Tuesday, September 30, 2014

SUMU YA RASIMUNa Makengeza,

Wabongo sina hamu nao. Juzi tulipokuwa sebuleni jamaa mmoja alituchekesha kweli hadi wengine walipaliwa na supu zao.

‘Aisee, mimi napenda sana polisi wanavyofanya kazi siku hizi?’

‘Hawakudai rushwa tena?’

‘Achana na wale. Juzi kuna wezi walitaka kuvunja nyumba yangu usiku. Basi tulipoona hali mbaya, mke wangu akapiga simu polisi wakati mimi natafuta sime. Majibu kama kawaida … ‘Oh hatuna petroli, huwezi kutuletea M-pesa kidogo tununue na majibu mengi ya kukera, hadi mke wangu akakata simu kwa hasira. ‘
‘Hapa kuna nini cha ajabu? Yaleyale.’

‘Ngoja Bwana. Mbona kiherehere kama mheshimiwa mbele ya posho? Wakati nasikia wezi bado wanatafuta jinsi ya kupenya na mimi nilipiga simu polisi. ‘Jamani eee, kuna vijana wamejikusanya hapa, eti wanajiandaa kuandamana kupinga Bunge letu tukufu la Katiba.’
‘Wacha wewe’

‘Ndiyo. Nakuambia hata dakika kumi hazikupita, polisi hao! Tena walikuja na kasi ya ajabu na magari matano na deraya na mabomu ya machozi na maji ya kuwasha hadi wale wezi hawakufurukuta tena. Nadhani bado wanajikuna huko selo. Sisi tu tulibaki ni athari kidogo ya mabomu yale, lakini angalau sisi tulikuwa salama na wezi sasa wameswekwa ndani bila kuona ndani.’
Duh!’

‘Kabisa. Kwa hiyo, mambo yamebadilika. Eti utoe taarifa ya wizi au uhalifu wowote, umepitwa na wakati. Ukiona jambo lolote siku hizi, piga simu na ongelea maandamano. Hapo magari yao yanafufuka na petroli inajitokeza kama miujiza. Udumu mchakato wa kutibua.’

Basi wacha watu wacheke. Na wengine waliongeza.

‘Siku hizi ya nini kuandamana ili uandamwe. Tangaza maandamano na polisi watafanya maandamano kwa niaba yenu. Kaa pembeni na waangalie tu na wakimaliza maandamano yao, tangaza maandamano mengine sehemu nyingine, ili mradi wazunguke mji mzima wakiandamana siku nzima. Senema ya bure nakuambia.’
Ndiyo maana nawapenda sana Wabongo. Si tu kwamba kila mtu ana wazo lake tofauti na mwenzie (na sijui wangapi wako tayari kweli kuwasikiliza wengine na kupima iwapo wana hoja au la), lakini wanajua kugeuza hata hali mbaya ili hali ya kuwafaidi wao.

Lakini siyo wote waliokubali. Mwingine alikasirika sana.
‘Huu ni upumbavu kabisa, eti kuvuja kwa pakacha. Ukiwa umebeba samaki na wameanza kuoza, unapata nini pakacha ikivuja?’

‘Una maana gani?’

‘Sasa kodi zetu wananchi zinatumika kutuzuia sisi wananchi tusiweze kupinga matumizi mabaya ya kodi zetu wananchi.’

Watu wakacheka.
‘Mnacheka nini? Miaka yote hii tunaambiwa kwamba hakuna fedha za kuboresha jeshi la ndani. Hawawezi kujengewa nyumba bora, hakuna hata fedha za kununua karatasi za kuandika maelezo sembuse gari linalofanya kazi na petroli ya kutosha. Ghafla vitu vyote hivi vipo, tueleweje? Hakuna fedha za kuwakamata wezi na mafisadi, lakini za kutupiga kichwani zipo za kutosha. Mwisho tutaanza kupigwa kwa kukataa kutoa rushwa, eti ni kutotii amri halali bila shuruti.’

Watu wakacheka hata kama yule alinuna. Mwingine aliamua kubadili mada.

‘Lakini tusiwalaumu sana ndugu zetu wenye rungu ya dola. Hayo yote ni matokeo ya kuchakachua mchakato laivu. Kwa kuwa wameanza kuburuta, lazima waburute hadi mwisho.’
‘Kweli kabisa. Lakini ni wajanja pia, maana naona katiba sasa imekuwa dili ya uchaguzi. Wakati wa uchafuzi mkuu, watu wanaahidi hili au lile, badala ya kuongelea sera kiasi kwamba imebidi kuweka watu kukusanya ahadi zote zinazotolewa kila mahali. Sasa ni katiba. Hawa wa bangi maalumu ambao walichaguliwa hapo awali kwa kutotaka katiba, sasa wanasikiliza kila kikundi na kuweka maneno matamu yanayowahusu ili mradi wajenge uhalali wa kubomoa rasimu na kuweka ya kwao.’

‘Kabisa. Bado nauliza ni wajenzi wa aina gani wanaohangaika kurembesha paa wakati misingi haina nguvu. Hawajaona yaliyotokea huko Nigeria. Kupandisha jengo, hata likiwa jengo zuri namna gani, juu ya misingi mibovu ni kukaribisha janga, mporomoko na vifo vya watu. Hata ukiwa mtabiri namna gani au ukiwa umevimbiwa na kutawala miaka yote hii, jengo ni jengo na misingi yake haiwezi kupuuzwa.’

‘Na ahadi hizi za kutuhadaa ni duni kabisa, maana wamebomoa misingi kwa hiyo nakshi za juu ni sura tu ya kutudanganya.
Hapo kijana mmoja alibisha.

‘Si kweli. Sisi vijana tunashukuru. Hii rasumu mpya …’

‘Rasimu Bwana …’

‘Sumu … simu yote hali moja. Rasumu hii ni kiboko. Unaona hatimaye tumepata hata baraza la vijana.’

‘Ohoo mwenzangu, unaona unavyodanganyika kirahisi. Suala si kuona kama hiki au kile kimepachikwa. Yale mambo ya msingi mbona yameondolewa.’
‘Lakini wameweka na ardhi pia.’

‘Kwani ardhi isingekuwepo? Chini ya mapendekezo ya Serikali tatu, ardhi ingekuwepo kwenye Katiba ya Tanganyika.’

Mama mmoja naye aliingia.

‘Hapana, lazima tushukuru,maana hata mambo ya jinsia yameingia.’
‘Mmh, nyinyi kinamama mmeshasahau wakati wa mapambano ya Sera na Sheria ya Ardhi. Wengine walipigania kwanza ardhi ibaki mali ya Watanzania, wakati wengine walitaka tu kuhakikisha kwamba mwanamke ana haki ya ardhi. Tukawauliza, haki ya ardhi ya nini iwapo ardhi imechukuliwa na wawekezaji. Si mwanamume, si mwanamke atapata kitu. Linda mambo ya msingi kwanza. Na watu wakajenga umoja sana hadi Serikali ikaona kuna hatari ya kushindwa, ndiyo maana walibadilisha sheria kusema kwamba wanawake wanaweza kumiliki ardhi. Basi wanawake wengi walihamia upande wa Serikali na ardhi yetu ikazidi kuchukuliwa na wawekezaji. Angalia huko Loliondo, angalia mashamba ya jatropha.’
‘Lakini hii rasumu mpya sasa inalinda ardhi …’

‘Naona hunielewi kabisa. Sawa wamesema. Lakini hayo yote ni kutufanya kukubali rasumu yao kama unavyoiita. Vijana wafurahie baraza lao, wanawake wafurahie kwamba jinsia ipo ili mradi kila mtu akubali kwamba yale ya msingi si ya msingi tena. ‘
‘Lakini ni mapendekezo mazuri.’

‘Nani anabisha. Suala ni kwamba bila kuangalia yale ya msingi wa uhusiano wetu kitaifa na uwezo wa kuwajibisha viongozi wetu na mamlaka yetu sisi wananchi, hayo mengine ni pipi tu.’

‘Duh, we angalia Bwana maana unavyowashwa na hii rasumu, mwisho utakuta unajikuna selo sasa. Hujui kwamba sasa tunatawaliwa kimabavu kabisa. Hatuna hiari tena, ni shuruti tu.’

Wakati anaongea hivi, tukasikia ving’ora kwa mbali. Kila mtu alisambaratika bila kuangalia nyuma.
MWANANCHI

No comments: