Friday, January 24, 2014

TANZANIA IKO HOI KIFEDHA C.A.G

 Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utoh amesema kuwa Serikali ya Tanzania iko hoi kifedha hivyo Bunge na Serikali lazima wajitathmini.


Hata hivyo, alisema kuwa wanayo matumaini makubwa kutokana na ushauri mwingi ambao umekuwa ukitolewa na ofisi yake kufanyiwa kazi ikiwemo mfumo wa utayarishaji wa bajeti za Serikali kuanzia mwaka 2013/14.
Utoh alitoa kauli hiyo jana katika ukumbi wa St Gasper nje kidogo ya Mji wa Dodoma kwenye mkutano wa pili wa baraza la wafanyakazi wa ukaguzi nchini.
Mkutano huo uliwajumuisha wajumbe wawakilishi kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara pamoja na wataalamu wengine na ulilenga kuendelea hadi leo ambapo CAG ndiye mwenyekiti wa mkutano huo.
CAG alisema katika maswali hayo kuna changamoto na matatizo makubwa ambayo yanatakiwa kutafutiwa ufumbuzi.
Alisema ni vyema Serikali ikaangalia kwa makini matumizi yake ikiwemo kusimamia kwa nguvu vyanzo vya mapato ili kuondoa changamoto hizo.
Kuhusu ofisi yake alisema bado inakabiliwa na changamoto kubwa ya watumishi jambo linalosababisha ufanisi katika utendaji kazi kuwa wa chini ya kiwango.
Alitaja kwa Serikali za Mitaa pekee wanahitajika wakaguzi 500 kwa nchi nzima, lakini waliopo hivi sasa ni wakaguzi 278 hivyo kuwa na upungufu wa watumishi 222.
Kwa upande wa wafanyakazi wa ofisi hiyo kwa ujumla, alisema wako wakaguzi 802 ukilinganisha na wakaguzi 531 waliokuwepo mwaka 2010, aidha kati yao 81 ni wakaguzi wa Umoja wa Mataifa ambao wanatakiwa kuongezwa wengine 69 ili kufikia 150.
Akizungumza katika Mkutano huo, Katibu Mkuu Utumishi, George Yambesi alisifu kuwa ofisi ya CAG imesaidia kwa kiasi kikubwa katika utendaji wa watumishi pamoja na kupunguza hati chafu na zenye shaka ndani ya Serikali Kuu na Serikali za Mitaa.
Hata hivyo, Katibu Mkuu alisema bado kuna changamoto kubwa kwa wakaguzi kwani baadhi yao wamekuwa si waaminifu katika shughuli zao ikiwemo kupokea rushwa.
“Serikali itaendelea kupokea ushauri mzuri wa CAG, lakini napenda mfahamu kuwa lazima mzingatie maadili yenu na wakaguzi wawe wasafi kwa tabia kuliko wanaowakagua kwani ziko tetesi kuwa baadhi yenu ni wala rushwa,” alisema Yambesi.
 
Alimtaka CAG kuendelea kutoa ushauri wa kitaalamu namna ambavyo Serikali itaboresha makusanyo yake na matumizi na kuahidi kuongeza idadi ya wakaguzi pale uchumi wa nchi utakaporuhusu.


MWANANCHI

No comments: