Tuesday, September 30, 2014

YA MAHAKAMA YA KADHI NA RASIMU YA KATIBA MPYA


KHIDMAT DWAAT LISIAMIYAT CENTRE REGISTERED TRUSTEES.
P. O. BOX 16106, MOB. 0713-290272, 0784-403020.


1. Uanzishaji wa Mahakama ya Kadhi utaleta madahara makubwa ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa vile Wakristo hawagawanyiki katika suala la kuipinga, lakini sisi Waislamu tunagawanyika katika suala hilo. Kwa taarifa yako napenda nikuhakikishie kuwa Waislamu wa Madhehebu ya AnsarSunna HAWAIKUBALI Mahakama hiyo kwa vile wanaelewa kuwa itakuwa chini ya BAKWATA.

2. Pia wanaelewa kuwa miongoni mwa mamlaka ya Kadhi ni kutangaza mwezi wa Ramadhani kufunga na kufungua na wao wanaye Amir wao ambaye hutangaza mwezi kwa kufuata mwezi unaoandama Saudia (Saud Arabia). Kwa maana hiyo katika nchi yenye Kadhi kutokea mtu mwingine nje ya Kadhi kutangaza mwezi ni kosa la jinai.

3. Kitu ambacho kitaleta madhara makubwa kuliko mafanikio ingawa AnsarSunna ni kundi dogo lakini wanaburuza kundi kubwa sana la Waislamu, kuliko Taasisi yoyote ya Kiislamu hapa Tanzania kwa vile ushawishi wao ni mkubwa sana katika jamii ya Kiislamu.

4. ANSAR SUNNA ndio wanaoendesha Shuura ya Maimam, GAZETI LA AN-NUUR, AL-HUDA, NASAHA na RADIO IMANI. Pia wana ushawishi mkubwa TIMES FM. Je, BAKWATA wana uwezo wa kupambana na vyombo hivyo?

5. Je, Serikali inaweza kukabidhi Mahakama ya Kadhi kwa wanaharakati wa Kiislamu? Nina hakika haiwezi kufanya jambo hilo na kama haitofanya hivyo Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinaweza kupata hasara zifuatazo:

(a) Wakristo wote wanaweza kujitoa ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kujiunga katika chama cha CHADEMA ambacho hakina Mahakama ya Kadhi katika Ilani yake.

(b) Waislamu wote walioko chini ya Shuura ya Maimamu ambayo ni Mpinzani Mkuu wa BAKWATA wataendelea kuipinga Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwa kuikumbatia BAKWATA na huku wakiendelea kuiunga mkono CUF, hivyo CCM itajikuta imebakia na Waislamu wanaoiunga mkono BAKWATA tu. Suala la wanaharakati kuipinga Mahakama ya Kadhi ni jambo rahisi sana kwa vile Mahakama ya Kadhi sio madai yao ya msingi.

6. Waislamu (wanaharakati) dai lao la msingi ni MGAWANYO SAWA WA MADARAKA. Hivyo Serikali inapounda Wizara, wao hutizama Baraza la Mawaziri, WAISLAMU NI WANGAPI NA WAKRISTO NI WANGAPI NDIO MAANA WANAIUNGA MKONO CUF, KWA VILE CUF IMEELEWA TATIZO LAO NA WAO WAKAJA NA KAULIMBIU YA HAKI SAWA KWA WOTE, yaani kwa Wakristo na Waislamu, wala Ilani ya Uchaguzi ya CUF haisemi lolote kuhusu Mahakama ya Kadhi WALA HAITOSEMA!!

7. Pia Waislamu wanaharakati wanaelewa kuwa Mahakama ya Kadhi haina manufaa yoyote kwa Waislamu, kwa vile Zanzibar ipo na WAISLAMU WA ZANZIBAR HAWANA MAENDELEO YOYOTE KUWAPITA WALE WA BARA, NA UISLAMU SI NDOA NA MIRATHI TU WALA MUNGU HASEMI "SOMETHING IS BETTER THAN NOTHING." Huu ni msemo wa Wazungu.

8. Mwenyezi Mungu anasema: INGIENI KATIKA UISLAMU WOTE NA MSIFE BALI MMEKUWA WAISLAMU KAMILI (Surat Baqarah ya 2 aya ya 208). Kwa hiyo mimi nikiwa kama Mwislamu nashauri kuwa Mahakama hiyo ISIWEPO kwani haitakuwa na manufaa kwa Chama cha Mapinduzi (CCM) na italeta mgawanyiko miongoni mwa wanachama wako, chukulia mfano Zanzibar, Mufti na Kadhi wanavyopingwa na wanauamsho ambao wanaongozwa na Sheikh Farid hali wanauamsho ndio Shura ya Maimam na Shuura ya Maimam ndiyo Uamsho.


KWANINI MASHEIKH WA BAKWATA WANAITAKA?

9. Wanaelewa wanachokifanya, wao wanajua fika kuwa Serikali itakapoanzisha Mahakama ya Kadhi watakuwa wamepata AJIRA, kwa hiyo wao wanapigania maslahi yao tu, hawawezi kuangalia madhara yatakayokikumba Chama Cha Mapinduzi (CCM) na huku wakijua kuwa ushawishi wao ni mdogo katika Jamii ya Kiislamu na hawana hata Miundumbinu ya kuwashawishi Waislamu wote waweze kumkubali Mufti, na hali ya Mufti ameshaweka wazi milango kwa Taasisi zote za Kiislamu na Waislamu waje washirikiane naye.
10. Masheikhe hawa wanaelewa kuwa hakuna Hakimu anayehukumu makosa mawili tu, yaani NDOA na MIRATHI, ukiletewa mzinifu huruhusiwi kumhukumu, ukiletewa mwizi huruhusiwi, nk. lakini wanang'ang'ania hivyo hivyo kwa ajili ya mishahara tu na hiyo ni hatari.

11. Hujaribu kutoa hata mifano ya Serikali ya Uingereza kwamba mwaka 1920 iliweka Mahakama hizo, ukweli ni kwamba Serikali ya Uingereza haikuweka Mahakama za Kadhi tu bali za Maakida na Maliwali, lakini pia sababu ya kuziweka Mahakama hizo siyo kwa ajili ya kuutunza Uislamu au uliwali bali ilikuwa ni mbinu ya kuwatuliza Viongozi hao ili waweze kuwatawala bila vurugu kwani mkoloni aligundua kuwa ni watu wenye ushawishi katika jamii kwa hiyo ile ilikuwa ni mbinu ya kiutawala ili Masheikhe, Maliwali na Maakida wajione kuwa na wao ni sehemu ya Serikali ya Muingereza, kumbe ni watawaliwa, hivyo bado hoja hiyo haina msingi wowote wala haina maana kwamba Serikali ya Mkoloni ilikuwa nzuri kwa Waislamu kuliko hii ya CCM, na huku tukiambiwa kuwa Waislamu ndiyo walioanzisha harakati za kudai Uhuru, kama walikuwa wazuri kwa nini tuliwaondoa.


12. CCM inayo mambo mengi ya kujivunia kwa Waislamu kama vile kuwapatia Chuo Kikuu, na hilo ni jambo muhimu na la msingi kwa maendeleo ya Uislamu na Waislamu, kwa hiyo JAMBO HILO LA MAHAKAMA YA KADHI mnapaswa kuliangalia kwa umakini ijapokuwa limo ndani ya Ilani yenu. Lakini si kila jambo lililomo ndani ya Ilani litekelezwe, mengine yanaweza kushindikana kwa matatizo mbalimbali na hili ni tatizo kubwa KWANI LINAWEZA KUZAA MGOGORO WA KIDINI!!

WAKRISTO WANA HAKI YA KUPINGA MAHAKAMA YA KADHI
13. Sehemu kama Zanzibar ni rahisi kuweka Mahakama ya Kadhi kwa vile Waislamu kule ni asilimia 99.99 hali kama hiyo Wakristo kule ni kama hawapo wamemezwa kwa uchache wao. Lakini BARA NI PAGUMU kwa vile HUENDA WAKRISTO NI WENGI KULIKO WAISLAMU. KWA VILE WAISLAMU KWA UHAKIKA HUPATIKANA MIKOA ISIYOZIDI SITA AMBAYO NI DAR ES SALAAM, LINDI, TANGA, MTWARA, KIGOMA NA TABORA, pia katika mikoa hiyo siyo Wilaya zote, kwa mfano Mkoa wa Kigoma ni Ujiji na Kigoma Mjini tu.

14. Pamoja na hayo Masheikhe wa BAKWATA wanaoshikilia suala la kuwepo kwa Mahakama ya Kadhi bado hawajafahamu nini tatizo la Wakristo, hata hawakubali kuwepo kwa Mahakama hiyo, siyo kweli kabisa kwamba Wakristo hudhani Mahakama hizo zitawahukumu wao, la hasha na Masheikhe hutumia muda mwingi kuwaelimisha juu ya hilo, wakati hilo sio tatizo lao, na ni udhaifu wa kutokujua madai au matatizo ya mpinzani wako, ni nini tatizo la Wakristo ni hili:
(a) Mkumbuke kwamba mwaka 1993 hapa Tanzania kulikuwa na mgogoro wa bucha za nguruwe, mgogoro huo ulizaa harakati kubwa za Waislamu ambazo makao yake makuu yalikuwa msikiti wa Mtoro na kiongozi mkuu alikuwa marehemu Kasim bin Juma. Waislamu walipinga kuwepo Ubalozi wa Vatican hapa Tanzania na bado wanaendelea na msimamo huo hadi leo, wakati ubalozi huo hauendeshwi kwa Fedha za walipa kodi wa Tanzania bali ni Vatican yenyewe. 

JE, ITAKUWAJE LEO WAKRISTO WAKUBALI ZIWEPO MAHAKAMA AMBAZO ZITATOA AJIRA KWA WAISLAMU, KUANZIA MTAA, KATA, TARAFA, WILAYA, MKOA HADI TAIFA, TENA KWA FEDHA ZA WALIPA KODI WA TANZANIA WAKIWAMO NA WAO WAKRISTO? 

Hilo ndilo tatizo lao na hapo ndipo BAKWATA wanatakiwa wapatolee maelezo.
(b) Kwamba, mabilioni ya Watanzania yatakayowalipa Masheikhe kila mwezi nao wao watanufaikaje? Huo ndio mgogoro uliotengenezwa na Ilani yenu na ambao unaweza kuwagharimu katika uchaguzi ujao wa mwaka 2010 ENDAPO WAKRISTO WAKIIGA MFANO WA WAISLAMU WA MSIKITI WA MTORO walipoamua kukusanya Kadi za CCM mwaka 1993 ingawa jaribio hilo lilizimwa na Viongozi wa CCM.


HOJA ZA SHEIKH BASALEH

15. Sheikh Ali Basaleh ndiye ambaye amelielewa tatizo la Maaskofu ingawa ametoa mfano mzuri wa kuwatuliza katika kipeperushi chake cha Wito cha tarehe18/08/2006. Ijumaa kuwa kama mtu ana watoto wawili mmoja anakula sana na mwingine hali sana, Je, baba atamzuia yule anayekula sana ili alingane na yule asiyekula sana? Mfano wake ni mzuri lakini haufanani na tatizo lililopo kwani fedha za baba hazichangiwi na watoto wake, bali baba huzitafuta yeye mwenyewe kwa nguvu zake, LAKINI FEDHA ZA BABA SERIKALI ZINATOKANA NA KODI YA WAISLAMU NA WAKRISTO, HIVYO SERIKALI HAIPASWI KUTUMIA FEDHA NYINGI KWA DINI MOJA LAZIMA ITALETA MGOGORO NA NDIYO MAANA SISI WAISLAMU TUMEKUWA TUKIDAI HAKI SAWA!
16. Katibu Mkuu ni matumaini yangu kuwa hekima itatumika katika kulitatua tatizo hilo kwani ni rahisi kuziba ufa kuliko gharama za kujenga ukuta mwisho nakutakia kazi njema pamoja na afya njema.


WABILAH TAUFIQ,
ASANTE.
USTADH A. S. MKAMBAKU,

KATIBU MKUU.- JAMII FORUMS

No comments: