Tuesday, February 4, 2014

YAGUINE KOITA NA FODE TOUNKARA: MASHUJAA WA TAFAKURI JUU YA NAMNA MISAADA YA KIGENI INAVYOLEA UNYANG'AU AFRIKANa Seif Abalhassan, (Kupitia  Ukurasa wake wa Facebook)

Jioni ya Agosti Mosi, 1999 vijana wawili, Yaguine Koita na Fodé Tounkara walifanikiwa kuingia katika Uwanja wa Ndege wa Conakry, Mji Mkuu wa Guinea, Nchi iliyo katika Pwani ya Afrika Magharibi, na kuamua kujivingirisha katika sehemu ya mizigo ya ndege ya Shirika la Ndege la Sabena iliyokuwa inafanya safari ya kwenda Brussels, Ubelgiji.


Vijana wawili hao walijua kuwa nafasi yao ya kufika salama mpaka mwisho wa safari yao ni ndogo, mwaka mmoja uliopita kijana mwengine kutoka Senegali alikuwa amejaribu kufanya mchezo kama huo wa kudandia ndege iliyokuwa inaelekea Paris, Ufaransa, akifika salama lakini akiwa yu taabani, mahututi hajiwezi, kwa dhahiri joto la injini iliyokuwa karibu na sehemu aliyojiegesha ndilo likimuokoa.

Vijana hawa wawili wa Conakry hawakuwa na bahati kama yule mwenzao wa Senegali, kwa masikitiko makubwa miili yao ilikutwa bila uhai mara baada ya ndege waliyozamia kutua Brussels. Mkono wa mmoja wa Vijana wawili hao ukiwa umeng'ang'ania karatasi iliyokunjamana na kuandikwa kwa mkono.

Ujumbe ndani ya Karatasi hiyo ulikuwa na maneno yafuatayo, "Kwenu Watukufu, Watu na Maofisa wa Ulaya, karatasi hii inaelezea kuhusu 'kukiukwa kwa haki za watoto', zaidi katika Shule za Umma za Afrika. Ni pale tu katika Shule binafsi ndipo Vijana wanaweza kufurahia Ufundishwaji na Usomaji mzuri, lakini fursa hiyo inahitaji pesa nyingi ambazo wazazi wetu hawana kwa sababu ni Mafukara. Kwa hiyo basi, sisi watoto na vijana wa Afrika tunawaomba mtengeneze taasisi imara ya kusaidia maendeleo ya Afrika, kama tunayahatarisha maisha yetu na kuyaweka hatiani kwa safari hii basi ni kwa sababu tunauhitaji msaada wenu."
Ujumbe huu wa Vijana hao ulihuzunisha kama lilivyohuzunisha tukio la kupoteza kwao maisha. Balozi wa Guinea katika Umoja wa Ulaya alionekana kwenye Televisheni moja ya Ufaransa siku moja baada ya vifo vya watoto hao akionyesha huzuni kwa vifo vya kusikitisha vya Vijana hao lakini akionyesha kuwa hakukuwa na umuhimu wa vijana wawili wale kuitangazia dunia kuhusu hali ya nchi yao. "Ni kama vijana wawili hawa walikuwa wanaiambia Dunia kuwa 'tupeni msaada zaidi' ili hali hii isijitokeze tena", alinukuliwa akisema Balozi huyo.

Siku mbili baada ya kadhia ya vifo vya watoto wale, Meya wa Jiji la Conakry 'aliisafisha' na kuiondolea lawama Serikali ya Nchi yake katika kuwajibika juu ya suala hilo, zaidi akilitupia lawama shirika la ndege la Sabena na mamlaka Za Uwanja wa Ndege. "Jambo hili lisingetokea kama Sabena na Mamlaka za Uwanja wa Ndege zingeweka Ulinzi wa kutosha kuzuia wazamiaji", Alisema Meya huyo.

Watu wa Guinea waliuelewa ujumbe wa Vijana wale vema sana, Siku miili ya vijana wale ilipokuwa inarejeshwa nchini humo kundi kubwa la raia wa nchi hiyo lilijitokeza uwanja wa ndege kuipokea miili hiyo huku wakiombeleza kwa hasira. Mwananchi mmoja alimuendea Mwandishi wa Kifaransa huku analia kwa kwikwi akimwambia "Vijana hawa wameongea kwa niaba ya sote sisi." Huku akionyesha namna alivyochukizwa na Serikali ya nchi hiyo.

Katika hali ya kawaida, janga la vifo vya vijana wale halikupaswa kutokea kabisa. Katika muktadha huo Meya wa Conakry alikuwa sahihi kabisa, lakini ni Elimu bora mashuleni ndiyo ambayo ingeliweza kuzuia kutokea kwa janga hilo na si ulinzi imara wa kuzuia wazamiaji.

kadhia ya vifo hivi ilikuwa ni tone tu ukilinganisha na vifo vya Mamilioni wa Waafrika wanaokufa kila siku kwa Ukimwi na athari za vita. Lakini kwa watu waliokuwa na matumaini machache ya kusonga mbele kwa Afrika, vifo vya watoto hawa ilikuwa ni kama kukitwa mkuki moyoni. Ni vifo vilivyomkasirisha kila mmoja ambaye alijua kiwango cha pesa na nguvu za misaada ya kigeni iliyotumika kuhakikisha msingi wa elimu wa vijana wa Afrika unasimikwa, ni kadhia ambayo iliamsha tafakuri mpya juu ya 'nini hasa lilikuwa tatizo la Afrika?, kwanini pamoja na misaada yote kwa Afrika bado nchi za Afrika ni Masikini zaidi?

Nasoma Vitabu viwili wa wakati mmoja, 'The Touble with Africa: Why Foreign Aid Isn't Working' cha Robert Calderisi, Mtumishi wa miaka zaidi ya 30 wa Benki ya Dunia na Shirika la Fdha Duniani, IMF katika Nchi mbalimbali za Afrika, Kitabu husika kikiwa ni zawadi ya Zitto Z Kabwe kwa Tumaini Mbano na Kitabu chengine ni 'Dead Aid' cha Dambisa Moyo, Mtaalam Mweledi wa Uchumi Duniani Mzaliwa wa Zambia.

Kimoja kikijikita katika kuchambua kufeli kwa misaada ya Wazungu kwa Nchi za Afrika katika Mtazamo wa Mtumishi wa Benki ya Dunia na IMF na kingine kikijikita katika kuangaza suala hilo hilo lakini katika mtazamo wa Kiafrika, ni Vitabu vinavyonipa tafakuri nzito.

Kwa kiasi kikubwa vitabu vyote viwili vimeasisiwa katika kadhia hiyo ya Vijana wa Conakry Yaguine Koita na Fodé Tounkara, pichani. Tafakuri iliyojitokeza juu ya nini tatizo la Umasikini wa Afrika hata mara baada ya misaada ya zaidi ya Shilingi Trilioni Elfu Moja (1,000,000,000,000/-) kwa muda wa miaka 50 iliyopita ndiyo iliyozaa Vitabu viwili hivi.

Kwa dhahiri Vitabu vyote viwili vimeainisha Uongozi mbovu wa Kinyang'au kama moja ya sababu kuu ya Ufukara wa Afrika hata baada ya misaada yote hiyo, Huku Dambisa Moyo akiainisha namna Misaada hiyo inavyolea na kukomaza Unyang'au, Ufisadi, Rushwa na Wizi kwa Tawala za Kiafrika.
Majina kama 'Live 8', 'Make Poverty History', 'The Millenium Development Goals', 'Th Millenium Challenge Account' na 'Tha Africa Comission' ni sehemu ya Miradi mashuhuri ambayo ilifadhiliwa na Mataifa Tajiri kwa nchi Masikini za Afrika, lakini bado baada ya misaada hiyo Umasikini kwa Afrika umepanda kwa 66% kutoka 12% miaka 40 nyuma.

Nchi yetu inategemea zaidi ya 40% ya Bajeti yake kutokana na Misaada na Mikopo ya ndani na ya nje, huku Deni la Taifa likongezeka kwa kasi kutokana na mikopo ambaye haijawahi kuleta tija kwa wanyonge, ni dhahiri kuwa dhana ya Dambisa Moyo juu ya Misaada na Mikopo hii kwa nchi za Kiafrika kama yetu ikijithibitisha kwa namna rushwa ilivyotamalaki nchini, Ufisadi ulivyopamba moto kwa jamii ya tabaka Tawala, Unyang'au ulivyoshika kasi kwa wenye mamlaka na Umasikini ulivyowatopea Wanyonge, ikiwa ni nchi ambayo zaidi ya theluthi mbili ya wananchi wake wanaishi katika Ufukara.

Kwa dhahiri misaada na mikopo hii haijatuondolea Umasikini wananchi wanyonge wa Tanzania, zaidi ya kuwa ni kivutio cha Matumizi ya anasa, ufisadi, rushwa na unyang'au wa kila aina wa Viongozi wetu Manyang'au. Ni aina hii ya Mikopo ndiyo inayoleta mifumo ya Mishahara minono ya Wabunge, Posho za Makalio na hata 'Kiinua Makalio' cha zaidi ya Milioni 160.
Miaka zaidi ya 13 leo mara baada ya vifo vya Vijana hawa wa Conakry hali ya Afrika ya sasa inaonekana kuzidi kuwa mbaya zaidi.

Tafakuri ni Nzito.

No comments: