Wednesday, October 8, 2014

RUKSA: MIKUTANO YA KISIASA LINDI NA MTWARA

Serikali imeondoa zuio la mikutano ya Vyama vya Siasa lililokuwa limetangazwa mwezi Mei mwaka juzi kuzuia mikutano hiyo kufanyika katika mikoa ya Lindi na Mtwara.

Zuio hilo limeondolewa leo na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Mathias Chikawe.

Mikutano hiyo ilizuiliwa kutokana na vurugu za wananchi waliokuwa wakipinga ujenzi wa mradi wa bomba la gesi kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam hali iliyosababisha kuvunjika kwa amani na utulivu katika mikoa hiyo.

Katika vurugu hizo, watu kadhaa walipoteza maisha na wengine kujeruhiwa huku magari na nyumba zikichomwa moto.

Hatua hii ya sasa imechukuliwa baada ya Serikali kuridhika kuwa hali na amani na utulivu imerejea katika mikoa hiyo na kuwa mikutano hiyo sasa inaweza kuendelea kwa kufuata sheria na utaratibu uliowekwa.

Aidha Jeshi la Polisi litaendelea kutoa ushirikiano katika uendeshaji wa mikutano ya kisiasa inayoendelea katika maeneo mbalimbali nchini na kuwa vibali vya mikutano vitaendelea kutolewa kufuatana na mazingira yatakayokuwepo katika eneo ambapo Chama husika kitakuwa kimeomba kibali.

Ni matumaini ya Serikali kuwa Vyama vya Siasa vitatumia fursa hii kuendesha mikutano yao kwa amani na utulivu kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi kama taratibu za uendeshaji wa mikutano hiyo zinavyoelekeza.


Imetolewa na: 
Isaac J. Nantanga
MSEMAJI
WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI
07/10/2014

No comments: