Sunday, October 12, 2014

BERNARD MEMBE: KACHERO ALIYEBOBEA, MWANADIPLOMASIA MTATA.
Na Prof. Kitila Mkumbo,(KUTOKA GAZETI LA RAIA MWEMA).

Katika mfululizo wa makala hizi zinazochambua wasifu wa wagombea urais katika Uchaguzi Mkuu ujao, leo tunamwangalia Bernard Kamillius Membe, Mbunge wa Jimbo la Mtama mkoani Lindi na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.

Kama tutakavyoona katika uchambuzi huu, huyu ni mgombea mwenye historia fupi lakini tajiri katika siasa za Tanzania na kimataifa.

Katika uchambuzi huu nimetumia vyanzo mbalimbali vya taarifa, vikiwamo machapisho mbalimbali ndani na nje yanayomhusu Membe, mahojiano na baadhi ya watu waliopata kusoma na kufanya naye kazi, taarifa za maendeleo yake kitaaluma shuleni na vyuo alikosoma, na taarifa za utekelezaji wa Ilani ya CCM katika Jimbo la Mtama.
Aidha, katika maandalizi ya makala haya, nilipata bahati ya kufanya mazungumzo ya ana kwa ana na Membe jijini Dar es Salaam.


Kuzaliwa, malezi na familia

Bernard Kamillius Membe alizaliwa Novemba 9, 1953 katika Kijiji cha
 Rondo-Chiponda, Wilaya ya Lindi Vijijini, akiwa ni mtoto wa pili katika familia ya watoto saba wa mzee Kamillius Anton Ntanchile na mama Cecilia John Membe.

Membe alifunga ndoa ya Kikristo na Dorcas Richard Masanche mwaka 1986, na wamejaliwa kupata watoto watatu-wawili wa kiume na mmoja wa kike.

Membe tunaweza kusema alizaliwa na kukulia katika hali ya maisha ya Mtanzania wa kawaida aliyezaliwa kijijini. Alizaliwa katika kijiji ambacho maji ilikuwa shida na hivyo kulazimika kutembea kilometa nyingi kufuata maji; hali hiyo ikifanya kuoga mara moja tu kwa wiki-siku ya Jumamosi.
Hapakuwa na hospitali na kwa hivyo uhai ulitegemea zaidi kudra za Mwenyezi Mungu na hekima na akili za wazazi na wazee wengine kijijini. Kimsingi haya ndiyo maisha ambayo Watanzania wengi tumekulia, hasa katika miaka ambayo Membe alizaliwa.

Baba yake Membe alikuwa mwindaji aliyelazimika kuwa hivyo. Akiwa bado mtoto mdogo miaka kama mitano hivi, wakiwa shambani, Kamillius Anton Ntanchile alishuhudia simba akimnyatia na kisha kumdaka mama yake na kutokomea naye, na walikuja kupata baadhi tu ya viungo vya mwili wake. Tangu wakati huo Kamillius akawa na ndoto ya kumiliki bunduki na kuwa mwindaji. Na kweli alipokuwa mkubwa alifanikiwa kumiliki bunduki na kuwa mwindaji maarufu, na baadaye kuiambukiza familia yake kuwa familia ya wawindaji.

Kwa hivyo, kwa maneno ya siku hizi katika siasa za Tanzania unaweza kumwita Membe kuwa ni mtoto wa mwindaji!

Baba yake Membe alifariki dunia mwaka 1987 kwa ajali ya kulipukiwa na bunduki pajani akiwa katika harakati zake za uwindaji. Kutokana na kutokuwa na huduma za afya karibu, Kamillius alikaa masaa kumi bila huduma yeyote na hivyo alifariki dunia kutokana na kuvuja damu nyingi. Kwa maelezo ya Membe, hii ndiyo hali iliyomchochea kupigania uwepo wa hospitali ya Wilaya katika Jimbo lake la uchaguzi.


Elimu

Kwa kiasi kikubwa, Membe amefuata mtiririko wa kawaida katika kusoma kwake, kuanzia shule ya msingi hadi chuo kikuu. Elimu ya msingi alisoma katika Shule ya Msingi Rondo-Chiponda (1962-1968). Utaona kwamba aliingia shule akiwa na umri mkubwa kidogo, kama miaka kumi hivi, badala ya miaka saba, ambao ndio umri wa kawaida wa kuanza shule Tanzania.

Hii nayo ni hali ya kawaida kwa Watanzania walio wengi tuliozaliwa vijijini. Shule ya sekondari alisomea katika seminari ya Namupa (1969-1972), na baadaye akajiunga na Itaga Seminari Tabora kwa kidato cha tano na sita (1973-1974).

Pengine jambo moja ambalo wengi hatukulijua kabla ni kwamba Membe alipata kusomea upadri kwa miezi kadhaa kabla ya kujiunga na Itaga Seminari. Kwa mujibu wa Paul Maokola, rafikiye Membe wa siku nyingi na ambaye kwa sasa ni mtaalamu wa uchumi na meneja miradi ya maendeleo wa Jimbo la Mtama, Bernard Membe alikuwa miongoni mwa vijana 11 waliopata wito wa kusomea upadri na hivyo walichaguliwa kujiunga na Seminari Kuu ya Peramiho, Songea.
Hata hivyo, baada ya matokeo ya kidato cha nne kutoka Membe alikuwa ni miongoni mwa vijana watatu waliofaulu vizuri sana. Kwa sababu hii aliyekuwa Askofu Mkuu wa Jimbo la Mtwara wakati huo, (sasa marehemu) Maurus Libaba, aliamua kuwahamishia Itaga Seminari, ambayo ilikuwa ni seminari pekee ya Kikatoliki iliyokuwa na masomo ya kidato cha tano na sita.

Baada ya kumaliza kidato cha sita mwaka 1974, Membe alijiunga na mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa mujibu wa sheria kwa muda wa mwaka mmoja. Wakati huo huo palitolewa Azimio la Musoma lililotaka watu wote waliomaliza kidato cha sita kufanya kazi miaka miwili kabla ya kujiunga na masomo ya chuo kikuu.

Alipomaliza kutumikia Jeshi la Kujenga Taifa, Membe hakurudi tena kuendelea na kusomea upadri kwa kile ambacho rafiki yake Maokola anaeleza kwamba alipata wito mwingine wenye masharti nafuu ya kutumikia ulimwengu.

Aidha, Membe hakujiunga moja kwa moja na chuo kikuu hata baada ya kumaliza miaka miwili ya utumishi wa lazima. Ni kwa sababu hii utaona kwamba alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1981/82 badala ya mwaka 1979 kama ilivyokuwa kwa rafiki yake Paul Maokola, akisomea shahada ya Sayansi ya Siasa na Utawala wa Umma, maarufu Mlimani kama PSPA.

Kuna sababu kubwa mbili ambazo zinaweza kuwa zilimchelewesha Membe kujiunga na chuo kikuu mapema.
Sababu ya kwanza ni kwamba tayari alishaajiriwa kufanya kazi Ofisi ya Rais na ilikuwa ni lazima apate kibali (clearance) ili kwenda masomoni.

Sababu ya pili ni matokeo yake ya kidato cha sita. Ukiangalia kwa makini matokeo yake ya Kidato cha Sita, ambayo ni ‘S’ mbili na ‘E’ moja, utaona kwamba pengine kwa matokeo haya asingepata nafasi moja kwa moja ya kujiunga na masomo ya chuo kikuu, ukizingatia kwamba kwa wakati huo nafasi katika elimu ya juu zilikuwa finyu.

Hali hii inathibitishwa na ukweli kwamba Membe aliingia Chuo Kikuu kwa kufanya mtihani unaoitwa ‘Mature Age Entry Examination’, alioufanya mwaka 1981/82.

Kwa taratibu za Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, mtihani huu hufanywa na watu ambao hawakupata alama za kuingia chuo kikuu moja kwa moja kupitia matokeo ya kidato cha sita.

Matokeo ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam yanaonyesha kwamba Membe alifaulu vizuri kwa kiwango cha kupata GPA ya 4.1. Huu ni ufaulu wa juu sana katika elimu ya juu Tanzania ambao unamuwezesha mhitimu kuajiriwa kuwa mwalimu wa chuo kikuu chochote nchini.

Taarifa zinaonyesha kwamba Membe alipewa barua ya ajira ya uhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika ngazi ya uhadhiri msaidizi (tutorial assistant).

Hata hivyo, alishindwa kujiunga na Chuo Kikuu kwa sababu mwajiri wake alikataa na kumwamuru arudi kazini mara baada ya kumaliza masomo yake.

Bernard Kamillius Membe anayo pia shahada ya uzamili katika Uhusiano wa Kimataifa aliyoipata kutoka Chuo Kikuu cha Johns Hopkins nchini Marekani mwaka 1992. Hiki ni moja ya vyuo vikuu bora kabisa kikishikilia nafasi ya 15 kwa ubora duniani (kwa mujibu wa Times Higher Education).

Malezi na historia ya Membe yanatuambia mambo mawili makubwa. Mosi, huyu ni mtu aliyekulia maisha ya kawaida katika mazingira ya Mtanzania wa kawaida kijijini. Kwa hiyo amefika hapo alipo kwa kupambana na kwa kupenya.

Pili, Membe ana elimu nzuri, na hasa elimu ya chuo kikuu. Aina ya elimu ya chuo kikuu aliyonayo inatupa picha kuhusu hulka ya Membe ya kupenda mijadala na wasomi, na hasa mapenzi yake ya kutembelea ukumbi maarufu wa Nkrumah mara kwa mara.
RAIA MWEMA


No comments: