Friday, October 10, 2014

ALIYEKUWA MWANASHERIA MKUU Z'BAR AWAZODOA WASOHAYA

Na Zanzibar Yetu,

LAITI kama si utaratibu “tuliojiwekea” kikazi, leo ukurasa huu niliridhia utoke ukiwa hauna kitu. Niliandaa tu maneno yafuatayo: “Ni masikitiko makubwa.” Utaratibu hauruhusu ukurasa kutoka wazi hata niliposema nitafungamanisha maneno hayo na picha yangu. Nilibanwa niseme japo kidogo.

Mwenzenu nilikosa maelezo. Niliishiwa nguvu ya kusema. Ninayo, tatizo sikuwa na utulivu wa moyo. Nilijawa simanzi zisopimika.
Niliumizwa. Nikawa najisikia mwili kuzidiwa joto kali lililonivaa utosini hadi nyayoni. Akili yangu kama iliyokuwa imeduru. Kama imesimama kufanya kazi – imevia au imedunda.

Rohoni najisikia vibaya; kama niliyezugwa. Awali sikujua nifanyeje.
Sikujitambua maana nilizongwa. Sikwenda kwa daktari, niliamini nitatulia siku mbili-tatu zijazo.

Nina simanzi hivi kwa yale yaliyotokea Bunge Maalum la Katiba lililokuwa katika hatua yake ya mwisho ya wajumbe kupiga kura za kuiamua Rasimu ya Katiba mpya.

Rasimu halisi iliyoandaliwa na kuwasilishwa bungeni na aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, ilikuwa na Sura 17 zilizoundwa na Ibara 271.

Rasimu iliyowasilishwa na Andrew Chenge, Mbunge wa Bariadi Magharibi na mwenyekiti wa Kamati ya Uandishi, ina Sura 19 kwa Ibara 289.

Nilikuwa peke yangu. Wala sikujali bunge maalum limefanikiwa kuipata rasimu. Hili sikuwa na shaka nalo. Chama Cha Mapinduzi (CCM) kiliwekeza sana kulifanikisha.
Mliona nguvu yoyote ya kuweza kuzuia rasimu yao katika bunge lililodhibitiwa kwa kila namna na dola ya CCM?

Kama mwenyekiti ni Samwel Sitta, serikali inayogharimia ya CCM, rais wa jamhuri na wa Zanzibar CCM na hao ndio waliodhamiria mapema kuivuruga katiba ya wananchi, nani azuie?

Kwa bahati njema, dhamira yao imemridhi Mola. Ana makusudi anaporuhusu wanaadamu kutenda uovu. Viumbe wake hatupaswi kudadisi.

Kilichoniumiza ni rasimu ilivyopitishwa. Ushiriki wa Wazanzibari.

Lakini kilichonigusa hata kunidhuru, ni wana-CCM kutoka Zanzibar walivyoruhusu rasimu kupitishwa vile na kuhitimisha kwa shangwe za mapinduzi daima.
Labda wenzangu hamjaona. Wazanzibari kutajwa kufanikisha rasimu itimize theluthi mbili (2/3 au mbili ya tatu), kumedhihirisha mgawanyiko.

Kuna mgawanyiko kwa Watanzania wa Tanganyika katika suala hili. Wazanzibari nao wamethibitisha kugawanyika.

Sigusii kilichowapasua Watanzania wa Tanganyika. Hili lina siku. Wazanzibari wamegawanyika kwa kukosa uongozi madhubuti. Na kule kusabilia sehemu ya mamlaka ilipoungana na Jamhuri ya Tanganyika 1964, ingali tatizo.

Muungano uliandaliwa kukidhi maslahi ya kisiasa zaidi. Ndio maana na uendeshaji wake unakuwa kwa misingi hiyohiyo ya kisiasa. Muungano siasa tupu. Basi na uingiaji wa viongozi Zanzibar, unaathiriwa nazo.

Mmesikia wapi nchi iliyoungana ikakosa mambo ya maslahi nayo wakati wa kuandika katiba mpya inayohusu muungano huo? Ni Zanzibar peke yake?

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, anayoiongoza Rais Dk. Ali Mohamed Shein, haikuweka mambo ya kutumaini. Mnakumbuka tulipigania msimamo; wajumbe hata wa CCM katika Baraza la Wawakilishi, walipigania. Sote tukapuuzwa.
Ni ujinga tu leo baadhi ya walewale CCM waliopuuzwa walipotaka msimamo wa kuutetea bungeni, wanajitia hamnazo na kumshambulia Mwanasheria Mkuu Othman Masoud Othman.

Eti kamsaliti Rais. Hakumshauri. Kama vile walimuuliza akasema kweli hakumshauri. Hawa wanajua alichokisema Makamu wa Pili, Balozi Seif Ali Iddi pale Barazani.

Walikuwepo, aliyekosa alisimuliwa, Balozi aliposema wakati akifunga mkutano wa baraza Disemba 2013: “Wajumbe mkatumie akili zenu, kila mmoja atumie akili yake mtapokwenda Bunge Maalum la Katiba. Serikali haina msimamo wa kuwaambia.”

Ndivyo alivyokijibu kilio cha wawakilishi kutaka semina pamoja na wabunge Wazanzibari waelewane mambo muhimu ya kuyashikilia hadi yajumuishwe katika katiba mpya.

Tulishawishi uongozi ulielewe hili. Ah wapi, wakaziba mashikio. Wakajizuia kusoma tuliyoyaandika kuhimiza. Hawa bado wanaamini nchi ni yao wao tu, wengine dhambi.

Uongozi unajua vizuri una nyaraka zenye malalamiko ya namna Zanzibar isivyopewa mamlaka ya kuamua wapi na kwa nani ikope na inavyopangiwa wa kushirikiana naye.

Vilevile wanajua Serikali ya Muungano (SMT) imeweka mifumo, na inaitii, ya kisheria na kimazingira ya kuibana Zanzibar ili ilazimike kusubiri huruma kwa kila inachokitaka kwa hayo machache niloyataja.
Hivi viongozi wanadhani hayo huondoshwa kwa lelemama? Wanajua yamekuwa yakijadiliwa bila ya ufumbuzi kupatikana. Wanajua hata ulipopatikana kwa kuwepo mapendekezo, SMT wanagoma kutekeleza.

Ushahidi ni kodi mbili kwa bidhaa ziingiazo Zanzibar. Kuficha mapendekezo ya Tume ya Pamoja ya Fedha (JPC) kuhusu mapato ya Muungano na mgawanyo wake.

Leo, watu waliotulia akili na kutambua tatizo la uendeshaji Muungano usio wa haki/usawa wala maridhiano/kuheshimiana, wameipata nafasi kuyaeleza haya kwa ufasaha ili katiba iyatambue na kuyatafutia dawa, wanazembea.

Balozi Seif, msemaji wa serikali barazani na popote, siyo tu anachekelea, kwa hakika ameyaridhia. Aliyoyasema, wacha aliyotenda ufichoni Dodoma, yanazidi kushuhudisha namna CCM wanavyolea tatizo.

Basi kwa Zanzibar kukosa msimamo, licha ya kauli za Jaji Warioba kuwa Wazanzibari wamoja kwa mambo yenye maslahi na nchi yao, wajumbe wakagawanyika.

Ikaanzia na kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kutoka bungeni. Wajumbe 66 waliondoka kwa kutoridhika na majadiliano yalivyokuwa.
Pia walijiridhisha kuwa CCM ilishajipanga kuivuruga rasimu yenye maoni ya wananchi ili kulazimisha yao. Madai ya UKAWA yakapuuzwa. Eti hawajui kilichowatoa.

Kwa hivyo, kwa awamu yote – baada ya Sura ya Kwanza na Sita kujadiliwa awamu ya kwanza kufikia Aprili 16 UKAWA walipotoka – iliyohusisha kujadili rasimu kwenye kamati, mpaka kuandika rasimu ya kupendekezwa, na hatimaye kuiamua, hawakushiriki.

Majadiliano yalikuwa ya mtizamo wa vyama viwili vikuu kikiwemo Chama cha Wananchi (CUF) vinavyovutana kila kimoja kikiamini Jamhuri inapaswa kuendeshwa chini ya muundo wa serikali tatu, badala ya mbili zinazoendelea kushikiliwa na CCM.

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na NCCR-Mageuzi, kama CUF, navyo vinaamini Muungano wa serikali tatu.

Majadiliano yakawa malumbano; mashambulizi na kashfa za kutunga; tena yakaja matusi ya nguoni – mnakumbuka Mama Asha Bakari Makame, makamu mwenyekiti wa UWT-CCM, alichokitenda ukumbini.

Nasema laiti uongozi Zanzibar ungetimiza wajibu wake – kutoa uongozi mwema na kujenga hoja kinchi ikizielekeza kwa wajumbe Wazanzibari, hayo yasingetokea.

Yangetokea, matarajio ya wananchi ni uongozi kuwaonya watakuwa wanasaliti wananchi. Nani hapo angeinua sauti akahoji viongozi? Thubutu!

Kinachosikitisha wananchi, ambao wananibana nilalamikie udhaifu unaogharimu nchi yao, ni kwamba viongozi wa CCM, maana ndio wenye hatamu ya uongozi, wameyapalilia hayo.
Utasemaje kama maneno ya kuhitimisha Bunge ndiyo yale aliyoyatoa Balozi Seif, alipopewa nafasi ya kusema neno bungeni?

Hivi wewe unayesoma hapa sema ukweli wako, yale maneno yake msaidizi na mshauri mkuu wa Rais Dk. Shein ni ya kuijenga au kuibomoa Zanzibar? Ila makada wanafanya uchuro kumshambulia mshauri wa sheria. Ametumia usomi wake akatofautiana na wasohaya.


Sijajadili takwimu za kura zilivyonajisiwa.


ZANZIBAR YETU

No comments: