Sunday, March 30, 2014

USIFE MOYO WARIOBA, UVCCM NI KIOTA CHA FIKRA FINYU NA MATUSI

Na Seif Abalhassan,
UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) tangu zama za TANU umechukuliwa kama kiota cha kulea na kutayarisha wanachama na viongozi wa kisiasa na hata wa kiserikali kwa lengo la kujenga siha njema ya kujitawala.


Ndio maana Mmoja wa waasisi wa taifa hili, Mwalimu Julius Nyerere alipata kusema lazima vijana wajengwe kuweza kujenga hoja, Wafundishwe na kujizoeza kujenga hoja, kutathmini vitu kwa kutumia tafakuri kwa sababu ni kwa njia hiyo tu ndiyo wanaweza kutumia hazina waliojaliwa na Mungu; ubongo, kukabiliana na changamoto za maisha.

Pengine ni katika kutambua hili, mwaka 1994, Jaji Joseph Warioba, wakati huo akiwa mbunge wa kawaida alikumbusha vijana wa CCM wajibu wa kujifunza kujenga hoja na si kujiingiza katika malumbano ya kisiasa yanaoendeshwa kwa hisia na jazba.

Warioba alisema hayo akijibu tuhuma za aliyekuwa Katibu Mkuu wa UVCCM ambaye alikuwa Mbunge pia, Sukwa Said Sukwa. Sukwa akisukumwa na hisia zisizokuwa na hoja, alipandisha mori na kumsakama Warioba bungeni kwa matusi na maneno yasiyo na staha kwa kuwa tu Hoja ya Warioba haikumpendeza yeye na Wakuu wake.

Sukwa alimwambia Warioba kuwa amesukumwa na tamaa ya madaraka ndiyo maana aliwasilisha hoja binafsi ya kulitaka Bunge kuishurutisha serikali izingatie maoni ya wananchi kabla ya kufanya mabadiliko ya katiba na hasa, mambo yanayohusu Muungano.

Katika wakati husika Serikali kupitia Bunge lenye Wabunge wenye 'nidhamu ya Chama' ilikuwa na Mpango wa Kufanya Mabadiliko ya Katiba yenye kumuondolea Rais wa Zanzibar nafasi ya Umakamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mabadiliko ambayo si tu yalipingwa kwa kiasi Kikubwa na aliyekuwa Rais wa Zanzibar na Makamo wa Pili wa Rais wa wakati huo, Dkt Salmin Amour Juma 'Komandoo' bali pia yalikuwa yanakiuka 'Mkataba wa Muungano' ambayo ndiyo Sheria Mama ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Lengo la Mabadiliko hayo lilikuwa ni kuleta Utaratibu wa Mgombea Mwenza ambaye ndiye anakuwa Makamu wa Rais unaotumika sasa. Aliyekuwa Mbunge wa Bunge hilo, Twaha Khalfan Ulimwengu 'Jenerali Ulimwengu' alisema mabadiliko hayo yaliletwa kwa sababu ya 'khofu tu' kuwa Maalim Seif wa CUF angeweza kushinda Uchaguzi wa Kwanza wa Vyama Vingi nchini wa mwaka 1995 kwa Zanzibar, na hivyo kuweza kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Rai ya Jaji Warioba katika hoja yake hiyo aliyoiwasilisha Bungeni, ilikuwa ni kutaka Jambo hilo la kufanya mabadiliko hayo makubwa ya Katiba na Mfumo wa Kuendesha mambo ya Muungano liendewe kwa busara, kwa kuwa ni kubwa mno na lina athari kubwa kwa hatma ya Muungano wetu, hasa baada ya matukio ya G55. Kwa hiyo, akapendekeza kwenye hoja yake kuwa Wananchi washirikishwe kwanza kwenye Mabadiliko hayo ya Katiba.

Sukwa hakujikita kwenye kujibu hoja hiyo iliyowekwa mezani, bali yeye alikwenda mbali zaidi kwa kusema kuwa Jaji Joseph Sinde Warioba amesukumwa na ubinafsi zaidi ndiyo maana wakati akiwa Waziri Mkuu hakufanya hayo aliyokuwa anayapendekeza wakati huo akiwa Mbunge tu, Kati ya Mwaka 1985 na 1990 Warioba alikuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais AlHaj Ali Hassan Mwinyi.

Katibu huyo wa UVCMM, Sukwa hakuishia hapo, Alitaka Waziri Mkuu wa wakati huo, Cleopa David Msuya, akiondoka kwenye kiti hicho asiwe kama Warioba. Kwa kifupi, kauli za Sukwa zilivuka mpaka wa kutambua mantiki ya hoja. Alikuwa ameishiwa hoja na kupumzisha ubongo, Kwa kuwa hakujikita kwenye kuchambua na hata kupinga hoja ya Warioba bali aliamua kumshambulia Warioba mwenyewe.

Jaji Warioba alikuwa amewasilisha hoja hiyo kwa nia njema na mapenzi yake kwa Muungano na nchi yake, na kwa hakika baadaye aliiondoa baada ya serikali kumuomba kwa sababu tayari Serikali ilidai kuwa ilikuwa katika mchakato wa kutekeleza hayo aliyokuwa anapendekeza kwenye hoja yake binafsi. Japo baadaye Serikali haikutekeleza ahadi yake hiyo kwa kuwa ilifanya mabadiliko hayo makubwa ya Katiba bila kuwashirikisha wananchi.

Akijibu michango mbalimbali ya wabunge waliokuwa wamechangia hoja yake hiyo, kabla ya kuiondoa, Warioba alisema: "kuhusu Sukwa sina la kusema kwa sababu alichokizungumzia ni hisia zake, Siwezi kujibu hisia, Ila kama aliyoyasema yanawakilisha nguvu ya umoja wa vijana (UVCCM), basi kuna tatizo kubwa katika umoja huo.

Warioba alikumbusha kwamba ni vema vijana wakajifunza kujibu hoja. Kujenga hoja, kwa sababu huko ndiko viongozi wa taifa hili wanaandaliwa.

Nimekumbuka kauli hiyo ya Warioba baada ya kuona katika wakati huu kauli zinazofanana na kauli za Sukwa mwaka 1994 zikitolewa na Vijana mbalimbali walio Viongozi na Wanachama wa UVCCM, mara tu baada ya Jaji Warioba kutoa kwa Wananchi Rasimu ya Katiba iliyotokana na maoni ya Wananchi yaliyokusanywa na kuratibiwa na Tume aliyokuwa anaiongoza, huku mashambulizi yakionekana kuzidi zaidi mara tu baada ya Hotuba ya Rais Jakaya Kikwete wakati wa Uzinduzi rasmi wa Bunge la Katiba.

Kwa maoni yangu naweza kuwaelewa vijana wenzangu hawa wa UVCCM kuwa wanataka kutetea chama chao dhidi ya muundo wa Serikali 3 uliopendekezwa na Tume kuhusu Muungano kuhusu, ambao ni kinyume na sera yao ya muundo wa Serikali 2. Naweza pia kutambua kuwa wana damu inayochemka, ya ujana, na wanataka kuendesha mapambano.

Lakini nashindwa kuwaelewa kuwa sasa wanataka kuendesha mapambano ya hoja au ya matusi? Sitaki kuamini kuwa ndani ya UVCCM kuna nafasi ya matusi, si kwa mwanachama wa kawaida bali hata kwa kiongozi.

Ila kwa dhahiri inaonekana kuwaTanuri la kupika viongozi bora wa CCM, yaani UVCCM, limepandikizwa watu ovyo, na kwa hivyo tunaishia kupata siasa ovyo na viongozi ovyo. Vijana wasioweza kujibu hoja, wanaoporomosha matusi, ni watu dhaifu wasioweza kuhimili mikikimikiki ya siasa shindani, achilia mbali kuweza kubuni mikakati ya kukwamua taifa lao kutoka lindi la umasikini. Hawa ni ndio CCM inatuandalia waje kuwa viongozi, mawaziri wa kesho na Mungu aepushe mbali, marais wa kesho. Kweli tumo katika mkwamo mkali.

Lipo fundisho moja kubwa: yale aliyoyazungumza Warioba miaka 20 nyuma, hayajafanyiwa kazi. UVCCM haijafanikiwa kujenga viongozi na wanachama wake katika uwezo wa kujenga hoja. Wakikasirishwa na maoni wasiyoyapenda wanaporomosha matusi badala ya hoja za kubomoa wapinzani wao.

Mwaka 1994 Sukwa alithibitisha kukosa sifa hizo. Alijikita katika hisia na matusi zaidi, mwaka 2014, miaka 20 baadaye, Vijana wa UVCCM bado wanajikita katika matusi na hisia kuliko kupinga kwa hoja yale mapendekezo yasiyowapendeza yaliyomo katika Rasimu iliyoletwa na Warioba na Tume yake.

No comments: