Tuesday, February 10, 2015

DR. JAKAYA MRISHO KIKWETE NDIYE KIONGOZI BORA WA WATANZANIA AWAMU YA NNE.


Rais wa awamu ya nne Tanzania Dr. Jakaya Mrisho Kikwete

Na Baraka Mfunguo,

Wapo ambao watakaokubaliana nami, na wapo ambao watakaopingana nami. Lakini napenda kukiri wazi kwamba Jakaya Mrisho Kikwete ni kiongozi thabiti mwenye misimamo na asiyeyumbishwa . Kuna tofauti kubwa kati ya kiongozi na mtawala na mwanasiasa. Jakaya sio mtawala ni kiongozi  mwenye kukubalika katika medani zote za kisiasa ndani na nje ya nchi kiongozi mwenye ushawishi, kiongozi anayezijua kuzichanga karata zake vyema. 

Sifa moja ya kuwa kiongozi ni kuweza kutambua mahitaji ya wale unaowaongoza na kuyatekeleza, kushirikiana na wale unaowaongoza katika mikakati mbalimbali, kusimamia kile unachokiongoza ukionyesha mfano, dhamira ya dhati ya uongozi, uvumilivu  na kukubali kukosolewa pasipo kuonyesha hisia. Katika historia ya nchi hii Jakaya ni rais wa kwanza katika hilo. Wapo waliomkosoa na wengine kumpopoa na mawe  lakini akavumilia.

Nitatolea mfano Rais wa Marekani ndugu Andrew Johnson ambaye mwaka 1867 alifanya uamuzi ambao Wamarekani na washindani wake kisiasa walimkosoa sana kiasi ambacho alionekana hana maana na kunyata miongoni mwa Wamarekani. Uamuzi wake ulikuwa ni kuinunua Alaska kwa dola za kimarekani 7.2 milioni kwa wakati huo kutoka katika dola ama taifa la Kisovieti. Wengi waliukosoa uamuzi wake huo kwa sababu hawakuona manufaa ya kununua Alaska kwa wakati ule. Lakini ajabu ni kwamba Alaska ilikuja kugundulika baadae kuwa na hazina kubwa ya mafuta na gesi.  Sasa hivi humwelezi kitu chochote Mmarekani juu ya Alaska na Warusi wanajutia kweli kweli uamuzi wao.

Wengi wetu tumeukosoa kwa kiasi kikubwa uamuzi wa Jakaya wa ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam. Kikubwa ambacho kimepelekea madhila haya ni ukosefu wa mawasiliano stahiki kwa njia stahiki kutoka kwa watendaji mbalimbali wa Serikali pamoja na Wanasiasa waliopewa dhamana ya kumsaidia rais. 

Wengi wao walitumia kauli ambazo hazikuwapendeza wananchi waliotaka kujua ni nini hatima yao na matokeo yake ni majeraha makubwa ambayo hawajaweza kuyakabili vyema na visasi vya nafsi vimetawala. Kilicholeta utata ni kauli, kauli thabit haki, kauli pekee za viongozi  na wanasiasa wetu. Ujenzi huu una manufaa makubwa kwa nchi na uchumi wake si kwamba utasaidia kupunguza adha na kero zingine zinazosababishwa na gharama za tozo la umeme bali litachochea ukuaji wa viwanda mkoani Mtwara na kwingineko na kuweza kukuza ajira kwa watanzania. Leo Jakaya anaweza akaonekana mtu mbaya lakini ninaamini haitafika mbali tutamkumbuka na tukilaani dhamira zetu kwanini tulimhukumu mapema.Napenda kuchukua hatua hii kumpongeza mheshimiwa Rais  Dr. Jakaya Mrisho Kikwete kwa yote aliyoifanyia nchi yake ya Tanzania. Ni mweledi, shupavu, msikivu, mvumilivu, mwanadiplomasia imara na mcheshi mtu asiyechokwa kupendwa na watu. Jakaya ni kiongozi adhimu ambaye mwenyezi Mungu amemjaalia na kutokea kuwa Mtanzania. Wapo wengi katika bara hili wangetamani wawe na kiongozi kama Jakaya. Lakini ni ngumu kumfanana Jakaya na yeye ni kiumbe wa Mungu kikubwa tusichojua "we do not know what it takes to be the president of a country"  sio kitu rahisi sana kama wengi tunavyodhani.

Binafsi na ninapenda nikiri wazi, tokea nikiwa shule ya sekondari, nilivutiwa sana na haiba yake na utaratibu wake na nikavutiwa sana lau kuwa kiongozi ili niweze kuyafanya yale ambayo yeye amekuwa akiyafanya tokea mwaka ule wa 1995 akiwa naibu waziri wa Nishati mpaka alipomrithi Mhe. Alnoor Kassam na mpaka pale alipomrithi Prof Malima Wizara ya fedha na mpaka alipokuwa Waziri wa mambo ya nje. Jakaya hakuwa mzembe katika maeneo yote na takwimu ziko wazi. Hata baadhi ya watu waliokwenda kwake kwa ajili ya kumwomba mialiko mbalimbali alikuwa mcheshi na aliwapokea.

 Kitu kimoja ambacho mzazi wangu alipata kunieleza uzoefu wake juu ya Jakaya ni kwamba, ikiwa utapeleka mwaliko kwake, katika warsha ya aina yoyote ilikuwa ni lazima hotuba atakayoisoma yeye kama mgeni rasmi aihariri mwenyewe na kupitia kipengele kimoja baada ya kingine. Pia kitu kingine ambacho alichokuwa nacho ni kiongozi mwenye kumbukumbu ya hali ya juu. Mzee akiwa na miadi naye akifika ofisini atamkirimia na kumkaribisha kwa tabasamu " Aaaah  mzee fulani  habari ya utokako , eeeh hebu mwandalieni chai mzee wangu hapa". 

Huyo ndiye Jakaya ambaye nilipatwa kuhadithiwa. Ambaye leo hii ameleta sio mabadiliko makubwa katika nchi, bali ataweka historia ya kuwa rais wa kwanza atakayewezesha utatuzi wa mustakabali wa Watanzania wa sasa na vizazi vinavyokuja. Katika uongozi wake tumeona wananchi wengi wakizitambua haki zao, ukuaji wa demokrasia, shule zikiongezeka, vituo vya afya pamoja na mahospitali pia ushirikiano mkubwa baina ya makampuni binafsi na serikali katika huduma za kijamii na uchumi, suala la miundombinu ni la kipekee na Jakaya ameanzisha kwa mara ya kwanza mchakato wa kuijenga upya reli ya kati. 

Mwisho napenda kusema kwamba Jakaya ni tunda la Watanzania ikiwa tutamuenzi tutakuwa si kwamba tumeuenzi utawala wake bali tumeienzi nchi ya Tanzania na watanzania kwani yeye ni alama muhimu katika historia ya nchi yetu. Jakaya kama viongozi wengine wa Tanzania wamejitolea katika kuijenge nchi hii na taifa hili na demokrasia hii ya kukubali kukosoa na kukosolewa yeye aliweza kustahimili sio viongozi wote watakaowezana nalo. Katika ukuaji wa nchi hii zipo changamoto nyingi lakini kubwa ni ajira, rushwa na ubaguzi pamoja na ukabila na udini unaoshamiri, ukosefu wa huduma muhimu za kijamii kwa  haki maeneo ya chini, ubadhirifu na ufisadi. Hivi ndivyo vinavyowakera watu na Jakaya amejitoa mhanga kukabiliana navyo tumuunge mkono katika dakika ya lala salama ili watanzania tupate ushindi katika maendeleo.

No comments: