Thursday, October 2, 2014

PUMZIKA KWA AMANI PROF. LIVIGA "NURU YA KUSINI"


Nimezipokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha Prof. Athuman Livigha wa Chuo Kikuu cha Dsm. Livigha alikuwa mwalimu wangu na naweza kusema alipenda kutufundisha kile ambacho aliamini ni sahihi kwetu na kile ambacho ni cha hakika na kilichofanyiwa utafiti. Alikuwa ni mpenda mizaha wakati wa kufundisha ila hakuwa na mzaha katika taaluma yake. Aliipenda timu ya Arsenal na katika ule msimu wa neema wa akina Wenger wakati Arsenal ilipoweka rekodi ya kutofungwa alikuwa akitunanga sana sie vinara wa Manchester/"Man U".

Pumzika kwa amani Mwalimu, Pumzika kwa amani taa ya kusini iliyozimwa ghafla. Wana wa Kusini walijivunia uwepo wako katika taaluma, walijivunia pia namna ulivyowawakilisha na kwamba watu wa kusini wanaweza na inawezekana. Poleni sana kwa familia yake, ndugu, jamaa, marafiki, na wale akina sie tuliopata fursa "priviledge" ya kusikiliza mihadhara yake ya kitaaluma na mafunzo. Pengo lako ni kubwa hususan katika idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala pale Kitivo cha Sanaa/ Shule ya Sanaa Mlimani Chuo Kikuu.TAARIFA YA KIFO CHAKE

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Athuman Livigha, amefariki dunia baada ya kupigwa risasi na watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi nyumbani kwake, jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa taarifa zilizothibitishwa na Makamu Mkuu wa UDSM, Profesa Rwekaza Mukandala, ni kwamba Profesa Livigha alikutwa na masahibu hayo akiwa nyumbani kwake Bunju, Wilaya ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam, usiku wa kuamkia jana.

No comments: