Thursday, April 10, 2014

KATIBA BORA TANZANIANa Zitto Kabwe,

( nimepitia vichwa vya habari vya magazeti Leo na kukuta habari ya 'wasomi wapinga Serikali 3'. Kwamba wameandika kitabu kwa ajili hiyo. Nilifanya mapitio ya kitabu hicho mwishoni mwa Mwezi Machi, 2014)
Hiki ni kitabu kilichotokana na mada mbalimbali ambazo zimekusanywa pamoja kuhusu Katiba ya Tanzania na mchakato wa kuandika katibampya ya Tanzania. Kitabu hiki kimehaririwa na Wasomi na Wanataaluma Teddy Malyamkono, Mason H na Rutinwa B na kuchapishwa na taasisi ya ESAURP mwaka 2014. Leo nimeona tuangalie kitabu hiki kwa sababu za dhahiri kabisa kuwa hivi sasa Tanzania ipo katika mchakato wa kuandika Katibana Bunge la Katiba tayari limeanza kazi hiyo mjini Dodoma.


Kitabu hiki kina jumla ya Sura Kumi na mbili ikiwemo Hitimisho. Sura zimejadili masuala mbalimbali kuhusu Katiba ya Tanzania na muundo wa Muungano ambao wasomi wanaona unafaa kwa nchi kama Tanzania. Sura ya Kwanza inazungumzia aina ya Katiba inayofaa Tanzania, sura ya pili inatoa mifano ya Dola mbalimbali duniani ambazo zimeungana au kuunganishwa. Sura ya tatu na ya nne zinazungumzia kuhusu uwakilishi wa kisiasa kupitia vyama vya siasa kati ya Taifa na Serikali mbili na Uraia na haki za uraia ndani ya rasimu ya Katiba mpya. Sura ya Tano inahusu mahusiano ya kiuchumi na kikodi kati ya Tanzania bara na Zanzibar na Sura ya Sita inahusu Katiba ya Afrika ya kusini. Sura ya Saba inahusu madhara ya kiuchumi ya muundo wa Serikali mbili au Serikali Tatu na Sura ya Nane inahusu hatua ambazo Zanzibar inaweza kuchukua kujinusuru kiuchumi katika mfumo unaopendekezwa na Rasimu ya Katiba. Sura ya Tisa, Kumi na Kumi na Moja zinahusu masuala ya Utamaduni wa Zanzibar, Madhara ya muundo wa Serikali unaopendekezwa na Namna ya kuepuka gharama za Katiba mpya: Somo kutoka Kenya. Sura ya Kumi na Mbili ni Hitimisho la Kitabu.


Hiki ni kitabu kipya lakini masuala yake sio mapya sana, ni masuala ambayo yamekuwa yakizungumzwa kwa miongo mingi sana kuhusu hatma ya nchi yetu na Katiba itakayotuvusha. Mada zimeandikwa na Wasomi waliobobea katika maeneo yao na wengine wamebahatika kufanya kazi pande zote mbili za Muungano. Kwa mfano Profesa H Mushi ambaye ameandika sura ya Tano alikuwa Mshauri wa masuala ya Uchumi wa Rais Amani Karume wa Zanzibar kwa miaka takribani minane. Profesa Maliyamkono yeye amekuwa akiandika kuhusu masuala ya Muungano kwa muda mrefu na hivyo ana mawazo na fikra zilizo wazi kabisa kuhusu muungano. Umuhimu wa kitabu hiki unakuja kwa sababu mawazo mengi sasa yamewekwa pamoja na kufanyiwa utafiti wa kisomi. Sura zinazogusia masuala ya uchumi zimenivutia zaidi kwani zimejadili masuala hayo kwa takwimu za muda mrefu. 


Profesa Osoro, Nehemia amechambua suala la gharama za kuendesha Serikali, iwe moja, mbili au tatu. Kwa mara ya kwanza sasa tunaweza kupata uhalisia wa gharama za Muundo wowote katika makala moja ya Kitabu hiki. Licha ya kwamba unaweza usikubaliane na mawazo yaliyomo ndani ya makala za kitabu hiki, lakini ni kitabu ambacho unaweza kusoma na kupata faida kubwa na kupanua mawazo kuhusu Muungano wetu na hatma ya Tanzania.


Katika Sura ya Kwanza tu Kitabu kimeanza na nukuu kutoka kwa msomi aliyebobea katika masuala ya Muungano Prof. Issa Gulamhussein Shivji “Katiba zinaundwa kuhudumia watu; watu hawaumbwi kuhudumia Katiba”. Mwandishi wa Sura hii Prof Maliyamkono ana mashaka makubwa sana na muundo unaopendekezwa na Rasimu ya Katiba kwa kuandika “…..Muundo huu unaopendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba sio wa kawaida kwa sababu sio tu kuna maeneo mawili ya utawala - Zanzibar na Bara - ndani ya Shirikisho lakini pia kuna tofauti kubwa sana kijiografia kati ya pande hizo. Serikali ya Juu itazidiwa nguvu na Bara na kutakuwa na migogoro isiyokwisha kati ya Serikali ya Muungano na Serikali ya Zanzibar” (uk.4)(tafsiri yangu binafsi). 


Hata hivyo Sura inapendekeza kuwa muundo wa Serikali mbili uliyofanyiwa maboresho makubwa ungefaa kwa hali ya Tanzania kwa kuiga kinachoitwa “One nation - two systems” kama ilivyo huko HongKong na Macau Nchini China. “Ikitokea Serikali mbili zikashindwa kuelewana kuhusu jambo fulani, Serikali ya Muungano haitakuwa na Mamlaka yeyote ya kuingilia na kutoa maamuzi dhidi ya Serikali mojawapo na hilo litapelekea muungano kuvunjika” (uk. 11). 


Hata hivyo kuna makosa madogo katika sura hii ambapo katika masuala ya Muungano ndani ya Rasimu ushuru wa forodha sio sehemu ya mambo ya muungano (uk.9) na badala yake ni ushuru wa bidhaa. Pia mwandishi anaiita Serikali ya Zanzibar ‘discrete government’ (uk.9) kitu ambacho kinaweza kumfanya Mzanzibari yeyote kukasirika na kuacha kabisa kusoma sura hii akifika hapo tu. Hata hivyo sura inashauri kuwa lazima kuwe na nia njema kutoka kila upande katika kukubaliana katiba sahihi. Ameacha swali kwa waandishi wa rasimu ya sasa “Rasimu ina ulinzi gani wa kutosha kuhusu utatuzi wa migogoro ndani ya Serikali tatu?”


Ndani ya kitabu hiki tutaona mifano mingi sana kuhusu miungano mbalimbali duniani lakini ni maeneo machache sana au hakuna kabisa ambayo yana muungano ambayo nchi mbili zenye tofauti kubwa ya eneo la kijiografia na idadi ya watu zimeungana. Mifano ya Muungano wa Marekani (USA) imetolewa lakini wenyewe ni muungano wa Nchi hamsini zenye ukubwa tofauti tofauti na idadi ya watu tofauti tofauti. Vile vile mfano mwingine ni ule wa Uingereza ambapo Nchi za Scotland, Wales, England na Northern Ireland ziliungana na kuunda United Kingdom. 


Kuna mifano pia ya The Faroe Island na DenMark, Puerto Rico na USA, Hongkong, Macau na China, Jersey na Uingereza, Aland na Finland na pia Acey na Indonesia. Vile vile mifano ya kihistoria ya Yugoslavia na Nchi zilizounda Yugoslavia, USSR na nchi zilizounda USSR na Canada na Quebec. Hoja moja kubwa ambayo unaipata hapa ni kwamba maeneo kadhaa ambapo Nchi kubwa imeungana na nchi ndogo kwa eneo na hata idadi ya watu, nchi kubwa inakua haina Serikali na nchi ndogo inakuwa na Serikali. Mfano ni USSR ambapo Russia haikuwa na Serikali yake na masuala yake yalikuwa chini ya Serikali ya Muungano wa Jamhuri za Soviet. Siku ambayo Russia iliunda Serikali yake, muungano ule ulikufa siku ya pili. Uingereza pia, wakati Scotland una Serikali yake na Bunge lake, vile vile Wales na Northern Island, England inahudumiwa na Serikali ya Uingereza (Serikali ya Muungano). 

Yugoslavia pia nchi kubwa ya Serbia haikuwa na Serikali yake na ilihudumiwa na Serikali ya Muungano na Serikali ya Serbia ilianzishwa baada ya Jamhuri nyingine kuanza kujitenga kufuatia muungano ule kuwa na nyufa nyingi sana. Hata hivyo ni vema kusisitiza kuwa tunapoangalia mifano ya nchi nyingine ni vema kutambua kuwa kuna tofauti kubwa sana kati ya historia ya muungano wa nchi hizo na Tanzania. Zanzibar ilikuwa Dola huru inayojitegemea wakati inaungana na Tanagnyika kuunda Tanzania ilhali hiyo mifano mingine ni mifano ya nchi zilizopigana vita na kukombolewa na hivyo kutawaliwa. Zanzibar haijawahi kuwa koloni la Tanganyika na hivyo ni lazima kutambua tofauti hiyo kabla ya kuona ni muungano upi wa kuiga.


Kitabu hiki pia kimeonyesha misimamo ya vyama vya siasa kuhusu muundo wa muungano ingawa uchambuzi wake hauonyeshi hasa sababu za vyama kuwa na misimamo hiyo zaidi tu ya kuonyesha kuwa vina sera tofauti. Hata hivyo ninashauri sana kuwa sura mbili zinazohusu masuala ya kiuchumi zisomwe kwa kina sana. 

Prof Osoro na Prof Mushi wamechambua takwimu mbalimbali na namna gani kila muundo wa Muungano unaweza kugharimu Taifa. Inawezekana uchambuzi wao una mapungufu kadhaa (ikiwemo kuwepo kwa takwimu za hivi karibuni kuhusu matumizi ya Serikali kwenye mambo ya muungano na pia mapato ya Serikali, kuhusu mchango wa awali wa Zanzibar katika kuanzisha Benki Kuu na hata ni muungano gani ambao hauna Monetary Union au Common External Tariff).

HABARI INATOKANA NA MITANDAO YA KIJAMII-FACEBOOK

No comments: