Thursday, December 19, 2013

MENGINE MAPYA GESI, MAFUTA.WAKATI Tanzania ikielekeza nguvu katika udhibiti wa mapato ya gesi na mafuta baada ya kuyapoteza kwenye madini, mjadala umezuka kuhusu Chapisho la Maliasili (Natural Resource Charter –NRC) lililoandaliwa Ulaya, linalopigiwa debe liasiliwe kama Hati Maalumu ya usimamizi wa shughuli za uziduaji (gesi, madini na mafuta) barani Afrika.

Chimbuko la mjadala huo, kwa mujibu wa wapinzani wa NRC, ni kwamba limeandaliwa na vyombo vilevile vya kimataifa vilivyoandaa mikataba laghai ya madini na linalenga kufanya mambo yale yale ambayo yanapendekezwa na vyombo kadhaa vya Kiafrika kama vile Africa Mining Vision (AMV) na Africa Peer Review Mechanism (APRM).

AMV na APRM ni vyombo ambavyo vimepitishwa na vikao vya juu vya viongozi wa Afrika. APRM iliridhiwa na Bunge la Tanzania Februari 2005, ripoti yake ya karibuni kabisa kuhusu Tanzania, iko katika mchakato wa mwisho wa kuzinduliwa.
Mjadala huu unakuja katika wakati ambao nchi za Afrika, ikiwamo Tanzania, zenye utajiri mkubwa wa madini, gesi asilia na mafuta, zikitafuta suluhisho la ndani ya Afrika kwa matatizo yake ya upotevu mkubwa wa mapato.

Utajiri mkubwa wa madini umekuwa ukinufaisha kampuni za kimataifa kutokana na mikataba tata isiyo na faida kwa nchi za Afrika, ikiwamo Tanzania. Mikataba hiyo ilibuniwa na kampuni hizo na mashirika ya fedha ya kimataifa na Benki ya Dunia (WB).
Wapinzani wa NRC wanasema kwamba hakuna tofauti kubwa kati ya waasisi wa NRC na mashirika kama WB hata kama ndani ya Bodi ya NRC kuna majina ya watu mashuhuri katika Afrika, kama vile Mo Ibrahim, tajiri mkubwa wa vyombo vya mawasiliano na mzaliwa wa Sudan; na mwanamama, Luisa Dias Diogo, aliyepata kuwa waziri mkuu wa Msumbiji.

Wajumbe wengine wa Bodi ya NRC, ni Ernesto Zedillo, rais wa zamani wa Mexico; Mkurugenzi Mkuu na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mfuko wa Uarabu wa Uchumi na Maendeleo,  Abdlatif Y. Al-Hamad na Mwenyekiti wa Citigroup Asia-Pacific, Shengman Zhang, ambaye alipata pia kuwa mkurugenzi wa WB wa China.

Raia Mwema limeambiwa kwamba nchini Tanzania, NRC iko katika hatua za juu za kuasiliwa katika mchakato ambao unaongozwa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, na kwamba shughuli zake zitakuwa zikiratibiwa na Wakala wa Serikali, Uongozi Institute, ulioko Dar es Salaam.

Balozi Sefue hakuweza kupatikana kuzungumzia mchakato huo kwa vile wakati tukienda mitamboni alikuwa safari nje ya nchi. Mawasiliano na Uongozi Institute yalieleza kwamba taasisi hiyo haijawa tayari kuzungumzia NRC kwa waandishi wa habari wakati huu.

“Asante sana kwa barua pepe yako kuomba mahojiano kuhusu NRC ambayo inatarajiwa kuwa ikifanya kazi zake kutokea Uongozi Institute. Kwa wakati huu NRC iko katika hatua za mwanzo, kwa hiyo tunashindwa kuandaa mahojiano kwa sasa. Nitaweza kuwasiliana nawe mapema iwezekanavyo, hata hivyo, hiyo ikiwa ni kama tutakuwa katika nafasi nzuri ya kuzungumza na vyombo vya habari kuhusu chapisho hilo,” aliandika Meneja Mawasiliano wa Uongozi Institute, Hanna Mtango, kumjibu mwandishi wetu.

Katika kujinadi, NRC inataja maeneo yapatayo 12 kuziambia serikali za nchi husika jinsi ya kusimamia na kukabiliana na changamoto za uziduaji, kwa vile kama changamoto hizo zikikabiliwa sawasawa, zitatoa fursa na maendeleo kwa kizazi cha sasa na vizazi vijavyo.
Hata hivyo, NRC inaonya kwa kusema endapo changamoto hizo zikitumika vibaya “zinaweza kuzua mtafaruku wa kiuchumi, mizozo katika jamii na uharibifu wa kudumu wa mazingira.”

Baadhi ya waasisi wa NRC, akiwamo Profesa Paul Collier, Mkurugenzi wa Kituo cha Stadi za Uchumi wa Afrika, katika Chuo Kikuu cha Oxford, Uingereza, wanazungumzia sehemu ya maneno ya utangulizi wa NRC wakisema: 

“Lengo la NRC ni kuzisaidia Serikali na jamii za nchi tajiri wa maliasili zinazoweza kwisha, kuzitumia maliasili hizo katika mfumo ambao utakuza uchumi, utaboresha maisha ya jamii na zitakuwa endelevu kimazingira.”  

Hivi karibuni, Profesa Collier alikuwa nchini Tanzania na alifanya mahojiano na Uongozi Institute kwa pamoja na Balozi Ami Mpungwe.

Kwa upande wao, waasisi wa AMV wanasema, pamoja na mambo mengine kwamba: “Africa Mining Vision ni matokeo ya jitihada na kazi mbalimbali za ki-maeneo, ki-Bara (Afrika) na ki-dunia kubuni sera na miundo ya usimamizi ili kupata matokeo mazuri ya shughuli za uziduaji.
“Jitihada hizo ni pamoja na Johannesburg Political Declaration and Plan of Implementation [sura ya 46 na aya f na g za sura ya 62 (Sustainable Development for Africa)} World Summit on Sustainable Development; Yaoundé Vision on Artisanal and Small-scale Mining; Africa Mining Partnership’s Sustainable Development Charter and Mining Policy Framework; SADC Framework and Implementation Plan for Harmonisation of Mining Policies, Standards, Legislative and Regulatory Frameworks; UEMOA’s Common Mining Policy and “Code Miniere Communautaire”; Summary Report of the 2007 Big Table on “Managing Africa’s Natural Resources for Growth and Poverty Reduction” iliyoandaliwa kwa pamoja na ECA na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB);na International Study Group to Review Africa’s Mining Regimes (ISG).

Wanaongeza waasisi wa AMV: “Mabadiliko ya kimuundo katika uchumi wetu, ni lazima yawe sehemu yenye umuhimu mkubwa kwenye mkakati wa muda mrefu wa kufikia Malengo ya Milemia (MDGs) katika Afrika, kuondoa umasikini na kusimika maendeleo endelevu. Ufunguo wa haya yote, hata hivyo, umo katika uundaji na utekelezaji mikakati mahsusi iliyobuniwa kuzingatia nafasi ya pekee ya hazina ya Afrika badala ya kutegemea (tu) uzoefu wa nje ya Bara hilo.”

Kati ya watetezi wakubwa wa AMV, ni Antonio Pedro, raia wa Msumbiji ambaye ni Mkurugenzi wa eneo la Afrika Mashariki, katika ofisi za Umoja wa Mataifa, Kamisheni ya Uchumi ya Afrika (UNECA), Addis Ababa, Ethiopia, anayehusika na masuala ya uziduaji.

Ukiacha kuwa yeye ni kati ya waasisi wa AMV, amekuwa msitari wa mbele kuhakikisha kuwa maono ya AMV yanatekelezwa katika nchi za Afrika zilizo tajiri wa maliasili. Na hiyo si bure, yeye ni mjiolojia mziduaji kwa miaka 30 ambaye amekuwa katika shughuli hizo nchini mwake, katika maeneo kadhaa ya Afrika na katika ngazi ya Bara hilo, akiwa amepata kufanya kazi kama mkurugenzi mkuu wa Kituo cha Utafiti wa Madini cha Kusini na Mashariki mwa Afrika (SEAMIC) kilichopo Kunduchi, Dar es Salaam, Tanzania.

Msingi wa hoja ya Pedro na wenzake, ni kwamba tangu katika miaka ya 1990, Afrika imekuwa msitari wa mbele katika kuleta mageuzi kwenye sera za madini. Matokeo yake, ni ongezeko la uwekezaji kutoka nje, ugunduzi wa maeneo mapya ya madini na ongezeko katika uuzaji nje wa madini hayo.

Wanasema kina Pedro na wenzake: “Hata hivyo, (pamoja na jitihada zote hizo), bado hazijatosha kuwa na sekta endelevu ya madini ambayo ina mtangamano wa kijamii na kiuchumi ili kuwezesha matarajio ya muda mrefu ya maendeleo ya umma wa Afrika.”
Kwa maoni yao kina Pedro, AMV, iliyoasiliwa na Wakuu wa Nchi na Serikali za Afrika katika kikao chao Februari mwaka 2009, ni chapisho rasmi kwa nchi hizo linalozisukuma kuvuna utajiri wa maliasili, na hasa madini na kuyatumia mapato yake kupambana na umasikini.

Lakini wanasema ili Afrika iweze kufikia hatua ya kupambana na umasikini kwa kutumia mapato yatokanayo na uziduaji, itahitaji viongozi wenye maono na uhusiano makini katika ngazi za ndani na nje ya nchi.

Itahitaji pia kuimarisha uwezo wa kitaasisi wa vyombo na mamlaka mbalimbali kwa maana ya mipango ya muda mrefu, menejimenti makini, matumizi yenye tija, uwekaji akiba na uwekezaji mzuri wa mapato yatokanayo na uziduaji.

Kwa upande wake, ripoti ya APRM kwa Tanzania inarejea ukweli kwamba pamoja na Tanzania kuwa mzalishaji mkubwa wa dhahabu, mapato yatokanayo na madini hayo hayajaweza kuleta tija iliyotarajiwa miongoni mwa jamii.

“Watanzania wa kawaida hawafaidiki na mapato ya uzalishaji mkubwa wa dhahabu kwa sababu serikali iliridhia mikataba ya kodi inayozipendelea sana kampuni za kimataifa za uchimbaji madini,” inasema sehemu ya ripoti ya APRM ya Tanzania kuhusu mapato yatokanayo na madini.

Inaongeza ripoti hiyo iliyopitishwa Januari mwaka huu: “…kuna dhana inayojikita miongoni mwa wanajamii kwamba maliasili na utajiri wa Tanzania unaporwa. Kati ya mwaka 1997 na 2005, Tanzania ilisafirisha nje ya nchi dhahabu ya thamani ya zaidi ya dola za Marekani bilioni 2.54. Katika kipindi hicho serikali ilipata dola za Marekani milioni 28 kila mwaka katika kodi na mirabaha ambayo ni karibu asilimia 10 kwa muda wa miaka tisa.”

Kwa ajili ya upotevu huo wa mapato, paneli ya APRM imependekeza kwa Serikali ya Tanzania nini cha kufanya. Mapendekezo hayo, ni pamoja na Tanzania kupitia upya sera za madini na irekebishe sheria za madini ili uchumi na umma wa Watanzania ufaidike na shughuli za uziduaji; na zaidi ichapishe wazi mikataba ya sasa ya madini, na Bunge liiridhie.

Katika moja ya hotuba zake za mwisho wa mwezi Rais Jakaya Kikwete, Januari, 2013, alizungumzia Ripoti hiyo ya APRM Tanzania akisema pamoja na mambo mengine kwamba Tanzania ilipongezwa kwa mambo mengi na  “… tumepewa ushauri kwa baadhi ya maeneo waliyoona hatuna budi kuyaboresha.  Niliwashukuru na kuahidi kuufanyia kazi ushauri huo”.

Ni Rais Kikwete, wakati huo akiwa waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa,  aliyesimamia mchakato wa Tanzania kujiunga na APRM. Baada ya Bunge kuuridhia Februari 2005, Septemba 2009 akizindua Baraza la Usimamizi la Taifa alisema sababu za kujiunga na APRM zilikuwa ni pamoja na kutaka kuendeleza uwazi na kuimarisha utawala bora.

Alisema Rais Kikwete wakati huo: “ Tulijiunga na mchakato huu kwa sababu tunakubaliana na malengo yake. Tanzania inaheshimu utawala bora na iko tayari kushirikiana na nchi nyingine za Afrika kujifunza kuwahudumia vyema wananchi”.

Katibu Mtendaji wa APRM Tanzania, Rehema Twalib, anasema mapendekezo yaliyomo katika Ripoti ya APRM ni matokeo ya ushauri wa wadau.

“ Ushauri huo wa wadau unahusu kuhakikisha kuwa utekelezaji wa sheria, taratibu na kanuni zilizopo unafanyika kikamilifu na kusimamiwa vema na zile ambazo hazikidhi zinafanyiwa marekebisho ili kupata mafanikio katika sekta hii,” anasema Rehema Twalib.

Anongeza: “Ni kuhakikisha kuwa sheria za kazi, sheria za fidia na usalama mahala pakazi zinazingatiwa vema; kuhakikisha kuwa ulipaji wa fidia kwa maeneo yanayotwaliwa kwa shughuli za uziduaji unafanyika kwa haki na kwa wakati; kuhakikisha kuwa utekelezaji wa sheria za mazingira unasimamiwa kikamilifu na zile sheria ambazo si rafiki kwa mazingira zinafanyiwa marekebisho.”

Kwa mujibu wa Rehema Twalib, jukumu la APRM Tanzania ni kufuatilia utekelezaji wa maoni hayo ya wadau, ambao  unafanywa na wizara, idara na wakala za serikali pamoja na sekta binafsi, na hatimaye kutoa mrejesho kwa wadau juu ya utekelezaji huo kwa kuandaa taarifa za kila mwaka.

Je, Sekretariati ya APRM Tanzania inaweza kusaidiaje kuleta utawala bora na uwazi katika utawala wa shughuli za uziduaji Tanzanaia?
Anasema Rehema Twalib: “ Jukumu la APRM Tanzania ni kuratibu tathmini za utawala bora kwenye sekta mbalimbali, sekta ya uziduaji ikiwa mojawapo. 

“ Kwa mfano, katika sekta hii, tathmini hufanyika juu ya hatua zilizochukuliwa na nchi husika katika kusimamia na kukuza utawala bora katika sekta ya uziduaji, ikiwa ni pamoja na kutathmini mifumo ya kitaasisi na kisheria, uingiaji wa mikataba, kufuata sheria  na viwango vya Kimataifa  vya Uwazi katika Sekta ya Uziduaji(EITI)na uwezeshwaji na ushirikishwaji wa wananchi katika sekta hii.

“ Hivyo APRM Tanzania itasimamia tathmini za kuangalia maeneo ambayo nchi inafanya vizuri, kwa ajili ya kuendelea kuyaboresha na kuigwa na wengine, na pia yale maeneo yenye changamoto kwa ajili ya kuyafanyia kazi, ili hatimaye sekta hii iweze kuchangia kikamilifu katika kukuza uchumi na kuleta maendeleo”. 

Rehema Twalib anasema Ripoti ya APRM Tanzania inatarajiwa kuzinduliwa katika kipindi cha Januari- Machi 2014. Hiyo ni kwa kuwa kulingana Miongozo ya APRM, baada ya Ripoti kusomwa, muda zaidi huhitajika wa kuitafsiri katika lugha nyinginezo za kimataifa zinazotumika Afrika, ikiwa ni pamoja na Kifaransa, Kireno, Kispaniola na  Kiarabu pamoja na kuihariri. 

Anasema pia inatakiwa kuiwasilisha kwenye vyombo muhimi vya Utawala Bora vya Bara la Afrika kama vile Bunge la Afrika, Tume ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Afrika.
Anasema ndani ya APRM Tanzania zipo taarifa za NRC na kwamba kwao NRC ni taratibu kwa ajili ya serikali na jamii juu ya namna bora ya kutumia fursa katika sekta ya uziduaji kwa ajili ya kujiletea maendeleo hasa kwa kutumia mifano ya nchi zilizopata mafanikio kwa kutumia vema sekta ya uziduaji. 

“ Kimsingi ni  chapisho la kuhimiza uwazi na uwajibikaji katika sekta ya uziduaji kulingana na sheria na viwango vya kimataifa.
“ Kwa upande wake APRM ni Mpango unaoratibu tathmini ya utawala bora kwa lengo la kubaini maeneo ambamo nchi inafanya vizuri na yale yenye changamoto ili zifanyiwe kazi. Jambo lililo wazi ni kuwa NRC na APRM ni vyombo vinavyosaidiana kuchochea maendeleo ya nchi kwa kuwashirikisha wadau”.

Mmoja wa Watanzania magwiji wa mikataba ya shughuli za uziduaji Dk. Rugemeleza Nshala anasema Chapisho hilo la Maliasili halitakuwa na tija kwa Afrika wala kwa Tanzania.
Anasema Dk. Nshala kuhusu NRC: “Julai mwaka 2011, nikiwa Accra, Ghana, nilipata nafasi ya kuona muswada wa awali wa Chapisho la Maliasili. Mmoja wa waandishi wake kutoka Chuo Kikuu cha Oxford alitupatia na alikuwa akitaka kuungwa mkono na washiriki kutoka nchi za Kiafrika.

“Baada ya kulipitia tulilipinga kwani lilikuwa halilengi kushughulikia kwa ukamilifu udhaifu katika sekta ya uchimbaji madini na mafuta.  Nilidhani ujumbe umefika.
“Baada ya kusoma toleo lake la sasa, mtu anaweza kusema kuna baadhi ya mambo mazuri ndani yake, lakini hoja kubwa si kuzifanya nchi zinazondelea kuwa vinara katika sekta hii, bali washirika waangalifu. 

“Ni wazi kwamba lengo ni kuyawezesha makampuni makubwa ya nje na sekta binafsi kuwa ndiyo vinara wa uchimbaji na uendeshaji wa sekta hii.  Hili si jambo zuri.
“Lengo linatakiwa (liwe) kuzifanya nchi zetu kuwa ndizo wamiliki wakuu wa sekta hii na kuwa kampuni binafsi za ndani na nje zinafanya kazi ya kuunga mkono na kuboresha tu. 

“Umiliki wa nchi kupitia kampuni za serikali, zinazoongozwa kwa misingi ya biashara makini, bila kusahau jukumu lake kwa taifa, ndizo ambazo zinatakiwa kuwezeshwa kuongoza sekta hii. Aidha, serikali inaweza kuingia ubia wa haki na wazi na kampuni za nje kuendesha sekta hii. Ubia huu ujumuishe serikali kuwa na hisa katika kampuni mama ya kampuni hizo.”

Kwamba Tanzania imekuwa katika mchakato wa kujiunga katika NRC ni habari mpya kwa Dk. Nshala: “Kwa hapa Tanzania siwezi kusema (mchakato) umefikia wapi kwani sina habari kuwa nchi yetu ina nia ya kuwa na mchakato wa kujiunga nao. 

“Kama ndivyo basi inabidi kuwe na mchakato wa wazi na wenye nia njema kuweza kujadili mazuri na mabaya yake na kuona yepi kama nchi tunayakubali na yapi hatuyakubali. Si lazima ukubaliane na kila kilichomo. 

“Ukweli ni kuwa michakato kama hii inalenga kupunguza kelele za upinzani wa mfumo wa kinyonyaji ambao nchi zinazoendelea zinafuata.  Unatoa muda kwa kampuni na wachukuaji wa nje kuendelea na shughuli zao hapa nchini na kwingineko huku wakisema wamerekebisha mambo kwa kufuata Agano hili la Maliasili.”

Anaongeza Dk. Nshala kuhusu NRC: “Machapisho kama haya na mengineyo,  yanakuwa hayana maana sana kwani ni mambo ya hiari. Mtu anaweza kusema kuwa Chapisho la Maliasili ni nyongeza ya matamko na mikakati iliyofikiwa siku za nyuma. Lakini inasukumwa na watu na asasi zenye nguvu. 

“Cha maana ni kuwa Watanzania ndio ambao wanatakiwa kuamua jinsi gani rasilimali zao za asili zitumike. Machapisho na mikakati kama hii si matokeo ya michakato ya ndani ya nchi bali ni ya kutoka nje na halina uhalali wa kisheria, jamii na kisiasa.

“Ni vema kwa nchi kama Tanzania, kukaa kitako na kujiuliza hivi hii njia tuliyomo ni sahihi? Mbona licha ya kuchimba madini kwa viwango na ujazo mkubwa nchi yetu haijanufaika? 

“Je, tuendelee kuamini wale ambao wanatuambia kuwa tuwe na uvumilivu wakati vyetu vikiliwa?  Na tusiwashutumu wale ambao wanadai pawepo umakini na kufuatwa kwa dhati kwa matakwa ya Ibara 9 (c) na (i) na 27(1)-(2) za Katiba ya nchi (hawa) si watu wasiojua kuwa nchi yao inaporwa. Wao ndio wenye mali na hilo ni vema wale waliopewa madaraka ya kuongoza sekta au wizara husika walielewe. Wao ni watumishi wa wananchi na wanawajibika kwa wananchi na si makampuni makubwa ya nje au taasisi za fedha za nje.”

Wapo wenye maoni kwamba wakati huu wa kutafuta suluhisho la Afrika kwa matatizo ya Afrika kuibeba NRC ni kurejea katika mwongo mmoja na zaidi uliopita pale WB na vyombo vingine vya kimataifa, vilipoisukuma Afrika (Tanzania) kuingia mikataba ya uchimbaji madini ambayo imekuwa ikinufaisha makampuni ya nje kwa maana ya mapato. 

Dk. Nshala naye hayuko mbali na kundi hili. Anasema: “Nadhani kuna ukweli katika hilo, kwa sababu Chapisho la Maliasili, halilengi kuharamisha mikataba yote ambayo iliingiwa kwa hila na rushwa, au ambayo ni ya kinyonyaji. 

“Ujumbe ni kwamba yaliyopita si ndwele tugange yajayo! Tutagangaje yajayo wakati tunaporwa vyetu? Ukweli ni kuwa mikakati yote ile, ni lazima ituwezeshe kufutiliwa mbali mikataba ya shaka ambayo ilisainiwa na watu ambao ama walikuwa hawaelewi, kama Chifu Mangungo wa Usagara. Kwa nini walikuwa wakisaini au walikuwa na nia mbaya na nchi yetu?  

“Uchimbaji mkubwa wa madini unaendelea hivi sasa, je, nchi yetu inanufaika? Jibu li wazi, hapana? Sasa tunyamaze na tuache hayo? Katu kamwe.
“Ni muhimu sisi kama Watanzania tuamke na kudai kupata manufaa ya kweli kutoka kwenye rasilimali zetu na tusiwe kama mazuzu. Watu wanatuibia na sisi tunachekelea. Ni dhambi kubwa kwetu wenyewe, kubwa zaidi kwa watoto na wajukuu wetu, na isiyosameheka kwa Mwenyezi Mungu”.

Kutokulipa kabisa kodi ama kulipa katika miaka miwili au mmoja wa karibu na kufunga shughuli za uchimbaji madini, tena katika viwango vinavyoashiria ulaghai, ni kilio kikubwa cha muda mrefu miongoni mwa Watanzania, wanazuoni na wanajamii kwa ujumla, waliokuwa wafaidike kwa uchimbaji madini, mali asili inayopungua kila inapochimbwa, kwa maana kwamba siku moja itaisha kabisa.

Mpango wa Uhamasishaji wa Uwazi na Uwajibikaji Katika Tasnia ya Uziduaji Tanzania ( Tanzania Extractive Industry Transparency Initiative –TEITI) umekuwa ukielezea katika ripoti zake tatu zilizopita kwamba kampuni za uchimbaji madini, na hasa dhahabu, haziilipi Tanzania kodi stahiki na kwamba mapato mengi yanapotea.
“Malipo ya kodi ya shirika (corporate tax) ya kampuni za uziduaji yamekuwa hafifu, na kwa maana hiyo yamekuwa hayaisaidii serikali kupata mapato stahiki ya ndani kwa sababu kampuni nyingi za uchimbaji madini zimekuwa hazilipi kodi ya shirika.

Juni mwaka huu, TEITI ulitangaza ripoti yake ya tatu ya shughuli za uziduaji nchini ambayo kama ripoti  za kwanza na pili, zilizotangulia, inaonyesha kwamba mapato ya serikali katika sekta ya uziduaji yanatokana na mirahaba na kodi za kwenye mishahara (kodi ya mishahara ya wafanyakazi ambayo hukatwa kila mwezi kwa mujibu wa sheria).

Kati ya mambo ya msingi aliyoyasema wakati wa kutangaza ripoti hiyo ya tatu, Mwenyekiti TEITI, Balozi Mark Bomani, alieleza ya kuwa Tanzania haifaidiki na maliasili zake katika shughuli za uziduaji hiyo ikitokana na mikataba mibovu iliyoingiwa katika miaka ya 1990.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya tatu ya TEITI mapato ya serikali kutokana na gesi na madini yalikuwa dola za Marekani milioni 330 mwaka 2010/11, hilo likiwa ni ongezeko la asilimia 19, lakini tena ripoti hiyo inaongeza ya kuwa sehemu kubwa ya mapato hayo ilitokana na mirabaha na kodi za mishahara ya wafanyakazi.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo mapato yatokanayo na kodi ya shirika (corporate tax) yaliongezeka mara dufu ya mwaka 2009/10 kwa asilimia 15 ya mapato yote. Lakini ongezeko hilo linaitaja kampuni moja tu ya madini, Resolute ya Nzega, Tabora ambayo sasa imefunga mgodi baada ya kuvuna dhahabu kwa karibu miaka 10. 

Kodi ya shirika nyingine, kwa mujibu wa takwimu hizo ililipwa na kampuni ya gesi asilia ya Pan African Energy Tanzania Ltd, huku nyingine zikilipwa na kampuni za sementi.
Kampuni zinazomiliki migodi, hasa ya dhahabu, zimekuwa zikidai kwamba hazipati faida na kwa ajili hiyo kwa mujibu wa mikataba yao haziwezi kulipa kodi za shirika ambazo hupatikana baada ya kukokotoa mahesabu kwa kuondoa gharama za uzalishaji.

Takwimu zaidi zinaonyesha ya kuwa kati ya kampuni zote za madini nchini, ambazo zinaweza kutajwa kuwa zinapata hasara ni Williamson Diamonds (Mwadui) na TanzaniteOne (ya tanzanite) iliyoko Mererani, Simanjiro, Arusha.
Hayo yakiendelea, tayari migodi miwili ya migodi ya dhababu nchini Tanzania imekwishakufungwa ikiwa imelipa kodi ya shirika (corporate tax) mara moja katika uhai wa takriban miaka 10 ya uvunaji madini hayo.

Mgodi mwingine, wa tatu, North Mara, Tarime, uhai wake wa kuzalisha dhahabu utafikia ukomo mwaka 2020, ukiungana na migodi ya Golden Pride ama Resolute wa Nzega, na Tulawaka wa Biharamulo, iliyokwisha kufungwa kutokana na kutokuweza kuwa tena na uchimbaji wa faida wa dhahabu, ambao kwa muda wote huo haukuifaidia Tanzania kwa maana ya kodi stahiki zilizolipwa. 

Takwimu za TEITI, zinaonyesha kwamba migodi ya North Mara, Geita, Bulyanhulu na Buzwagi ambayo imekuwa ikichimba dhahabu, mingine kwa zaidi ya miaka 10 sasa, haijawahi kulipa kodi ya shirika.
Mgodi wa North Mara ulioko Tarime, Mkoa wa Mara unamilikiwa kwa asilimia 100 na African Barrick Gold, kampuni tanzu ya Barrick ya Toronto, Canada, iliyoingia mkataba wa kuchimba dhahabu na serikali mwaka 1999 na kuanza uzalishaji mwaka 2002. Kama ilivyoelezwa juu, uhai wa mgodi huo utafikia ukomo mwaka 2020, kiasi cha miaka saba ijayo.

Mgodi wa Bulyanhulu unamilikiwa pia na African Barrick Gold, upo Kahama, Mkoa wa Shinyanga. Mkataba wake uliingiwa mwaka 1994, uzalishaji mgodini ukianza mwaka 2001. Takwimu zinaonyesha kwamba uhai wa mgodi huu utafikia mwisho mwaka 2035.
Mwingine ni mgodi wa Buzwagi ambao nao uko Kahama mkoani Shinyanga ukimilikiwa pia na African Barrick Gold. Mkataba wake uliozua minong’ono mingi wakati ule, ulisainiwa mwaka 2007, huku kazi ya uvunaji dhahabu ikianza mwaka 2009. Kwa mujibu wa takwimu, uhai wa mgodi huu utakoma mwaka 2023, kiasi cha miaka 10 ijayo.    

Hakuna takwimu zinazoonyesha uhai wa mwisho wa mgodi wa Geita, ulioko Mkoa mpya wa Geita. Mgodi huo unamilikiwa na kampuni ya AngloGold Ashanti.Uzalishaji dhahabu mgodini Geita ulianza mwaka 2000 baada kuingiwa kwa mkataba mwaka 1999.

Kwa tafsiri ya takwimu za TEITI, kama hapatakuwa na ugunduzi wa migodi mingine ya dhahabu nchini Tanzania, maana yake ni kwamba ifikapo mwaka 2035, wakati mgodi wa Bulyanhulu ukifunga uzalishaji wenye faida, Tanzania itakuwa imevuna hazina yake karibu yote ya dhababu, lakini haitakuwa imepata mapato yoyote ya kuonyesha siku zijazo kuwa ilipata kuwa  mzalishaji mkubwa wa dhahabu duniani.

Kwa sasa Tanzania ni nchi ya nne kwa uzalishaji dhahabu barani Afrika ikitanguliwa na Afrika Kusini, Ghana na Mali, na ni karibu nchi ya 16 duniani kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2006. China ikifuatiwa na Australia na Marekani ndizo wazalishaji wakuu wa dhahabu duniani.

Kwa mtazamo wa mambo, asasi nyingi za ndani na nje ya Tanzania, zimekuwa zikishinikiza ama kufumuliwa au kupitiwa upya kwa Mikataba ya Uchimbaji Madini (MDAs) iliyoingiwa kati ya Serikali na kampuni za uchimbaji madini kwa ushauri wa (WB) na mashirika mengine ya kimataifa ili kuiwezesha nchi kufaidika na madini ambayo uhai wake una kikomo.


No comments: