Friday, October 3, 2014

MISINGI NA UHALISIA WA TASWIRA YA UCHAPAKAZI YA LOWASSA.Msingi na uhalisia wa taswira ya 

uchapa kazi ya Lowassa Na Prof. Kitila Mkumbo, (KUTOKA GAZETI LA RAIA MWEMA)

Taswira ya kwanza ni kwamba Lowassa ni mchapa kazi, mwenye uwezo wa kufanya maamuzi magumu na kuyasimamia bila kuyumba.
Taswira ya pili ni kwamba Lowassa si mwadilifu, na hivyo hafai kuwa kiongozi mkuu wa nchi katika kipindi hiki ambacho nchi ina njaa ya viongozi waadilifu baada ya kuchoshwa na kashfa lukuki za ubadhirifu na ufisadi wa fedha za umma kwa takribani miongo miwili iliyopita.

Katika makala hii na zitakazofuatia , pamoja na kuanisha wasifu wa jumla wa Lowassa, ninajadili na kuhakiki uhalalisia wa taswira hizi, na maana yake kwa Lowassa katika mbio zake za kuwania nafasi ya urais wa nchi yetu.

Chanzo cha taarifa zilizotumika katika uchambuzi huu ni tovuti (website) ya Lowassa (www.elowasa.com), mahojiano aliyoyafanya katika vyombo vya habari kwa nyakati tofauti, pamoja na mahojiano niliyoyafanya na watu waliowahi kufanya naye kazi katika sehemu mbalimbali pamoja na washauri wake wa karibu.

Lowassa ni nani?


Edward Ngoyai Lowassa alizaliwa Agosti 26, 1953, na kukulia katika Kijiji cha Ngarash huko Monduli, akiwa ni mtoto mkubwa wa kiume kwa mzee Ngoyai Lowassa.
Alisoma Shule ya Msingi ya Monduli (1967-1971), Shule ya Sekondari Arusha kwa kidato cha nne (1967-1971) na Shule ya Sekondari Milambo kwa kidato cha tano na sita (1971-1973). Ana shahada ya elimu na sanaa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam aliyohitimu mwaka 1977, na Shahada ya Uzamivu katika Maendeleo kutoka Chuo Kikuu cha Bath nchini Uingereza aliyohitimu mwaka 1984 kwa udhamini wa British Council.
Ni mume wa Regina Lowassa na wamejaliwa watoto watano, watatu wa kiume na wawili wa kike.

Kikazi, Lowassa amekulia na kufanya kazi zaidi ndani ya CCM na serikali yake. Mara baada ya kumaliza Chuo Kikuu cha Dar es Salaam aliajiriwa na CCM kama Katibu Msaidizi na baadaye Katibu wa Wilaya. Alipata kuwa msaidizi wa mzee Rashidi Mfaume Kawawa, Daudi Mwakawago na Horace Kolimba. Alifanya kazi pia jeshini sambamba na Rais Jakaya Kikwete pamoja na Abdulrahman Kinana na aliondoka jeshini akiwa na cheo cha Luteni.

Jambo moja ambalo watu wengi hatukulijua kabla ni kwamba Lowassa ni miongoni mwa wanasiasa wanajeshi waliopigana vita nchini Uganda mwaka 1978/1979.

Kwa nchi nyingi duniani, hii ni sifa muhimu ya ziada kwa mtu yeyote anayewania uongozi wa nchi kwa sababu kushiriki kupigana vita huchukuliwa kuwa ni kiwango cha juu kabisa cha uzalendo kwa kuwa tayari kuifia nchi.

Aliingia katika siasa za kiserikali mwaka 1985 alipoteuliwa kuwa mbunge wa vijana, sambamba na Anne Makinda na Jenerali Ulimwengu. Akiwa bado mbunge mwaka 1989 aliteuliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Mikutano ya Kimataifa cha Arusha (AICC) ambako alidumu hadi mwaka 1990 alipochaguliwa kuwa mbunge wa Jimbo la Monduli hadi leo.

Aliteuliwa kuwa waziri katika ofisi ya makamu wa kwanza wa rais akishughulikia Mahakama na Bunge 1990-1993, na baadaye aliteuliwa kuwa waziri wa ardhi, nyumba na maendeleo ya mijini 1993-1995.

Mwaka 1997 aliteuliwa na rais Benjamin Mkapa kuwa waziri katika ofisi ya makamu wa rais akishughulikia mazingira na umasikini.
Mwaka 2000 hadi 2005 alikuwa waziri wa maji na maendeleo ya mifugo.

Aliteuliwa na Rais Kikwete kuwa waziri mkuu Desemba 30, 2005, nafasi aliyodumu nayo hadi Februari 7, 2008 alipojiuzulu kwa kile kinachojulikana kama kashfa ya Richmond, lakini yeye mwenyewe akieleza kama kitendo cha kuwajibika katika kulinda maslahi ya chama chake kwa makosa yaliyofanywa na watendaji wa chini yake.


Uhalisia wa taswira ya uchapa kazi wa Lowassa

Ili kufanya tathimini kuhusu uhalisia wa taswira ya Lowassa kwamba ni mchapa kazi inabidi kumuangalia katika maeneo makubwa matatu alikofanyia kazi, ambayo ni katika chama chake cha CCM, AICC na serikali alipokuwa waziri na baadaye waziri mkuu. Msingi wa uchapa kazi wa Lowassa unaelezwa katika aina ya maamuzi ambayo amekuwa akiyafanya kama kiongozi. Nitaanisha baadhi ya maeneo haya.
Mzee mmoja aliyepata kushika nafasi mbalimbali ndani ya CCM na serikalini na ambaye amefanya naye kazi kwa karibu, anamweleza Lowassa kikazi kama ‘frontliner’.


Kwamba Lowassa siku zote alikuwa mbele akitaka kuhakikisha kwamba anatekeleza jambo mlilokubaliana na kuona matunda yake kwa haraka iwezekanavyo. Kichama, mzee huyu alimwelezea Lowassa kama mtu anayeijua CCM ya sasa kuliko mtu mwingine yeyote aliyeko madarakani ndani ya CCM na serikalini. Kwa mujibu wa mzee huyu, ambaye mwenyewe anajibainisha kuwa ni CCM asili, Lowassa “ndiye mchawi anayefaa kuilea CCM ya sasa”!!


Mmoja wa wafanyakazi wa zamani wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC) aliyepata kufanya kazi na Lowassa anakiri kwamba ni mchapa kazi, lakini kwa maoni yake ni kwamba aliivuruga sana AICC. Hii ni kwa sababu kwa muda mfupi aliokaa pale AICC alibinafisisha vitega uchumi vya AICC vikiwamo duka la zawadi (gift shop) lililokuwa Uwanja wa Ndege sambamba na kampuni ya magari ya watalii na hoteli.


Mfanyakazi huyu anamueleza Lowassa kama mtu mwenye maamuzi ya ‘kiMagufuli’ na ‘kiMrema’ yasiyozingatia umakini na utaratibu.
Hata hivyo, mfanyakazi mwingine aliutetea uamuzi wa Lowassa wa kubinafisisha vitega uchumi vya AICC kwa maelezo kwamba vilikuwa vinaendeshwa kwa hasara. Pengine uamuzi huu wa Lowassa wa kubinafisisha vitega uchumi vya AICC inatupa mwanga kidogo juu ya falsafa yake kiuchumi, ambayo tutaijadili katika sehemu ya tatu ya makala hii.


Mifano mingine inayotajwa kuwa ni uwezo alionao wa kufanya maamuzi magumu na kuyasimamia yanahusishwa na ujenzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma, ujenzi wa Shule za Sekondari za Kata, kuvunjwa kwa mkataba wa City Water na mradi mkubwa wa maji kutoka Ziwa Victoria. Tuitazame kidogo mifano hii.


Pamoja na kwamba wazo la kujenga Chuo Kikuu kipya cha Dodoma lilitolewa na Rais Kikwete katika kampeni zake za mwaka 2005, inajulikana kwamba Lowassa ndiye aliyesukuma utekelezaji wake kwa kutafuta fedha za ujenzi wa chuo hicho kupitia mifuko ya pensheni.


Kuna ‘hadithi’ kwamba mwanzoni alipowaita makatibu wakuu wa wizara walionyesha ugumu wa kutekeleza mradi ule katika muda ambao Rais alikuwa anataka utekelezwe. Hata hivyo, inaelezwa Lowasa aliwakaripia na kuwaambia kuwa Katibu Mkuu yeyote anayeamini kwamba mradi huu hautekelezeki ampelekee barua ya kujiuzulu na yeye angeifikisha kwa Rais.


Ni katika hatua hii ndipo makatibu wakuu walipokuja na wazo la kutafuta fedha kutoka mifuko ya pensheni. Panaweza pakawa na ubishi juu ya chanzo hasa cha wazo la kujenga Chuo Kikuu cha Dodoma, lakini hakuna ubishi mkubwa kuhusu ukweli kwamba Lowassa ndiye aliyesukuma utekelezaji wake na kuhakikisha kwamba fedha za ujenzi wa chuo hicho zinapatikana.
Ujenzi wa Shule za Sekondari za Kata ni jambo la kisera ambalo limeanishwa vizuri katika Sera ya Elimu ya Mwaka 1995 iliyotengenezwa wakati Profesa Philemon Sarungi akiwa waziri wa elimu.


Katika sera hiyo, ujenzi wa Shule za Kata umeelezwa kama mkakati sahihi wa kupanua elimu ya sekondari nchini. Utekelezaji wa sera hii ulianza mwaka 1997. Hata hivyo, ufanisi wake ulikuwa wa kusuasua hadi baada ya uchaguzi wa mwaka 2005 ambapo Rais Kikwete alihimiza zaidi kama sehemu ya mpango wake wa kupanua elimu ya sekondari na elimu ya juu nchini na hapa ndipo tunapomuona tena Lowassa. Hakuna ubishi kwamba ni yeye aliyesimamia kwa kasi zaidi ujenzi wa shule hizi alipokuwa waziri mkuu.


Baadhi yetu katika tasnia ya elimu hatuamini kwamba ilikuwa ni uamuzi wa maana kujenga shule hizi kwa mkupuo na kwa muda mfupi kiasi kile kana kwamba dunia inaisha kesho.
Kasi ya ujenzi wa shule hizi ndani ya muda mfupi ulisabisha kupatikana majengo mengi yakiitwa shule lakini pasipo elimu ya maana ndani yake.
Hata hivyo, shule hizi sasa zipo na maelfu ya watoto wa Kitanzania wanasoma, pamoja na kwamba elimu waipatayo inatia shaka ya kutosha.

Uamuzi mwingine unaoelezwa kwamba ni mgumu uliofanywa na Ndugu Lowassa ni kumshauri Rais kufuta umiliki wa kiwanja Mikocheni mwaka 1995 kwa mfanyabiashara maarufu wakati huo akiitwa Bipin Raichada.

Uamuzi huu ulisababisha kushtakiwa kwa Lowassa na mfanyabiashara huyu kwa madai kwamba alimshauri Rais vibaya. Uamuzi huu ulienda sambamba na raia kadhaa wenye asili ya kihindi kunyang’anywa viwanja katika eneo la mnazi mmoja ambalo walikuwa wamelivamia bila kujali kwamba ni eneo la wazi kwa kutumia fursa ya ‘ruksa’.


Akiwa waziri wa maji na maendeleo ya mifugo, Lowassa alivunja mkataba kati ya Serikali na Kampuni ya City Water iliyokuwa imekabidhiwa jukumu la kuendesha shirika la maji Dar es Salaam.
Kampuni hii baadaye iliishtaki serikali, kesi ambayo ilikuwa imemuweka pabaya Lowassa kwa maelezo kwamba alivunja mkataba husika kimakosa na alikuwa anakwenda kuisababishia serikali hasara kubwa. Bahati nzuri serikali ilishinda kesi hiyo na pengine hiyo ikawa ndiyo pona ya Lowassa.


Moja ya sifa za kikazi za urais nilizoeleza katika makala zilizopita ni bidii, weledi na umakini katika kazi. Nilibainisha kuwa “tunahitaji Rais ambaye ana historia ya bidii katika kazi popote huko alikopita, na tukimfuatilia tunaweza kuona alama yake alipopita”.
Jambo la wazi ambalo halihitaji mjadala sana ni kuwa popote alipofanya kazi Lowassa aliacha alama. Pengine jambo ambalo tunaweza kulijadili ni umakini wa maamuzi yake na kiwango ambacho alama alizoacha zilikuwa chanya na kwa manufaa ya Taifa.
Kwa upande mmoja unaona umuhimu wa kiongozi wa aina ya 

Lowassa mwenye uwezo wa kufanya maamuzi ya haraka yenye kuzingatia matokeo zaidi kuliko mchakato wa kupata matokeo husika. Hii ni taswira njema kwa kiongozi, hasa kama kuna mtu juu yake wa kuweza kudhibiti kasi ili kuhakikisha kwamba matokeo chanya yanapatikana bila kuathiri haki za watu.


Kwa upande mwingine, unaweza kumuogopa kiongozi wa aina ya Lowassa katika nafasi ya juu sana kwa kuwa kwa mtindo wake wa kufanya maamuzi makubwa kwa haraka na bila kuzingatia mchakato wa kimaamuzi anaweza kuirudisha nchi nyuma katika utawala bora na ujenzi wa demokrasia. Yote hii itategemea na nchi inahitaji kiongozi wa aina gani kwa wakati husika, maana mzee Ali Hassan Mwinyi alishatuonya kitambo kuwa kila zama na kitabu chake. Nawaachia wasomaji wafanye tathmini juu ya uhalisia wa taswira ya uchapa kazi wa  Lowassa.No comments: