Saturday, January 3, 2015

CHANZO CHA PANYA ROAD: TUSIMTAFUTE MCHAWI.

Heka heka jijini Dar wakati watu wakijilinda usalama wao na mali zao dhidi ya kundi la Panya Road.

Na Baraka Mfunguo,


Panya road walivamia  jiji la Dar  jana  ikidaiwa chanzo chake ni mwanachama mwenzao aliuawa na sungusungu walipokwenda kuiba. Walipitisha michango na mida ya saa kumi jioni walikusanyika magomeni kagera karibu na Friends corner hotel kwa ajili ya mazishi. Kundi kubwa kama la vijana miatano lililosemakana  kuwa  wanasubiri kwenda kwenye mazishi lilikuwa kwenye mkumbo wa kundi Panya Road. Inasemekana walipeana taarifa maeneo yote na viunga vyote vya jiji la Dar  waje kushirikiana  ili  wakimaliza kuzika waanze kulipa kisasi ingawa  haijathibitika kama dhima yao ilikuwa ni kulipiza kisasi ama kuzika ama ni matokeo ya kifo cha mwenzao inayeelezwa aliuawa.


Ilipofika muda wa kwenda kuzika  inaelezwa walifunga barabara na kuanza kuwapora makonda wa daladala na baadhi ya watu huku wakiwa  wakielekea makaburi ya Kagera Mikoroshini, kipindi hicho polisi walipata taarifa na wakapishana nao wao wakidhani wanaenda kuzika katika makaburi ya Mburahati  . Maiti ilizikwa kwa amri  na utaratibu wao huku mashekhe wakishurutishwa na mapanga kwa mujibu wa vyanzo vya taarifa .


Walipotoka kuzika ikawa wakarudi kupitia njia ya Morogoro road nakuanza uporaji hadi polisi wa kutuliza ghasia  walipofika na kuanza kupiga mabomu, na kufanikiwa kuwakamata wawili.Baada ya kutawanyika, wale waliokuwa wanaoenda mbagala wakawa  wanapora watu ovyo ovyo ,waliokuwa wakielekea Buguruni Tabata na Gongolamboto vivyo hivyo na kundi lililokuwa linadaiwa la Mwananyama ndilo lilirudi tena usiku na kuishia kukabiliana na  polisi wa kutuliza ghasia . 

Vijana  hawa wadogo kiumri  ukiwatazama umri wao unaweza ukakadiria ni  kati ya kuanzia  miaka 14-23 .


Matokeo ya kuasisiwa kwa makundi kama haya ambapo Mtwara lipo kundi maarufu la “Tukale Wapi” ni ni matokeo ya kukosa ajira, rushwa, kukosa elimu na pengo lililopo kati ya walionacho na wasionacho, upendeleo serikalini, hali mbaya ya kiuchumi, kukata tamaa ya maisha, pamoja na wanasiasa kukosa mbinu na ubunifu wa kutatua matatizo yao badala yake wanageuzwa ngazi ya kupandia, ugoigoi wa viongozi na watendaji wa serikali katika kufikiri, NGO's zinazowatumia kama mitaji ya kupata vipato na kuvimbisha matumbo ya wamiliki wake ambao hupita na kujitapa mbele za watu na vyombo vya habari kama wanaharakati. Vile vile  Ufisadi na ukosefu wa maadili kwa viongozi wa nchi pamoja na wale waliopewa dhamana.

Wakati kundi moja likionekana likiwa linaumia, kundi lingine la walionacho linalojumuisha wasomi, wafanyakazi wafanyabiashara, wanasiasa na watu wenye kipato cha kati linaonesha kutojali uhalisia. Jiulize  wewe binafsi ni mara ngapi umekutana na watoto wa mitaani ukiwa barabarani hususan wale wanaojitafutia riziki walau ya kufuta kioo ili wapate ugali  na kuonyesha kutowajali na kufikia hata hatua ya kuwatisha na kuwatolea maneno machafu yasiyoelezeka ama kuandikika. 

Ama kuwahi kusikia maswahibu yao kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii na Wizara  pamoja na vyombo vyenye mamlaka husika vipo  pamoja na watendaji wake na havionyeshi kujali na  jibu utakalopewa endapo utataka kujua kwa nini hali ya watoto mitaani inaongezeka kila kukicha  ni, "serikali haijatenga fungu la fedha katika bajeti ya wizara" . Na hata kama serikali ingetenga fungu maalum kwa watoto wa mitaani lingewafikia?  Thubutu! 

Hayo ndio majibu mepesi kwa tukio ambalo sasa linakua na litafikia mahali litawashinda. Sisemi litatushinda kwa sababu sidhani hata mimi ni miongoni mwao. Mimi najichukulia kama raia wa kawaida kabisa kutokana na dhana ya baadhi ya watu wenye madaraka, mamlaka , ajira na kipato kujiona wao wanastahili kuliko wengine. Ni hali halisi ya kibinadamu mmoja mmoja na ubinafsi wa ndani lakini sio hali halisi  ya uhalisia wa maisha ya binadamu kwa ujumla

Wakati wa enzi za Mwalimu Julius Kambarage Nyerere hali haikuwa hivyo kulikuwa na mikakati na mipango dhidi ya watoto wa mitaani na wale watukutu, japokuwa hali haikuwa nzuri kifedha na kiuchumi, lakini iliweza kudhibitiwa . Nakumbuka  pia miaka ya mwanzoni wa tisini nikiwa mwanafunzi wa sekondari ya Tambaza, pale  maeneo Upanga (sikumbuki vizuri mtaa) kama unaenda Zanaki sec ukitokea njia ya DIT(Zamani Dar Tech)  usawa wa  kanisa la Mennonite  kutokea mchepuko Morogoro road mkabala na iliyokuwa shirika la bahati nasibu, kulikuwa hata na mahabusu yao kulikuwa hata  na mjumuisho wa  watoto wa mtaani na watukutu walikuwa marafiki wazuri kutokana na malezi yao na sie tulikuwa tukipita njia  tulikuwa walau tukiwatupia karanga na matunda sasa hivi naambiwa hata magerezani na mahabusu watoto na watu wazima huchanganikana. 

Kimsingi watoto wa mitaani walikuwa hawaonekani na kila mwananchi alijivisha jukumu la kuhakikisha maadili yanakuwepo katika jamii kuanzia ngazi ya chini.

 Sasa imefika wakati huria ambapo watu huweza kuzaana na kutelekeza watoto, wengine kutupa watoto katika mfuko ya plastiki sitaki kusema ya Rambo, watoto kukosa malezi na misingi ya maadili, Elimu kugeuzwa biashara badala ya huduma ya msingi, na hata hizo haki zao zinazoelezwa katika Katiba ibayopendekezwa ni kama porojo tu za wanasiasa. Hao watoto wa mitaani wakiwa wamefikia hatua ya utu uzima yale manyanyaso, uonevu, dhuluma, vitendo vinavyoshusha utu wa mtu ambavyo vinafanywa na hao hao waliomo miongoni mwa watu  wanaojiita wasomi, wanasiasa, wajasiriamali, wanaharakati na watu wa kundi la kati na huku serikali iliwa imefumbia macho matukio hayo, hali  Fulani ya kisaikolojia hujitokeza  inayowafanya wachukie kila kitu na kila mtu.


Wakikutana na watu wakawahamasisha wajiunge na kundi fulani la uhalifu kwa ujira fulani ama kupata ulinzi dhidi ya vitendo vyovyote visivyostahili kufanyika kwao watakataa?Haya yote  kwa mtazamo wangu, inatokana na watu kuchoka mfumo dhulumati, mfumo wa kimafia and "that anger manifest itself into  those actions for them to be heard" hiyo ndiyo fimbo ya mnyonge. 

Mimi binafsi sitashangaa kama haya yakitokea kulikuwa na "Komando Yosso" miaka ya tisini baadae likaja kufa. Ikitokea  Wananchi  wakaamua kuanzisha makundi ya kukabiliana na uhalifu kuna mtu ambaye yuko katika ngazi ya juu serikalini (ukiacha Said Mwema aliyeanzisha polisi jamii ambalo nalo uhalali wake haueleweki mpaka sasa) ataweza kuwapa msukumo na hamasa katika jamii hii ya leo iliyojaa unafiki na uzandiki? 

Tumezoea kuwalaumu Polisi pale matukio mabaya yanayoyowagusa wengi (si mtu mmoja mmoja)yanapotokea Ninaamini  kwa hali hii ya ubadhirifu na ukosefu wa maadili wa viongozi na wale waliohodhi dhamana serikalini kwa njia zao za ghilba na kejeli dhidi ya wananchi, walalahoi na wasionachi,  itafika wakati hata hao panya road wakaonekana mashujaa endapo wakitumika vizuri kuuondoa uozo huu wa rushwa na ufisadi uliojaa na kuifunika nchi gubi gubi na serikali kulala fofofo. 

Pamoja na kwamba  njia walizotumia zinahatarisha usalama wa wananchi na mali zao, ni wakati wa kuchunguza na kubaini chanzo cha matatizo na kukata mzizi na sio tawi kama wengi wanavyotaka iwe. Kukata  tawi kwa mfano ni kuwatafuta kuwakamata na kuwaua, badala yake wawekwe kitako watu waangalie uwezekano wa kuwasaidia na kuwatumia kwa maendeleo ya nchi.

No comments: