Friday, September 26, 2014

AJIRA: SASA NI WAKATI WA KUFIKIRI NJE YA BOKSI
Na Ali Mufuruki,

KUNA matukio mawili ya siku za karibuni ambayo yanatakiwa kutazamwa na kila mmoja wetu kwa mapana yake kuhusu tatizo la ajira hapa nchini.
Benki Kuu ya Tanzania (BoT) pamoja na Idara ya Uhamiaji zilitangaza nafasi za kazi. Katika maombi yaliyotumwa, ingawa nafasi za kazi zilizotangazwa zilikuwa chini ya 100, maombi ya kazi yalizidi maelfu.


Katika suala la Uhamiaji, waombaji walifikia 70,000, kiasi kwamba ilibidi usaili uende kufanyikia katika Uwanja Mkuu wa Taifa jijini Dar es Salaam. Hili si jambo dogo.
Ripoti ya karibuni zaidi ya Benki ya Dunia (WB) inaonyesha kwamba katika kipindi cha miaka 15 ijayo, Tanzania itakuwa na nguvukazi ya watu milioni 40 ambao watakuwa wakihitaji ajira zenye staha.

Takwimu za serikali zinaonyesha kwamba kwa mwaka, vijana zaidi ya 800,000 wanamaliza masomo yao katika ngazi mbalimbali na hivyo wanataraji kuingia sokoni na kukuta ajira zao zikiwa atayari.
Kwa hali ya sasa ya uchumi wetu, idadi hii ni kubwa sana. Nimefanya utafiti katika mashirika makubwa yanayoajiri watu wengi zaidi hapa Tanzania na nimebaini kwamba waajiriwa hawazidi 20,000 kwenye sehemu hizo.

Na hapa nazungumzia mashirika makubwa kama vile Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Shirika la Reli, Mohamed Enterprises pamoja na Mamlaka ya Bandari za Tanzania (TPA).
Mashirika yote haya, kama utayajumuisha kwa pamoja, hayana wafanyakazi walioajiriwa zaidi ya 30,000.

Nimewahi kuzungumza na baadhi ya viongozi wa taasisi hizo na kusema kweli wengi wao wanaamini kwamba kama yangekuwa maamuzi yao, wangepunguza idadi kubwa ya wafanyakazi ilionao kwani kwa sasa ni mzigo mkubwa kuwa na idadi kubwa ya wafanyakazi ilizonazo.
Hii maana yake ni kwamba kama tutaenda kama tunavyokwenda sasa, nchi hii haitaweza kukidhi matamanio makubwa ya nguvukazi kuhusu suala la ajira.

Namna pekee ya kufanya hivyo ni kufikiria nje ya boksi ambalo tunafikiria kila siku. Ninaposema kufikiri nje ya boksi nina maana ya kuachana na mambo ambayo tumekuwa tukiyafanya kwa sababu ya mazoea tu.

Kitakwimu, uchumi wetu unakua vizuri. Kimsingi, kiwango cha asilimia saba ambacho uchumi wa Tanzania umekuwa ukipanda katika kipindi cha miaka ya karibuni ni kikubwa kulinganisha na nchi nyingi duniani.

Hata hivyo, ukuaji huo umeshindwa kumaliza tatizo la ajira lililopo hapa nchini. Hii maana yake ni kuwa, kama tutaendelea kushabikia takwimu hizi pasipo kuona tatizo lililopo, mwisho unaweza usiwe mzuri.

Kuna namna nyingi ya kufanya ili kupambana na tatizo hili la ajira. La kwanza, na hili linatokana na ripoti ya WB niliyoizungumzia awali, ni kuwezesha shughuli zisizo za kilimo ili ziweze kutoa mchango mkubwa kwenye soko la ajira.


Kwa mfano, Ripoti Mpya ya WB iliyopewa jina la “Tunahitaji Ajira Zenye Tija”, imeeleza kwamba kuna biashara ndogondogo milioni tano ambazo hazifahamiki na zina waajiriwa wasiozidi wawili.
Hizi ni biashara ambazo zinafanywa zaidi mijini. Watu wengi wanazijua kwa vile ndiyo ziko huko katika maeneo wanakoishi watu. Kama biashara hizi zikifahamika na kueleweka na kisha zikawekewa mazingira ya kukua, zinaweza kuwa chanzo kikubwa cha ajira.
Kama biashara hizi zikiwezeshwa, kuna uwezekano wa kupata ajira walau milioni moja kwa mwaka. Kuna wafanyabiashara wengine ni wakubwa lakini biashara zao hazihitaji mambo haya ya Maeneo Huru ya Biashara (SEZ).


Kuna watu kama waigizaji wa filamu, na nashukuru kwamba katika uzinduzi wa ripoti hiyo mpya ya WB, mwigizaji maarufu, Jacob Stephen JB, alihudhuria na kuzungumza.


Mwigizaji wa filamu hahitaji kwenda SEZ. Kama alivyo kwa mwanamuziki na baadhi ya sanaa nyingine. Lakini sote tunafahamu ni kwa kiasi gani, pamoja na kutokuwa katika utaratibu wa kisasa wa biashara, sekta ya burudani imeweza kusaidia vijana.
Nani alifahamu kwamba sekta ya filamu inaweza kuwa kubwa kama ilivyo sasa? Je, ni vijana wangapi ambao hawakuwa na matumaini ya maisha lakini leo wanaishi kwa sababu ya filamu au muziki? Je, wale waliofanikiwa, nao wameajiri watu wangapi ambao nao wanaishi kwa sababu hiyo?


Somo tulilolipata katika eneo la filamu linamaanisha kwamba zipo fursa nyingi za kusaidia nguvukazi iliyopo ambazo pengine hazijagundulika tu na kuwekwa hadharani.
Kama zitafahamika na kuwekewa mazingira mazuri, vijana wa kuzichangamkia watakuwepo tu na tutakuwa tumepiga hatua kubwa katika kukabiliana na tatizo hili kubwa la ajira.


Kama ajira katika sekta ya filamu halikuwa suala linalozungumzwa kabisa hadi mwaka 2005 na katika kipindi kifupi cha miaka kumi tu hali imefika ilipo sasa, Taifa litafaidika vipi endapo zitaibuka sekta nyingine chache na kuwa na faida kama ya kwenye filamu.
Jambo la msingi kwetu sote ni kufikiria nje ya boksi la kutazama ajira katika vyanzo vilevile na mtazamo ule wa wahasibu, wahandisi, wanasheria, waandishi wa habari, marubani na kadhalika.
Tufikiri nje ya boksi na majibu tutayapata.
No comments: