Monday, November 18, 2013

UPUPU WA NGONO.
 Na Richard Mabala,


Haya, waheshimiwa na waishiwa wasomaji wangu, kwa mara nyingine tena, magazeti yanatoa habari ambazo iwapo ni kweli, yanazidi hata uwezo wa ubunifu wangu. Ndiyo maana nilipata barua kibao.

Makengeza,
Ni matumaini yangu kwamba maprofesa wetu wa sheria wanasikiliza kwa makini maneno yanayotolewa na watu wengine wanaojidai kuwa na wataalamu wa sheria. Kwa mfano wiki iliyopita tumeambiwa kwamba suala la ubakaji, hata kama limefikishwa hadi vituo vya polisi au kutangazwa hadharani, ni suala binafsi. Nadhani tafsiri hii itatusaidia sana (sisi wanaume hasa) pamoja na kusaidia serikali isilazimike kujaza jela kutokana na mihemko ya watu wanaoshindwa kuihimiliki. Kwa hiyo, katika vitabu vya sheria, pawe na sehemu kabisa na makosa binafsi. Na ili kuwasaidia kaka (na dada) zangu wasomi, naomba nitoe yafuatayo kama masuala binafsi, yanafanyika na watu binafsi na ubinafsi wao.
• Masuala yote ya jinsia ni masuala binafsi, yaani kupigwa kwa mke, kupewa ulemavu na hata kuuliwa ndani ya ndoa ni suala binafsi. Aidha, unyanyasaji kijinsia wa aina yoyote kuanzia kushikwashikwa hadi kubakwa na kunajisiwa uhesabiwe kuwa na suala binafsi pia. Ila iwapo mwanamume anapigwa na mwanamke, hili ni kosa la jinai maana hii inaenda kinyume cha maumbile.
• Unyanyasaji wa watoto ndani ya ndoa ni suala binafsi. Kwa mfano, mtoto akitumia vibaya shilingi mia mbili au hata elfu tano za baba au mama na kuchomewa mikono yake kama adhabu, ni dhahiri kabisa kwamba hili ni suala binafsi na litashughulikiwa kibinafsi pia.
• Wizi pia ni suala binafsi. Mtu anapokupimia oili ndani ya daladala, au hata kukutisha na panga na kukunyang’anya pesa ni suala binafsi. Hata ufisadi ni suala binafsi. Kwa nini mtu anaamua kufisadi. Ni kwa sababu, kwa maoni yake binafsi, anaona mfuko wake binafsi haujajaa kulingana na matakwa binafsi ya nafsi yake.
Ila tu, inabidi kutoa hadhari. Kulingana na misingi ya sheria asilia, inabidi kutofautisha kati ya walio nacho na wasio nacho. Ndiyo maana, mke akimpiga mume, lazima ashtakiwe kwa kufanya tendo kinyume cha maumbile. Naam. Simba akimrarua swala, atashtakiwa, lakini swala wakiungana kumwadhibu simba, lazima wachukuliwe hatua kwa pamoja maana wanatishia amani na utulivu wa mbuga. Na kwa binadamu vivyohivyo. Itakuwaje swala aamke na kulalamika kwamba simba amemrarua?
Simba mtarajiwa.
Haya na mwingine,

Makengeza,
Mimi nawashangaa Wabongo wenzangu. Mkubwa katembea na mdogo. Hata kwa kutumia nguvu. Kisha tunaambiwa ni suala binafsi. Kipya ni nini hapa. Tangu zamani, walinzi wetu wa usalama (hasa usalama wa madume na vigogo) wamesema siku nyingi.
‘We si ulikunywa bia zake ana haki ya kudai malipo.’
‘Yaani sista, kweli unataka kumuumbua mumeo. Hebu rudini nyumbani mpatane.’
‘Ha ha ha ha. Na nguo kama hii unategemea nini?’
‘Ubinadamu huo jamani. Angalia anavyopendeza (huku udenda ukidondoka)
Ndiyo maana wanawake wengi wamekuwa na utu na busara wa kunyamazia mambo hayo. Nyeti za dume ni suala nyeti na zinapaswa kubaki nyeti. Potelea mbali kama wananyamaza kwa sababu wanajua wanapoteza muda na heshima wakilalamika kwa sababu wanageuziwa kibao kila wakati. Potelea mbali kama wadogo hawana imani na mfumo ili mradi umegusa mkubwa. Suala ni kwamba wananyamaza hivyo ni suala binafsi na hakuna cha zaidi.
Ndiyo maana naona dunia imeharibika kabisa. Sisi wazee tunakumbuka enzi za blanketi mtu. Wakubwa wakienda mikoani watalalaje peke yao bila kutiwa joto kidogo. Hivyo blanketi chapa mtu ilikuwa sehemu muhimu ya huduma kwa kigogo. Na Redio Manzese iliwaongelea wakubwa wengi wenye upupu wa ngono maana walikuwa wanawashwa kila wakati na msichana mzuri ndiye pekee mwenye uwezo wa kumkuna. 

Waziri fulani alipachikiwa jina la Mgonjwa kutokana na tabia hii.
Kwa hiyo iwapo tabia hii inaendelea kuna shida gani. Tujali haki ya nani? Haki ya kadogo eti asinyanyaswe au haki ya kigogo kutowashwa? Ni wazi kabisa kwamba haki ya kigogo kutowashwa ni muhimu zaidi. Hata kama msichana ni mdogo namna gani si hoja. Haki ya kigogo inabaki palepale na tukishapukutisha haki hii, sijui tutafikia wapi.
Kigogo mstaafu.
Lakini mwingine hakukubaliana nao kabisa.

Mwishiwa mwenzangu,
Nategemea utaelewa kwa sababu wewe ni mwishiwa si mheshimiwa kama hawa wengine wenye ubinafsi wa nafsi katika kudai masuala ya jinai ni masuala binafsi. Hebu tuangalie stori yenyewe:
Kufanya ngono na msichana mdogo ni kosa la jinai. Hata kama alitaka mwenyewe bado ni kosa la jinai.
Kuandika vitisho kwenye SMS kwa mtu yeyote ni kosa la jinai, hata kama umekasirika namna gani


Mimi na wewe tukifanya makosa hayo tutakamatwa mara moja. Hebu ona wale waliofungwa juzi kwenye masuala ya pembe za ndovu. Sasa hawa wakubwa wao wataguswa. Sisi punda ni wakupondwa. Lakini inaonekana kwamba kuna dawa fulani wanayopewa vigogo inayowafanya wasiguswe. Daima ukitaka kuwashika, mikono inateleza, hata ulimi unateleza hadi wanadai ni mambo binafsi.
Ndiyo maana najiuliza kwa nini sisi waishiwa hatuwezi kufanya kitu. Kwa nini asasi zilizoshikia bango jambo hili kwa kudai mtuhumiwa ajiuzulu tu wasitangulie mahakamani na kufungua kesi ya madai kwanza? Kama ni suala binafsi, kwa nini tusifanye mashtaka binafsi hadi wale wenye nafasi waache ubinafsi wa nafsi zao na kukubali kwamba hili ni suala la jinai. Ni suala la kuhakikisha si tu kwamba haki itatendeka bali itaonekana wazi kwamba imetendeka.
Naam. Maana iwapo mashtaka haya si kweli, hata yule aliyetoa naye amefanya kosa la jinai, kumkashifu mtu tena kigogo kabisa. Wananchi tuna haki ya kujua ukweli. Tuna haki ya kudai ukweli ili tuweze kupima tufanye nini. Lakini mwisho wa yote, wakati umefika kuona kwamba unyanyasaji kijinsia si suala binafsi hata kidogo. Hebu tujiulize hata kwenye jamii zetu, kwa nini mwizi anakamatwa mara moja lakini mbakaji, fataki, mtongozaji wa mabinti wadogo hawakamatwi kabisa, eti wana dawa fulani inayofanya wasionekane. Si kweli. 

Ni kwamba tunafumbia macho makosa hayo, eti hatukubali kwamba kumwumiza msichana au mwanamke kimwili na kiakili ni uhalifu, kuharibu nafasi yake katika jamii ni uhalifu, kumpatia magonjwa ya mwili na akili ni uhalifu. Kumpiga mwenzio ndani ya nyumba na kusababisha majeraha na hata ulemavu ni uhalifu. Kwa nini hatukubali?
Hivyo ubinafsi wa wenye nafasi wasituvuruge. Wakati umefika kuona kwamba masuala haya ni masuala ya uhalifu. Lazima haki itendeke.


MWANANCHI JUMAPILI

No comments: