Thursday, July 24, 2014

RAI YA JENERALI

MUISLAMU "KHAMSA SWALAWAT"

Na Jenerali Ulimwengu,
 
NIMEKUWA nikijadili na kukemea, unafiki unaotutawala katika maisha yetu kama taifa. Tumefanya unafiki umekuwa ni sehemu muhimu ya utu wetu au labda niseme nakisi yetu katika utu. Unafiki umetuenea kiasi kwamba wengi wetu tunapoona ni bora kusema uongo hata pale ambapo ingekuwa faida kwetu kusema ukweli.

Hali hii haikuanza leo, ingawa sasa imekomaa. Nimewahi kusema mara nyingi kwamba tangu Awamu ya Kwanza ya utawala wa nchi hii, chini ya Julius Kambarage Nyerere, mbegu za unafiki zilikuwa zimepandwa, hasusan na watu walioona kwamba kukubali kila alichokisema Nyerere ilikuwa ni tiketi ya kuendelea kuwa katika uongozi, hata kama mhusika hakukubaliana hata kidogo na Nyerere.

Hali hiyo imeendelea, chini ya Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na hadi leo chini ya Jakaya Mrisho Kikwete. Imekuwa ndiyo hulka ya nchi yetu, ‘ethos’ ya taifa: Mpendeze aliye na mamlaka ili upate mradi wake, hata kama mambo yake siyo tu huyaungi mkono kifikra, bali yanakuchukiza hasa. Kwa jinsi hii tumekuwa waongo wakubwa kiasi kwamba anachokwambia mwanasiasa wa Tanzania, au hao wanaojiita wanasiasa, unaweza kukikadiria kuwa na ukweli kwa asilima 20 (kwa sababu katika mazungumzo atakuwa ametaja majina halisi ya watu, mahali na vitu) lakini asilimia 80 iliyobaki ujue ni mizungu.

Tukichunguza kioja kinachoitwa mchakato wa Katiba tunapata kielelezo cha nisemacho. Ni dhahiri, na ushahidi upo, kwamba chama-tawala hakikutaka tangu mwanzo, hakitaki sasa na wala hakitataka kamwe kuandika Katiba mpya. Kisa? Chama hicho na wakubwa wake wanaona Katiba iliyopo sasa inawafaa wao na maslahi yao. Si maslahi ya nchi, bali maslahi ya wakuu walio madarakani leo.

Kwa sababu uwezo wa kutazama na kuzitambua alama za nyakati, kusoma kilichoandikwa ukutani kwa herufi ghaibu, wala kuona mambo yaliyo mbali zaidi ya upeo wa macho, hawa wakuu wetu hawana haja, akili, ari wala stamina ya kuyashughulikia mambo hayo. Ni makubwa, yanasumbua na hayana tija kwao. Kwa mantiki yao, wanaondoka kesho kutwa, hivyo kuna sababu gani ya kujiumiza bure?

Wakuu hao walitamka kwamba hatuna haja ya Katiba mpya kwani iliyopo inatosheleza mahitaji. Kisha mkuu wao alipotamka kwamba atateua tume ya kusaka Katika mpya, wakakaa kimya, na baadhi yao wakawa ndio watekelezaji wa utashi wa mkubwa wao. Sasa najiuliza ukitaka kufunga nguruwe, ukanunua viguruwe vidogo na kuvipeleka shambani, ukivijengea zizi la kisasa, ukavinunulia chakula kilichopasishwa na dawa zipasazo, lakini mwishowe ukakabidhi shamba hilo kwa meneja Muislamu wa swala tano, utapata nini? Chukua mfano huo, kisha uangalie mchakato wetu wa vichekesho vya kuliza wazalendo.

Muislamu ‘khamsa swalawat’ hawezi kufuga nguruwe, hata angekufa njaa. Ama atavitelekeza viguruwe vyako viliwe na mbweha, ama ataghairi kuvilisha, ama atavipa sumu vifilie mbali. Kwa vyovyote vile, hawezi kuishi katika shamba moja na wanyama ambao kwake ni najisi. Hivyo ndivyo tulivyosukumwa kufanya na matokeo yake tunayaona. Ipo siku watu watauliza mantiki ya hili zoezi ilikuwa nini hasa?

Aidha, kwa muda mrefu, miaka na miaka katika maandiko yangu nimekuwa nikisema kwamba haiwezekani kupambana na ufisadi kwa kuwakamata watu wadogo na kuwapeleka mahakamani wakati wewe mwenyewe unayetoa maelekezo ya kuwakamata hao unaowafanya wakamatwe una uhusiano wa karibu na wahalifu wengine ambao, kwa sababu ya uhusiano uliopo kati yako na wao, hawakamatwi na wala hawabughudhiwi.

Hawa hawakamatwi na hakuna hatua zozote zinazochukuliwa dhidi yao kwa sababu wewe mkuu wa shughuli ya kuwakamata au kuwashughulikia unawalinda. Kwa mantiki hii asasi yoyote ambayo inaendelea kuwa na wezi, wala rushwa na mafisadi na hifanyi lolote kuhusu watu hao, ni asasi ya kifisadi.

Ziko nyingi hizi, na baadhi ya hizo ni asasi zinazohusiana na uongozi na utawala wa nchi moja kwa moja. Imekuwa ni kawaida zama hizi kwa watu ambao wanayo mambo mengi ya kuficha, na ambao huko walikotoka wametengeneza fedha za kutosha, halali na haramu, kutaka kujipenyeza katika nafasi za ‘uongozi’ kwa sababu mbili kuu.

Ya kwanza ni kukata bima dhidi ya kugundulika na kufuatiliwa. Hivyo ndivyo watu walivyoingia katika nafasi za juu za ‘uongozi’ wa chama-tawala hata kama hawajui iwapo TANU ilikuwa timu ya soka au klabu ya kucheza gombe-sugu. Hawajui nadharia moja, moja tu, kuhusu uhusiano wa kijamii na mifumo ya kiuchumi.

Hawa ndio wachangiaji wakubwa katika mifumo ya chama. Baadhi yao ni majangili wanaojulikana, lakini wao ndio mihimili mikuu ya chama ambacho kiliacha zamani sana kuwa na mihimili ya kinadharia na kiitikadi na kikajikita zaidi katika mihimili ya kifisadi.

Sababu ya pili ya watu hawa kukimbilia nafasi za ‘uongozi’ ni kuongezea juu ya kile walichonacho tayari. Mwizi hawezi kutosheka, na hakutakuwa na siku atakapojihisi kuridhika na mali alizochuma kwa njia haramu. Atataka kuongezea siku zote.

Chama-tawala ndicho kinachoendesha Serikali, na Serikali ndicho kituo kikuu cha rushwa na ufisadi katika nchi yoyote ya dunia ya tatu, na hata nyingine. Hii ni kwa sababu Serikali ndiyo inayoendesha miradi yote kabambe katika nchi na ndiyo inayotoa kandarasi na mipangilio mingine ambayo inakimbiliwa na wawekezaji na wahuni wa kila aina. Pia Serikali ndiyo inayotoa misamaha na afadhali kadha wa kadha kwa wale inaopenda kuwapa faida hizo.

Ili kuthibitisha kwamba Serikali inaweza kufanya mambo ya hovyo yanayoumiza nchi, sote tunajua kwamba Serikali yetu iliwahi kutoa misamaha ya kodi kwa majumba ya kamari! Unataka kujua nini zaidi kuhusu kinachowezekana na kisichowezekana serikalini.


Itaendelea...


RAIA MWEMA

No comments: