Friday, January 31, 2014

NCHI ZOTE HUINGIA KATIKA MACHAFUKO SABABU YA UJUHA HUU.Na Ayoub Ryoba,

KATIKA dunia tunayoishi leo, sisi Watanzania tunayo bahati moja kubwa.

Tumekuwa moja ya nchi chache Afrika ambazo hazijaingia katika migogoro ya kijinga na ya hatari iliyowalazimu wananchi kuchukua silaha na kuanza kuuana wenyewe kwa wenyewe kwa sababu za kisiasa.

Na kama nilivyoeleza katika makala zilizopita, pamoja na ubishani mwingi, misuguano, dalili za chuki (hasa baina ya wanasiasa) na kuzuka kwa propaganda za udini, bado Watanzania kwa ujumla wao ni watu wema na wanaoishi kwa kushirikiana kwa masuala mbalimbali bila kujali tofauti zao.

Hakuna bahati kubwa (ukiona vyaelea vimeundwa) tuliyokuwa nayo kama nchi na kama taifa kujikuta tunazo sababu zote za kutuwezesha kupiga hatua kubwa tena za haraka za kimaendeleo, japo tunasuasua. Na endapo ingelikuwa kwamba Mungu alikuwa akipokea kwanza rushwa ili kuziwekea nchi raslimali na watu wa aina fulani, basi Watanzania tungeonekana tulitoa rushwa kubwa sana!

Karibu nchi zote Afrika zenye rasilmali nyingi, hasa madini na mafuta, zimekumbwa na migogoro ya vita na mauaji ya kutisha. Na hata zingine ambazo hazikujaliwa raslimali lakini zikawa na uongozi mbovu, nazo pia ziliingia katika vita na machafuko ya kutisha ambayo hayatasahaulika kamwe. Sisi tuna bahati sana.

Hoja yangu leo ni kwamba uendeshaji wa nchi zetu unaweza kutazamwa kama uendeshaji wa kiwanda cha kuzalisha bidhaa. Kiwanda huwa na mtaji wa fedha, mitambo, majengo, rasilmali watu (ikiwamo mafunzo kwao), mipango ya manunuzi ya malighafi na mahitaji mengine, mipango ya uzalishaji, mipango ya usafirishaji, mipango ya masoko (ikiwamo mipango ya ushindani), mipango ya uendeshaji (ikiwamo ushughulikiaji wa taka na vitu vichakavu), udhibiti wa fedha au mahesabu kwa ujumla na mipango ya uwekezaji zaidi.

 Na katika dunia tunayoishi tunafahamu kwamba vipo viwanda ambavyo vimefanikiwa sana duniani na vipo pia ambavyo vimeshindwa kabisa na kufa.

Na kwetu sisi Tanzania tunayo mifano mingi ya viwanda vilivyokufa kutokana na sababu ambazo nitazieleza baadaye. Hili la baadhi ya viwanda kufanikiwa sana lakini vingine vikafa linayo maelezo yenye sababu mbalimbali za kisayansi kama ambavyo yapo maelezo ya kiuchumi kuhusu ni kwa nini nchi zingine huwa na mafanikio makubwa kiuchumi na kiviwango vya maisha ya watu wake na zingine kubakia hohe hahe hata kama zina rasilmali nyingi, watu wa kutosha, ardhi ya kutosha, na sifa zingine muhimu kwa maendeleo.

Haiwezekani jamii ikafanya suala la kuongoza kiwanda (kama ilivyo katika kuongoza nchi) likawa suala tu la kufurahisha nafsi za watu fulani halafu jamii ile ikategemea itapiga hatua za maendeleo kisayansi na hata kubaki salama kwa muda mrefu. Haiwezekani suala la kuongoza kiwanda likawa suala la kusaidia watoto wa ndugu ajira badala ya kuangalia mahitaji ya nafasi na sifa za anayepaswa kuajiriwa pale.

Kwa hiyo ili kiwanda kiendeshwe kwa ufanisi na kipate faida kubwa na zipatikane fedha za kuwekeza na kuzalisha zaidi ni lazima uanzishaji wake na uendeshaji wake ufuate misingi ya kisayansi.
Endapo katika kuanza kwa kiwanda waanzishaji hawajakubaliana misingi ya uanzishaji wa kiwanda na ni kwa nini wanataka kuanzisha kiwanda, wanakianzisha wapi, taratibu za uagizaji mitambo zinakuwaje, nk., basi kuna uwezekano mkubwa wakaanza vibaya. Matokeo yake mmoja wa waanzishaji anaweza kusafiri kwa gharama kwenda kuleta mitambo na badala ya kununua mipya akatafuta iliyotumika ikapakwa rangi na akaiingiza nchini. Anatengeneza vijisenti kidogo kwa ajili ya familia yake.

Fikiria uanzishwaji wa kiwanda wa namna hiyo mwisho wake utakuwaje.
Kinachofuata baada ya kufunga mitambo ile na likaanza suala la ajira basi kunakuwa na mwendelezo wa tatizo. Huyo anayeajiri atataka na yeye atengeneze vijisenti kutokana na wale anaowaajiri na matokeo yake ataacha watu wenye sifa muhimu kwa sababu tu ama si ndugu zake, au hawakuwa na fedha za kuhonga au hawaamini katika kuhonga.

Tatu, wale waajiriwa nao, atakayetakiwa kuwa anaagiza mafuta atatafuta namna ya kuyachakachua ili yalingane na fedha alizoidhinishiwa ili kuyanunua.
Matokeo yake, mbali na hasara ya fedha taslimu, kiwanda kitapata hasara ya mitambo kuharibika kutokana na mafuta machafu aliyonunua mfanyakazi. Yeye kaiba laki moja na kusababisha hasara ya mtambo wa shilingi bilioni sita!

Kitakachofuata mitambo isipofanya kazi kama ilivyotakiwa na uzalishaji utapungua. Uzalishaji ukipungua na mapato pia yanapungua. Mapato yakipungua na mishahara pia inachelewa na kusuasua. Matokeo yake tena, wafanyakazi wale walioajiriwa kwa wingi tena bila sifa wanaaza kutafuta chochote cha kuiba na kuuza ili tu wapate kujikimu. 

Matokeo yake kiwanda kinakufa, kinafungwa na wafanyakazi wanaachishwa kazi na familia zao zinaanza kuteseka kwa sababu wamekuwa maskini zaidi. Na palipo na maskini wa hivyo hakuna amani hata siku moja. Hiyo ni sheria ya asili.


Lakini hebu tuangalie kiwanda kile kile kiamue kufanya mambo tofauti.
Kwanza inakaa bodi na kuhakikisha kwamba melekezo ya wataalamu yamefuatwa kuhusu aina ya mitambo inayoagizwa na kwamba taratibu za uagizaji zimefuatwa. Mitambo inaingia na kukaguliwa kwamba inafaa na inafungwa na wataalamu waliobobea na si watoto wa shangazi ambao ni fundi mchundo pale gereji. Na katika masuala ya ajira pia wenye kiwanda wanahakikisha wanajua wanahitaji kuajiri watu wangapi, wenye sifa gani na kwa malipo gani.


Utaratibu wa ajira pia unafuatwa ili kuhakikisha kila anayeajiriwa ni yule mwenye sifa kuwazidi wengine bila kujali kabila, dini au undugu na mwenye kiwanda. Na hata uzalishaji unapoanza kunakuwa na taratibu za kimenejiment za wazi za kufuatwa kuhakikisha kila kitengo kinatimiza wajibu wake kwa wakati na kwa ufanisi ili uzalishaji ufikie malengo yaliyowekwa.


Matokeo yake, kiwanda kinafanya vizuri na kupata faida kubwa na kutoa bonasi kwa wafanyakazi kitu kinachoongeza ari yao na dhamira ya kufanya kazi kwa kujituma zaidi na kwa ubunifu zaidi ili mwaka ujao uzalishaji uongezeke na bonasi yao pia iongezeke. Matokeo yake, familia za waajiriwa wale zinakuwa na furaha na maendeleo na zinasoma vizuri, zinapata matibabu mazuri na zinakuwa familia bora za watu wanaofikiri sawasawa.


Ninayo mifano kadhaa (labda siku moja nitaitumia wahusika wakiniruhusu) ya mashirika (japo machache sana) ambayo kwa miaka mingi yalikuwa ya ovyo kabisa yakawa yamelazwa ICU yakisubiri kufa.

Tukumbuke kwamba serikali ya awamu ya tatu iliyauza sana mashirika ya umma kwa sababu moja kubwa kwamba yalikuwa yameshindwa kujiendesha kwa faida.

Lakini kumbe walikuwapo vijana Watanzania waliopata elimu wakaelimika, wenye uzalendo katika damu zao na wenye ubunifu wa asili ambao kwa bahati ilitokea wakapewa mashirika fulani ya umma katika miaka ya hivi karibuni. Waliyakuta yamejaa vumbi na watu waliokata tamaa, waliokuwa wakisubiri kuuza chochote walichokiona cha thamani katika ofisi ili waendelee kuishi. Vijana wale walikuta mashirika ambayo kila mwaka yalipeleka bajeti ya fedha yaliyohitaji kutoka serikalini ili yaweze japo kulipa mishahara ya wafanyakazi waliobaki.


Lakini wao waliamua kutumia uzalendo wao, elimu yao, ubunifu wao na kuyabadili kabisa mashirika yale kiasi kwamba vigogo wa wizarani wakaanza kuyatamani ili waweke watu wao kwa sababu sasa yalikuwa yameanza kuingiza fedha. Somo tunalolipata hapa ni kwamba kumbe unaweza kuwa na meneja A,B na C ambao hawana uzalendo, hawakuelimika vizuri na hawana ubunifu ila wana tamaa wakaua kiwanda.


 Lakini waweza pia ukawa na meneja X,Y na Z, wenye sifa na uzalendo wakakifanya kiwanda kile kile kiikafufuka bila hata kuwekeza fedha zaidi na kikawa kinapata faida, kinalipa kodi serikalini (badala ya kuomba ruzuku) na wafanyakazi wakawa na maisha bora tena yenye matumaini.

Na hili ndilo hasa tatizo kubwa la bara letu. Nchi zetu bado zinaendeshwa kama kiwanda cha kwanza hapo juu, kile cha majuha ambao kila mmoja alifikiria namna ya kunufaika yeye binafsi na hatua ya kwanza tu ya uanzishwaji.


 Matokeo yake siyo wenye kiwanda wala waajiriwa wao wanaokuja kuendelea kunufaika na kiwanda kwa muda mrefu. Uendeshaji wa kiwanda unahitaji fikra za kisayansi ambazo zikichakachuliwa na ujinga au tamaa ya wenye kiwanda au waajiriwa basi kinakufa.

Katika nchi hali kadhalika. Mnaanza kwa misingi, kama waasisi wa nchi yetu walivyoanza. Mnakubaliana ili nchi iende vizuri ukienda kununua meli halafu ukaacha kununua mpya ukafuata kuukuu ukaomba wakupakie rangi, ili utengeneze vijisenti vya familia yako, ukirudi unachapwa viboko.

Na mara nyingi kinachotokea katika nchi zetu ni kwamba wanaokosea, halafu makosa yao yanashuka hadi chini kabisa, ni viongozi wakuu. Wao, wenye kiwanda, wanapoanza na kununua mitambo mibovu ya kiwanda, na baadaye kuajiri wafanyakazi kwa misingi ya upendeleo, basi wanakuwa wamejenga msingi wa uborongaji kuanzia juu hadi chini.
itaendelea

No comments: