Wednesday, May 7, 2014

BUNGE LA BAJETI NA POSHO

Bunge la bajeti limeanza vikao vyake leo mjini Dodoma huku wabunge wakitarajiwa kuanza kulipwa viwango vipya vya posho vya Tsh 300,000/= kwa siku badala ya viwango vya zamani vya Tsh 200,000/= kwa siku. Nyongeza hiyo ya posho ya 50% kwa kila mbunge italigharimu Taifa kiasi cha Tsh 18.5/= Bilioni kwa siku zote zilizotengwa kwa ajili ya bunge hilo la bajeti. 

 Kabla ya kufikia uamuzi wa kupandisha viwango hivyo kwa Sh100,000 zaidi, wabunge walikuwa wakilipwa Sh200,000 kwa siku (yaani Sh70,000 kama posho ya kikao (sitting allowance), Sh80,000 posho ya kujikimu (perdiem) na Sh50,000 ya gharama za usafiri).

Nyongeza hiyo kwa kila mbunge kwa siku, sawa na asilimia 50, italigharimu Bunge la Jamhuri ya Muungano kiasi cha Sh18.5 bilioni kwa siku 52 zilizotengwa kwa ajili ya Bunge la bajeti linalotarajiwa kuhitimishwa Juni 27.

 Mtazamo.

Hili sio tena bunge limegeuka kuwa "pipa la wajinga" waliomo na wasiokuwamo wote waambukizwa kasumba hii ya kudai posho posho posho posho huku mtanzania wa kawaida akilia na hali ya umaskini, ujinga na maradhi.

 Bajeti ya serikali inayotangazwa kila mwaka ni sawa na mchezo wa kuigiza. Tumekuwa tukishuhudia kila mwaka serikali ikitangaza bajeti ambayo haitekelezeki. Kwa mfano, ni 43% tu ya bajeti ya 2014/2015 iliyotengwa kwa ajili ya TAMISEMI ambayo ilitekelezwa. Na hii ndiyo hasa wizara inayowagusa wananchi. Sasa ikiwa bajeti ya wananchi haitekelezwi maendeleo yatapatikanaje?

Fedha zinazotengwa kwa ajili ya bajeti huwanufaisha zaidi watawala kuliko wananchi. Hazijawahi kukosekana fedha za mishahara ya wabunge na mawaziri au fedha za kununulia mashangingi, kukimbiza mwenge, kufisidi, kutanulia, kufanyia sherehe za kipuuzi, kufanyia maadhimisho uchwara na upuuzi mwingine kama huo. Fedha kwa ajili ya upuuzi zipo tele sana, za maendeleo hakuna!

Bajeti inayotegemea wafadhili na mapato duni ya kodi ni bajeti mfu na haiwezi kuleta maendeleo yoyote. Ni afadhali kutangaza bajeti ndogo inayotogemea vyanzo vya uhakika vya fedha kuliko kujifariji kukadiria bajeti kubwa inayotegemea fedha za kufikirika kutoka kwa wafadhili.

No comments: