Friday, September 12, 2014

BURIANI GABRIEL MWASYEBULE UMASKINI WETU WA FIKRA NDIO CHANZO CHETU CHA KUKOSA MAENDELEO.Na Baraka Mfunguo,

Naandika nikiwa nimekwazwa na kuhuzunishwa sana na tukio lililotokea mkoa wa Mbeya wa kijana kuuawa kwa imani za kishirikina ati alikuwa anawafanya watoto misukule na kuwatumikisha ili afanikiwe kibiashara. Kijana Gabriel Mwandemwa ama Mwasyebule  wa kijiji cha Ikamambanda ameuawa tena ameuawa na watu ambao ni jirani zake, watu anaokula nao na kucheka nao wakimtuhumu tuhuma ambazo hawana uthibitisho nazo.

Uthibitisho waliokuwa nao kwake yeye ni maendeleo yake katika kilimo, ujenzi wa nyumba yake ambayo ameweka maru maru na gypsum pamoja na mipango yake ya baadaye ya kununua gari kulingana na biashara zake. Hao ni Watanzania, watanzania ambao ni mafukara na maskini wa kutupwa wa kufikiri. Kwao wao, maendeleo ni ufisadi, uchawi ama wizi au kuuza madawa ya kulevya ama kwa wanawake kuuza miili yao ama kupewa pesa na wanaume. Dhana ya kijinga na ya kipumbavu kabisa ambazo sio ngeni katika maisha yangu.

Hivi sisi ni nani aliyetufumba macho kiasi cha kuamini kwamba maendeleo ni uchawi? Na huko makazini wapo watu ambao huficha maendeleo yao kwa kigezo cha kufuatwa fuatwa  na vyombo vya sheria hata kama maendeleo hayo yametokana na juhudi zao. Ukijenga nyumba ya ghorofa utafuatwa na TAKUKURU, Usalama wa Taifa, TRA. karibia vyombo vyote vya sheria swali litakuwa. "Umejenga nyumba kubwa kama hii, hii pesa umepata wapi?" Na unakuta mtu yuko makini serious kweli kweli anataka kujua  na atataka kupata mpaka taarifa zako za kibenki ili aweze kuona mchanganuo na kubaini na kupata uthibitisho wa  kile unachokisema. 

Dhana hii nadhani ndio ugonjwa ambao unaotutafuna watanzania kwa sasa. Hatuna utamaduni wa kufanya kazi kwa bidii, juhudi ama maarifa na matokeo yake ni kuanza kukaa vijiweni na kuanza kupiga porojo za majungu dhidi ya watu. Hebu tujiulize huyo Mwasyebule amewakosea nini hao wanakijiji wenzake? Ndio hata kama tuhuma zao zingekuwa zina uthibitisho, je ni halali kumfanyia unyama ule?

Huu ndio umaskini ambao hautofautiani na ule wa kuwaua binadamu wenzetu ili tupate viiungo vyao ambavyo tunaamini tukivitumia tutatajirika, ama dhana ile ya kuwaua vikongwe kwa tuhuma za ushirikina.Akili zetu zimekaa kwenye masuala ya chuma Ulete (Mtwara wanaita cheje ama chitola) ili tuendelee. Hatukatai kwamba mambo hayo yapo. Lakini hebu tuangalie na wahenga wetu waliwezaje kutatua mambo yale. Mimi ninavyokumbuka kadiri ya hadithi za zamani nilizosoma watu wa aina hii walitafutiwa mahala pao wenyewe. Walitengwa! Sio kuuawa!


Maendeleo ya mtu yamekuwa kigezo cha kumtafutia sababu. Mas'aala haya si mageni kwangu kuna wakati nilipata changamoto ya kimaisha na watu wakaanza kusema afadhali alikuwa anaringa sana akiwa anapita na gari lake, bora atembee kwa miguu kama sisi yaani watu wako wa karibu kabisa wanakung'ong'a na wengine makazini wakadiriki kubambika tuhuma za wizi wa fedha na tuhuma ambazo hazielezeki. I mean seriously? Wakati nahifadhi pesa yangu, ama nimechukua mkopo hukuwepo umeiona gari unaanza ushabiki. Hao ndio watanzania. Na wakati ule wa Mwalimu hali ilikuwa mbaya zaidi maana ukionekana na sabuni za Rexona, Lux, Lifebuoy na mafuta yale ya mikebe ulikuwa unaitwa mlanguzi ama mhujumu uchumi kutokana na hali ya kisiasa wakati huo. Hii dhana ya kipumbavu na kijinga tumeibeba mpaka sasa ingawa watawala wetu wakati ule walikuwa na nia njema ya usawa.

Umefika wakati wa kubadilika sasa na ni wakati wa Serikali kupitia Wizara ya Elimu kuutazama upya mtaala wa Elimu ya Kujitegemea ambao wameutupa katika pipa la taka na kuubadili kuwa mtaala wa ujasiria mali. Nitakuja kuandika makala yake  ndefu nikiielezea dhana ya mtaala wa kujitegemea na ule wa ujasiriamali na faida zake ukianza kutumika mashuleni kuanzia shule za awali nikipata nafasi. Mtaala wa kujitegemea hauna tofauti na ule wa ujasiriamali kwani dhana nzima ya kujitegemea iliendana sawia na uzalishaji mali pamoja na kuzalisha kipato kutokana na kile ulichokizalisha sanjari na kukufanya usiwe tegemezi. Serikali inatakiwa iende mbele zaidi ya hapo ili kukabiliana na athari ya ukosefu wa ajira. Zamani mwanafunzi wa darasa la saba alikuwa amekamilika .

Sasa hivi tunazalisha fikra ambazo zinafikiria bongo flava, udaku, filamu za ngono na bongo movie, madawa ya kulevya, uchangudoa na wizi ama udokozi pamoja na umaskini wa fikra. Sina maana mbaya na wahusika wasikwazike ila ni lazima tutambue wahusika wa bongo flava, bongo movie ni watu wenye vipaji vyao na sio kila mtu atafanya bongo flava ama movie. Watanzania tunatakiwa tubadilike, tuamke la sivyo tutaachwa mbali sana na wenzetu. Yapo mambo mengi ambayo ni changamoto za kimuundo na za kisera katika nchi lakini ni vyema kwanza tukarekebisha akili zetu, mitazamo yetu na fikra zetu katika ulimwengu huu wa sayansi na teknolojia.


Buriani Mwasyebule, buriani jembe mimi nakuita jembe hata kama wao wamekutuhumu kuwa ni mchawi. Wamefaidika na nini walivyoutoa uhai wako? Wao ndio wachawi na watahukumiwa na dhamira zao kutokana na hila zao. Mwasyebule ulijitahidi katika kilimo cha viazi, ukajenga nyumba ukanunua pikipiki na ulikuwa na mpango wa kununua gari hizo ni juhudi zako binafsi. Lakini wamezikatisha Mungu atawahukumu.

Mwisho nawapa rai wajasiriamali wote wasikate tamaa ama kukatishwa tamaa na masuala haya ambayo mara nyingi yanachangia kuwakwamisha. Wasonge mbele wafanye kazi kwa bidii, juhudi na maarifa, walipe kodi ya nchi ili nchi iwe na maendeleo. Hii haimaanishi kwamba hawapo wale ambao sio waaminifu, wapo ila tunatakiwa tuache sheria ichukue mkondo wake dhidi yao. Tuache kujichukulia sheria mikononi, tuachane na dhana za kipumbavu na za kijinga zilizopo vichwani mwetu ambazo ndizo zinazoturudisha nyuma.

No comments: