Thursday, January 30, 2014

KUELEKEA UCHAGUZI MKUU 2015.............  LOWASSA AMEANZA SAFARI, NI NDEFU KIASI GANI?

 Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa akiwasalimia wananchi waliohudhuria sherehe za mwaka mpya nyumbani kwake wakiwamo wabunge, viongozi wa dini, wafanyabiashara wakubwa na wakazi wa Mkoa wa Arusha na viongozi wa CCM. Kushoto ni aliyekuwa Naibu Waziri wa Ardhi, Godluck ole Medeye na kushoto mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Arusha, Onesmo ole Nangole.

“Nimefarijika sana leo kuwaona hapa marafiki zangu wengi. Ninapowatazama hadi machozi yananitoka na kwa uwezo wa Mungu tutashinda kwani nyote mnajua nia na ndoto yangu…WanaCCM msiwe na shaka, tutavuka kwa nguvu zetu... Wingi wenu huu unanipa faraja katika safari yetu na kwa kumtegemea Mungu tutashinda.”  ni kauli ya aliyewahi kuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa.

Lowassa alitangaza hivi karibuni kuanza rasmi kwa safari hiyo aliyoiita ya matumaini ya ndoto zake, ambayo anasema itatimiza ndoto za Watanzania za kupata elimu bure, majisafi na maendeleo ya uhakika.

Alitoa kauli hiyo katika ibada ya shukrani na kuupokea mwaka mpya, katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT),Usharika ya Monduli Mjini mkoani Arusha.

Bila ya kutaja safari hiyo ni ipi, Lowassa anawataka waliohudhuria ibada hiyo waungane na kaulimbiu yake, ‘Tulifurahi pamoja, tulihuzunika pamoja na tutashinda pamoja’.

Hafla hiyo ya kimkakati, ilihudhuriwa  na baadhi ya wabunge, wengi wakiwa wa CCM, wenyeviti wa mikoa kadhaa wa chama hicho, wakiongozwa na Mwenyekiti wa Wenyeviti wa CCM, viongozi wa jumuiya za chama na wengineo.

Licha ya kutoweka bayana aina ya safari anayoanza, Lowassa ni miongoni mwa wanaCCM wanaotajwa kuwa wanaowania urais, kumrithi Rais Jakaya Kikwete.
Dalili hizi za Lowassa kuutaka urais na kutafuta kabla ya kipenga kupulizwa, zimeishtua CCM na kumtahadharisha kuwa atapoteza sifa ya kupitishwa ifikapo 2015.

Safari tangu 1995
Tamaa ya Lowassa kuutaka urais haikuanza leo wala jana, ni ya tangu 1995 alipojitokeza kwa mara ya kwanza. Mwaka huo alikuwa miongoni mwa wagombea 17 wa CCM walioomba kuteuliwa kuipeperusha bendera ya chama hicho.

Majina hayo yalipaswa kujadiliwa na vikao vitatu vya CCM –Kamati Kuu, Halmashauri Kuu na Mkutano Mkuu. Kikao cha kwanza kilikua ni Kamati Kuu ambacho Mwenyekiti wake alikuwa Mwenyekiti wa CCM wakati huo, Ali Hassan Mwinyi lakini Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere alikuwa bado na ushawishi na nguvu kubwa ndani ya chama hicho.

Nyerere bila kumung’unya maneno, alisema wazi akiwataja wazi Lowassa na Waziri Mkuu mstaafu, John Malecela kuwa hawakuwa wanafaa kugombea.

Nyerere alisema Malecela alikuwa na madhambi mengi na kwamba alikuwa ameyabainisha katika kitabu chake cha ‘Uongozi na hatima ya Tanzania’ ambacho pia alielezea udhaifu wa Horace Kolimba, aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM.

Kuhusu Lowasa, habari zilizokaririwa kutoka kwenye kikao hicho, zilisema Nyerere alihoji utajiri wake;

“Huyu kijana wa miaka 42 tu amepata wapi utajiri wote huu? Licha ya kutetewa na wapambe wake, Lowassa hakufanikiwa kupenya kwenye hasira za Nyerere.

Baada ya mchujo kufanyika kwa wagombea hao 17, jina la Benjamin Mkapa likaibuka kidedea na kuchukua nafasi hiyo.

Aluta continua
Licha ya Nyerere kumwengua katika kinyang’amyiro cha urais mwaka 1995, Lowasa hakukata tamaa.
Baada ya Mkapa kupitishwa na hatimaye kuwa rais, Lowassa alijiunga na Rais Jakaya Kikwete aliyeleta upinzani mkali.

Kundi hilo ndilo lililomwezesha Rais Kikwete kupitishwa na CCM kugombea urais mwaka 2005 huku Lowassa akiteuliwa kuwa waziri mkuu.

Hata hivyo, ‘la kuvunda halina ubani’, mwaka 2008, Serikali iliingia kashfa ya uzalishaji wa umeme tata wa kampuni ya Richmond.
Sakata hilo lilipofikishwa bungeni, iliundwa Kamati iliyokuwa chini Waziri wa wa sasa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe ambayo hatimaye ripoti yake ilitosha kabisa kumwengua Lowassa katika nafasi ya hiyo na hivyo Baraza la Mawaziri kuvunjika.

Hilo lilikuwa pigo la pili la Lowassa kisiasa. Bado hakukata tamaa. Licha ya kutoweka wazi, Lowassa sasa anaonyesha kila dalili za kuutaka urais ifikapo 2015.

Katika jitihada hizo yeye na wapambe wake, wamefanya mambo mengi ikiwa pamoja na kuweka mtandao mpana wa wafuasi na kuhakikisha kundi lake linaingiza wajumbe wengi kwenye Halmashauri Kuu ya CCM na mkutano mkuu pia.

Mbinu nyingine wanazotumia kujiweka karibu na makundi mbalimbali ya kijamii kwa kutoa misaada ya aina mbalimbali, kuchangisha fedha makanisani na misikitini, kutumia vyombo vya habari, mitandao ya jamii na baadhi ya wabunge kumsafishia njia. Sasa ameanza kujiweka karibu vijana na hasa waendesha bodaboda.

Mbio hizi zitafika wapi?
Akizungumzia suala hilo, Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Gaudence Mpangala anasema mwendendo wa Lowassa hautoi sura nzuri kwa ndoto yake ya urais.

“Mimi ukiniuliza, nitakwambia, Lowassa hafai kuwa rais… kwanza alishapewa tamko na Mwalimu Nyerere mwaka 1995 akihojiwa kuhusu utajiri wake ameupata wapi na hakujibu. Sasa amekumbwa na kashfa ile ya Richmond, hadi akajiuzulu,” anasema na kuongeza:
“Watanzania tuwe makini, uongozi siyo lelemama, tutaivuruga nchi yetu.”

Profesa Mpangala amekikosoa Chama Cha Mapinduzi kwa kushindwa kuwadhibiti watu kama Lowassa.
“Hayo ni mambo ya chama… kama kweli ameshaanza kujinasibu, basi amekosea utaratibu wa chama, lakini hakichukui hatua. Hawa ndiyo walisema watajivua gamba, wameshindwa. Wanasema tu taratibu zimekiukwa lakini hawachukui hatua. 

Na Lowassa kwa kuwa ana utajiri na ushawishi mkubwa anaweza kupitishwa na kushinda,” alisema.
Hata hivyo, kwa upande mwingine, Mhadhiri wa Chuo Kikuu kishiriki cha Elimu  (Duce), Dk Kitila Mkumbo amemtia moyo Lowassa akisema anachokifanya ndiyo utaratibu wa demokrasia.

“Sioni kama Lowassa anatofauti na wana CCM wengine. Mengi yamesemwa juu yake lakini huwezi kuyashika mkononi. Ameshafafanua hadharani kuwa kashfa ya Richmond ilisababishwa na mfumo uliokuwapo, hivyo alijiuzulu kwa niaba ya CCM,” anasema 

Dk Mkumbo na kuongeza:
“Nashangaa watu wanapozuiwa kujinadi kugombea urais mapema, huo ni ushamba. Mfumo wa vyama vingi wa kiliberali tofauti na chama kimoja ambao ungesubiri kutangazwa, unajiuza mwenyewe.”
Akizungumzia zuio la Mwalimu Nyerere kwa Lowassa mwaka 1995, Dk Mkumbo anasema yalikuwa ni maoni yake binafsi.

“Mambo mangapi yalisemwa na Mwalimu Nyerere na hatuyafuati? Ni kweli aliandika katika kitabu chake cha ‘Uongozi na Hatima ya Tanzania’ lakini Lowassa hayumo. Ni kweli alisema na tunamheshimu lakini hatulazimiki kuyafuata,” anasema Dk Mkumbo.


MWANANCHI:

No comments: