Friday, December 13, 2013

TETESI: RAIS KUPANGUA BARAZA LA MAWAZIRI.IMEELEZWA kuwa Rais Jakaya Kikwete wakati wowote kuanzia Desemba 15, mwaka huu atafanya mabadiliko makubwa ya Baraza lake la Mawaziri. Hatua ya kwanza ya mabadiliko hayo imeanza kwa kumteua Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), Idara ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Asha-Rose Migiro kuwa Mbunge wa Viti Maalumu na kwamba huo ni mkakati wa kumkabidhi mama huyo Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi inayoshikiliwa na Dk. Shukuru Kawambwa.
Kwa mujibu wa taarifa za ndani, zimeeleza kuwa hatua hiyo ya rais imekuja kufuatia uwepo wa shinikizo la ndani na nje ya chama chake la kuwataka baadhi ya mawaziri wake kujiuzulu kutokana na kushindwa kutekeleza majukumu yao kikamilifu.
Imeelezwa kuwa Wizara ya Elimu inaonekana kusuasua na mtu pekee anayetajwa kuimudu wizara hiyo kwa sasa ni Dk. Migiro ambaye pia alishawahi kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.
Uteuzi wa ubunge wa Dk. Migiro ulitangazwa jana na Kaimu Katibu Mkuu Kiongozi, Dk. Florens Turuka ambaye alisema uteuzi huo umeanza jana.
Dk. Migiro ambaye pia anatajwa kuwa chaguo la kwanza la baadhi ya wakubwa wa CCM kwenye kinyang’anyiro cha urais kwenye uchaguzi ujao, amekuwa katika ziara za chama hicho zinazoendelea, jambo ambalo linatafsiriwa kuwa ni mikakati ya kumtambulisha mama huyo kwa wananchi.
Kabla ya kwenda UN, Dk. Migiro alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, nafasi aliyoonekana kuitumikia vema.
Aidha uteuzi wa Dk. Migiro umekuja katika kipindi ambacho joto la mabadiliko ya baraza la mawaziri likizidi kupamba moto, kutokana na udhaifu wa baadhi ya mawaziri kiutendaji.
Dk. Migiro ambaye amekuwa akitajwa kuwa mwanamke shupavu kiutendaji, wachambuzi wa masuala ya kisiasa na wasomi, wamekuwa wakimwona kama mtu anayefaa kuongoza wizara yoyote kwa maslahi ya taifa.
Akizungumzia uteuzi huo wa ubunge, Dk. Migiro alisema kuwa ameupokea kwa unyeyekevu na kwamba anamshukuru Rais Kikwete kwa kuonesha imani kubwa kwa wanawake na kwamba ataitumikia nafasi yake hiyo kwa weledi.
Baadhi ya mawaziri ambao wamekuwa wakipatiwa shinikizo la kujiuzulu ni pamoja na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Kawambwa na Naibu wake, Philip Mulugo, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chiza, Naibu wake, Adam Malima pamoja na Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe.
Kinana amekuwa akiwaandama mawaziri hao, huku akishinikiza kuwashughulikia ndani ya Kamati Kuu ya chama hicho kwa kile alichodai wanakiangusha chama chao kwa kushindwa kutatua kero za wananchi ambao wanazidi kupoteza imani na CCM.
 
Kutokana na dhana hiyo, imeonekana wazi kumshtua Rais Kikwete katika kuonesha dalili za kufanya mabadiliko ya baraza hilo la mawaziri, ili kuweka sawa upepo wa kisiasa ndani ya chama chake.
Hali kama hiyo ilitokea pia Mei mwaka jana, ambapo Rais Kikwete aliwateua wabunge watatu wapya ambao ni James Mbatia, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, na Naibu Waziri wa Fedha na Uchumi, Janeth Mbene.
Taarifa za uhakika zimebainisha kuwa mabadiliko ya mawaziri yatafanyika mara baada ya kikao cha Kamati Kuu ya CCM kukutana mjini Dodoma wiki ijayo.
MTANZANIA

No comments: