Thursday, April 10, 2014

WIZARA YA NISHATI NA MADINI YATOA MILIONI 48.42 KUFADHILI MASOMO YA CHUO WANAFUNZI WA MTWARA NA LINDI

WIZARA ya Nishati na Madini imetoa sh milioni 48.42 kwa ajili ya kuwalipia ada wanafunzi 40 kutoka mikoa ya Mtwara na Lindi, wanasoma kwenye Chuo Kikuu cha Stella Maris.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana mjini Mtwara, Mkuu wa Kitengo cha Falsafa na Maadili ya Chuo Kikuu cha Stella Maris Mtwara, Mchungaji Dk. Aidan Msafiri alisema kilichofanywa na wizara hiyo ni majibu ya ombi la kuwahamasisha wakazi wa mikoa hiyo wasiende mbali kutafuta elimu ya chuo.
Alisema alipokuwa akiwasilisha kwenye kongamano la viongozi wa dini mbalimbali lililofanyika mjini hapa hivi karibuni ambapo Katibu Mkuu wa wizara hiyo Eliakim Maswi alishiriki, aliiomba wizara kuwasomesha wanafunzi 20 kutoka Lindi na wengine Mtwara.
“Wakati nawasilisha mada yangu katika kongamano lile, nilitoa changamoto na kuiomba wizara iwasomeshe wanafunzi 20 kutoka Lindi na Mtwara ili kuwahamasisha wengine wasiende nje ya mkoa huu kutafuta vyuo. Hapa walimu wazuri.
“Baada ya ombi hilo katibu mkuu wa wizara alijibu hoja yangu kwa kukubali ombi langu na tayari wanafunzi hao wameanza masomo, kati yao wanafunzi 36 wanasoma ngazi ya cheti na wanne wanasoma diploma,” alisema.
Alisema baada ya hilo walitangaza na kwa bahati nzuri mwamko wa wanafunzi na wananchi wa Mtwara na Lindi ulikuwa mara mbili yake kwani aliomba wasomeshwe wanafunzi 20, lakini maombi yalipelekwa 40.

“Ilikuwa changamoto kwa wizara baada ya kupeleka majina 40 badala ya 20 niliyoomba mwanzo, lakini halikuwa jambo baya ila nashukuru wizara hii ilikubali kuwasomesha wanafunzi wote 40. Naomba wizara nyingine ziige mfano huu,” alisema.

CHANZO: TANZANIA DAIMA

No comments: