Tuesday, October 14, 2014

MIAKA 15 BILA YA MWALIMU IMETUZIDISHIA MAUMIVU.Baba , Mwalimu Julius Kambarage NyerereMIAKA 15 BILA YA MWALIMU IMETUZIDISHIA MAUMIVU

Na Baraka Mfunguo,
Miaka 15 imeongeza maumivu
Wanajifanya kukupongeza kivivu
Laiti wangeweza tungezila mbivu
Miaka 15 bila ya mwalimu imetuzidishia maumivu.

Ni siku kama ya leo kwa mapenzi ya manani
Mwalimu kipenzi chetu ulipoondoka duniani
Sisi tunaokuenzi hatutasahau asilani.
Miaka 15 bila ya mwalimu imetuzidishia maumivu.

Watoto uliowaachia nyumba wamekosa umakini.
Kila wakifanyacho nchini kimetuzidishia umaskini.
Wamekosa usimamizi pamoja na dhamira ya ndani.
Miaka 15 bila ya mwalimu imetuzidishia maumivu.

Kila suala lautendaji lageuzwa la siasa
Wameacha  uwajibikaji wamekimbilia anasa
Laiti wangetambua  wangeacha vyao visa.
Miaka 15 bila ya mwalimi imetuzishia maumivu.

Miaka 15 umeondoka baba wanachokonoa muungano
Wanakiuka misingi uliyoweka kwa kigezo cha mkangamano
Wanapenda kusifiwa na kuabudiwa katika mikutano.
Miaka 15 bila ya mwalimu imetuzishia maumivu.

Walevi wa madaraka wameanza mchakato
Wanaitaka nchi kwa njia ya mkato
Wametulaghai wananchi kwa masinia ya pilau  kama  watoto.
Miaka 15 bila ya mwalimu  imetuzidishia maumivu.

Wanajifanya kukuenzi mioyoni kwa unafiki
Mambo mengi uliyofanya kamwe hawayaafiki.
Mpaka tunaanza kuwaona wamepotenza mantiki.
Miaka 15 bila ya mwalimu  imetuzidishia maumivu.

Afrika haitakusahau kwa yale uloyafanya.
Kwa utendaji na mtazamo wako kwa mambo yalo chanya.
Hawa waliobaki wamegeuka kuwa mafunza na mapanya
Miaka 15 bila ya mwalimu imetuzidishia maumivu.

Namalizia kwa kusema hautatoka moyoni
Yale ulioyafanya tumeyashuhudia machoni
Hawa uliodhani wataendelea, hawana haya wala soni
Miaka 15 bila ya mwalimu imetuzidishia maumivu.

Baba umeondoka natamani urudi
Ushuhudie jinsi wanavyoiua nchi kwa makusudi.
Namwomba mola azidi kuwahimidi ili awarudi.
Miaka 15 bila ya mwalimu imetuzidishia maumivu

No comments: