Monday, December 16, 2013

KOMREDI KAUNDA ALIVYOMUAGA MADIBA NA WITO KWA VIONGOZI WA AFRIKAHotuba yake ilivutia na kutia hamasa kwani aliongea kutoka moyoni mwake hakuwa mnafiki kama ilivyokuwa kwa wengine wanaomsifu Madiba ilihali wananchi wao hawana ajira, maskini, hawana elimu, vipato duni, kiwango kati ya walionacho na wasionacho kuongezeka. Hatuwezi kumuenzi Madiba kwa speeches nzuri isipokuwa kwa matendo. Leo ni siku ya mapatano kwa nchi ya Afrika ya kusini na Rais Zuma atazindua sanamu kubwa ya Mandela maeneo ya Nelson Mandela Ampitheatre zamani Union buildings.

Wanasiasa waache unafiki waangalie mambo ya Msingi enzi za ukombozi zimekwisha na historia wanaijua sote historia twaijua na ni kweli waasisi wetu pamoja na Komredi Madiba waliitekeleza vyema. Sasa wao jukumu lao ni kuwakomboa wananchi katika ukombozi wa fikra kwa elimu bora, ukombozi dhidi ya umaskini na kujenga jamii zenye shabaha ya umoja katika kuleta gurudumu la maendeleo. Wenzenu wanatumia Ukomredi wetu kujitajirisha sisi tumebakia na historia. Angalieni CHINA.

Hata huyo Madiba sidhani kama atafurahi akiona utitiri wa viongozi wakimmwagia sifa lukuki wakati miongoni mwao ni mafisadi, wezi wa mali ya umma, wasaliti kwa wananchi na wala rushwa. Ni unafiki huu uliosababisha hata kumfanyia ndivyo sivyo Askofu Desmond Tutu ambaye anaijua historia ya ukombozi na anajua namna ambavyo wale waliokuwa wanajiita makomredi walivyotajirika isivyo halali na huku wananchi wa kawaida wanaishi katika maisha duni na wanasiasa hao kutotekeleza ahadi zao. 

Hakuna ambaye hafahamu mauaji ya wachimba madini ya Marikana na hakuna asiyejua namna viongozi na wanasiasa hao wanavyojitapa katika ukabila,udini,rangi, uchu wa madaraka juu ya mustakabali wa siasa za nchi na wengine wanataka kufia madarakani kwa kuvuruga matokeo, kujitengenezea katiba zitakazo wabakisha madarakani,kuwa na mifumo inayoua demokrasia na wakati huo huo  kuwa vibaraka wa mabwanyenye wa magharibi na kuanza kuwanyooshea vidole viongozi wenzao wa kiafrika yaani vurugu mtindo mmoja. 

Siasa ya nchi moja  na mifumo yake haitofautiani na siasa na nchi nyingine hususan kwa nchi za kiafrika.  Ni wakati wa viongozi kujifunza na kuacha kuwa na fikra mgando za kizamani ili kuweza kuyafikia mafanikio.

No comments: