi wa shule ya Msingi Mlimani. Siku hiyo kulikuwa na ujio wa mwanapinduzi Komredi Walter Sisulu mwanamapinduzi wa ANC ambaye alikuwa mmoja wa wapambanaji dhidi ya Ubaguzi wa rangi Kusini mwa Afrika  pale Chuo Kikuu Mlimani na kwaya ya Jeshi ikiongozwa na kapteni Komba ilikuwa ikitumbuiza pale kwenye mti maarufu unaojulikana kama Mdigrii. Hata wimbo wake ulikuwa wa kimapinduzi kweli kweli nanukuu "we are happy Africa, to see you again Sisulu, dear leader dear father welcome to O.A.U eeeh", .... liberation is our goal ulikuwa kama kibwagizo.

Baadaye akaamua kuwa mwanasiasa baada ya kustaafu jeshi. Kapteni Komba ni msanii,mwanasiasa wa pekee aliyeweza kuhudumu katika awamu zote na ni mwanamuziki mwenye kuifahamu vyema historia na matukio ndani ya chama chake cha Mapinduzi.  Kapteni Komba ndiye aliyefungua milango kwa wasanii kuingia katika vinyang'anyiro vya siasa hususan ubunge. 

Hili ni pigo kubwa kwa C.C.M kwa kuweza kumpoteza mhamasishaji mkuu na ni pigo pia kwa wasanii ambao wangependa kufuata nyayo zake katika muziki.  Ni pigo kubwa pia kwa wananchi wa Mbinga ya Magharibi aliokuwa anawatumikia, wananchi wa Tanzania wapenda Maendeleo na wale wote wanaotoka katika mkoa wa Ruvuma. Ni pigo kubwa kwa familia yake iliyokuwa ikimtegemea kwa hali na mali.

Raha ya milele umpe ee bwana...... Na mwanga wa milele umwangazie .....Apumzike kwa Amani.

Bwana ametoa Bwana ametwaa jina lake lihimidiwe.


No comments: