Friday, November 29, 2013

MAENDELEO YA MTWARA NA LINDI KUELEKEA 2015
 Na Baraka Mfunguo,

Kuna umuhimu mkubwa wa wadau wa mikoa ya Mtwara na Lindi kukusanya nguvu zao ili kuweza kuhakikisha matumizi bora ya rasilimali walizokuwa nazo kwa maendeleo ya mikoa ya Mtwara na Lindi. Hivyo basi ni vyema wadau waliopo Dar es Salaam wakaandaa chakula cha jioni na wakamwalika mtu mmoja mwenye ushawishi atokaye katika mikoa ya Lindi na Mtwara kwa ajili ya kujadiliana kuhusiana na mkakati wa maendeleo katika mikoa hiyo pamoja na changamoto zilizopo na namna ya kuzitatua changamoto hizo (Mgeni rasmi aweza akawa Mama Salma Kikwete).

Wadau wote wafanyabiashara, wanazuoni, wanasiasa, watu wenye nyadhifa mbalimbali serikalini pamoja na wale ambao wana dhamana katika taasisi za serikali  bila kujali itikadi zao wanapaswa kushiriki kwa ajili ya mustakabali wa mikoa yao. Muandae mkakati wa kuuza meza maalum kwa watu maarufu wenye mapenzi mema na mikoa ya Lindi na Mtwara (Mfano Mzee Sabodo) na wengineo wenye ushawishi, uwezo wa kuisaidia mikoa hii kwa ajili ya maendeleo ya Mtwara na Lindi pia mfanye Harambee ambayo kiasi kitakachopatikana kiandaliwe utaratibu maalum kwa ajili ya kuboresha maeneo ya Elimu, Afya na Kilimo . Natambua kila mkoa unaandaa taarifa na ripoti maalum za utendaji na utekelezaji wa maeneo ya kila sekta kwa kila mwaka lakini suala la kujiuliza hayo yanayoandikwa kwenye makabrasha hayo yameshirikisha wadau wa kada zote? Ni taarifa halisia? Na je kuna utaratibu wowote wa kujitazama na kujisahihisha? Ama ndio zile za zimamoto!  Rai yangu kwa wadau wote wa mikoa ya Mtwara na Lindi kuweka tofauti zao kando katika suala la maendeleo katika mikoa yao. TOFAUTI ZENU WEKENI KANDO!


MAENEO YANAYOTAKIWA KUANGALIWA

Kuanzisha mchakato wa kuanzisha Benki ya Korosho ama Korosho Bank. Benki hii iwe kwa ajili ya kukuza na kuimarisha wakulima wa zao la Korosho kwa kuwapatia mikopo nafuu itakayowawezesha pembejeo, zana muhimu pamoja na kuwawezesha katika utaratibu mzima wa masoko katika mazao hayo. Benki ije na mkakati wa kumaliza kabisa kadhia ya stakabadhi ghalani. Kwa kufanya hivi kutampa mkulima fursa na uhuru wa kupata  na kuvuna  kile alichokipanda kwa uhalali. Mathalan mkulima ana uwezo wa kulima Korosho na kupata kiasi cha shilingi Milioni 50 kwa mwaka Benki inaweza kumkopesha mkulima huyo akalima korosho zake zikampatia kiasi cha shilingi milioni 200 ama zaidi kutokana na juhudi zake na mkulima huyo akafanikiwa. Lakini si kufanikiwa tu, hata uchumi wa mikoa hii itakua na ajira kuongezeka. Malengo ya Benki ya Korosho yaweza kubadilika kadiri benki inavyokuwa na kuwasaidia wakulima wa mazao mengine na hata wafugaji.

Mfuko wa Maendeleo kwa ajili ya mikoa ya Lindi na Mtwara. Nafahamu inawezekana ikawepo mifuko ya aina hii lakini sina uhakika sana weledi wake, utendaji wake, usimamizi wake ama tathmini na taarifa zake na mifuko hii ni mali ya nani. Ila kimsingi mifuko hii inatumika ndivyo sivyo kwani inatumika kama NGO's feki na ngazi za wanasiasa kupata madaraka. Uanzishwe mfuko utakao simamia maendeleo kwa matakwa ya wananchi na si vinginevyo. Waajiriwe watu wenye ujuzi wa kubuni miradi, mikakati na namna ya kuweza kukusanya rasilimali  ambazo zitakwenda kuwasaidia wananchi na matokeo tuyaone taarifa  zipatikane kwa wakati na ikiwa kuna nia ya kuwawajibisha wahusika taratibu zifuatwe. Pia katika angalizo ni muhimu kwa wanasiasa kutotumia ushawishi wao ama kuingilia shughuli za Mfuko huu. Na pia ajira kwa ajili ya kuweza kuwapata wataalam wa kuweza kusimamia isiangalie ukabila ama rangi ama utaifa bali uwezo, mbinu na mikakati ya kuweza kufikia malengo ya maendeleo kwa ajili ya mkoa. Mfuko wa maendeleo ujikite katika Elimu, Afya, Kilimo, Huduma za kijamii na mkakati wa kumkomboa Mwanamke kuondokana na mtazamo potofu wa ndoa changa, imani potofu na udhalilishaji wa  kijinsia.

Suala la Uwekezaji katika Utalii. Mikoa ya Mtwara imejaliwa kuwa na vivutio vikubwa vya utalii lakini kwa bahati mbaya vivutio hivi havijatumika kwa ufanisi pengine ni kutokana na mtazamo ama serikali kutilia mkazo katika kuwekeza katika mikoa mingine. Sasa wakati umefika kwa mikoa hii kutambua maeneo "potential" kwa ajili ya kuvutia watalii na wawekezaji wahimizwe kuja kuwekeza katika utalii kwa ujenzi wa mahoteli, nyumba za wageni na serikali kuweka utaratibu wa kuainisha maeneo tengefu na kuweka mikakati shirikishi kwa kutoa mafunzo kwa wazawa juu ya suala la vivutio vya utalii na namna ya kuweza kuwavuta wawekezaji na watalii kutoka nje. Kubwa mkazo uwekwe kwenye Lugha na utaratibu wa kuwajali wateje watu waachane na atttitude ya kizamani ya masikini jeuri. Mteja ni mfalme na hii itawafanya watu wavutike zaidi na kuondoa tofauti kati ya Kusini na Kaskazini. Naamini Inawezekana. Mafunzo yanayotolewa ni yale ya Hotel Management, Food and Beverages lakini kwenye suala la utalii na vivutio na kutangaza na masuala mengine ya PR"Public Relations" bado.

Uwekezaji katika viwanda vidogo vidogo. Natambua mchango mkubwa wa SIDO hilo halina ubishi. Umefika wakati sasa wa wananchi kwa kuitumia nafasi hiyo na kwa kupitia kuanzishwa kwa benki kama ya Korosho Watu wataweza kupata fursa zitakazoweza kuwasaidia. Viwanda vidogo vidogo katika maeneo ya Vinyago Mtwara inasifika sana kwa sanaa ya uchongaji vinyago na kwa bahati mbaya wanaofaidika na bishara hii sio wachongaji wenyewe bali wachuuzi tena wa nchi jirani. Hili linahitaji kukomeshwa kwa kupatiwa ufumbuzi. Uwekezaji katika kutengeneza vifaa mbalimbali vya sanaa mfano ngoma, Uwekezaji katika viwanda vya matunda, Uwekezaji katika kilimo cha mbogamboga na matunda kwa kutumia mfumo wa "Green Housing" ambao una ufanisi mkubwa, uwekezaji katika uzalishaji wa kuku wa aina mbalimbali, Uwekezaji katika kutengeneza vitu vinavyotokana na mazao ambayo yameonekana hayahitajiki mfano vifuu vya nazi, mfano mabibo ya Korosho na maganda ya korosho. Kuna msemo usemao" nothing is waste" yaani hakuna uchafu inatokana na namna unavyouchukulia lakini lau ungegundua faida zake usingechukulia uchafu kamwe. Mafunzo yatolewe na watu watumie fursa hizo na sio kulalamika kila siku.

Suala la Gesi - Imekuwa ni wimbo wa kisiasa kuhusiana na suala la gesi lakini gesi hii itamfaidia nani bado ni kitendawili. Kitendawili ambacho si mwanasiasa ama mwananchi wa kawaida aweza kukitengua. Jitihada za kulitatua suala hili zinahitajika kabla mambo hayajawa mabaya zaidi. Siasa ziwekwe pembeni, Itikadi pembeni na mitizamo iwekwe pembeni ni lazima muafaka wa suala hili ufikiwe na mwananchi atambue atafaidika kwa namna gani kwa fursa itakayojitokeza ama zitakazojitokeza kwa kuwezeshwa na kupewa kipaumbele sio wanasiasa kuzitaja fursa hizo kwa wananchi na wanaofaidika ni wengine. Mkazo uwekwe kwenye elimu na matokeo yaonekane. Sio kuwachukua watu "influential " waliokuwa wakidai gesi kwanza na kuwapa mamilioni ya pesa na kuwatishia na kuwageuza mapandikizi. Suala hilo ni la muda mfupi tu. 

Kwa kuongezea katika suala hili la gesi na nishati, tukumbuke pia katika mkoa wa Lindi kuna machimbo ya Bauxite na Dhahabu katika Wilaya na Nachingwea lakini pia Nickel na madini mengine yanapatikana tuzitumie rasilimali hizo na tuweke mikakati ya kuzitumia vyema kwa manufaa ya wazawa wa eneo husika kabla hatujajutia kama wengine.

Utitiri wa wanaojiita wawekezaji ambao wananunua na kuhodhi maeneo makubwa ya ardhi bila ya kuyatumia. Kumekuwa na utitiri mkubwa wa wanaojiita  wawekezaji wa ndani na nje ambao wanajitwalia maeneo makubwa ya ardhi na kuyaacha bila ya kuyaendeleza. Watu hawa wana uwezo mkubwa kifedha na wamekuwa wakiwahonga watendaji mbalimbali serikalini ili kufanikisha adhima yao. Ili linatakiwa kupatiwa ufumbuzi .

Ujenzi wa Reli kutoka Liganga, Mchuchuma hadi Mtwara suala hili limeainishwa vyema katika mkakati maalum wa "Southern corridor" na haieleweki mradi huu utaanza  lini. Tunafurahi hatua ya Mh. Rais wa kuifufua Reli ya kati lakini tunaona ni vyema pia suala hili likapata kipaumbele chake kutokana na umuhimu wake wa kuifungua mikoa yote ya kusini na kuiunganisha na nchi jirani isije ikawa "timing na matrix" zikawa "overlooked " kabla ya kutoa maamuzi ni lazima matriksia ifanyike ambayo itatoa tathmini ya umuhimu na faida za mradi kwa nchi. Kwa mtazamo wangu Mradi huu wa reli utaleta faida kubwa sana. 

Ujenzi wa hospitali ya rufaa. Tunatambua kwamba eneo limeshatengwa serikali iweke mikakati ya kuwezesha ujenzi wa haraka wa hospitali hii. Serikali kupitia Wizara ikipandishe hadhi Chuo cha Maafisa Tabibu cha COTC kwenda kuwa chuo kikuu cha Tiba na uuguzi. Jitihada za serikali zimeonekana kwa kuongeza rasilimali na kupanda kuwa chuo kinachotoa Advance diploma in Medicine. Tunadhani kwa utaratibu huo huo Chuo hiki kitoe pia digrii ya Tiba ili watakaofaidika kupata elimu ya chuo hiki wakawe Madaktari. Mkakati ufanyike ili elimu itolewe kwa ajili ya Madaktari bingwa. Vile vile kulikuwa na mkakati wa ujenzi wa chuo cha uuguzi maeneo jirani na chuo cha COTC, jitihada na ufuatiliaji ufanyike ili chuo hicho kijengwa haraka iwezekanavyo. Ni miaka takriban mitano ujenzi wa chuo hicho umesimama.

Suala la Elimu. Mikoa ya Mtwara  na Lindi imekuwa ikidorora kielimu kila kukicha suala hili linatakiwa lipatiwe ufumbuzi. Wapo ambao wamepewa dhamana ya kusimamia Elimu na wanatambua fika kwamba wao ni wazawa wa mikoa hii, watambue kwamba jamii itakuja kuwasuta siku moja na wala sio mbali. Changamoto zilizopo katika sekta ya Elimu ni Ukosefu wa waalimu waliobobea, Ukosefu wa vifaa kama vile vitabu, maabara za kusomea na pia suala la mtazamo hasi wa baadhi ya watu juu ya Elimu. Waziri Mkuu ameainisha juu ya Watendaji kujenga Maktaba za Wilaya nchini Tanzania, nadhani mkakati huo ungeanzia mikoa ya Mtwara  na Lindi. Tuna vyuo mbalimbali vinavyotoa mafunzo ya Ualimu kuanzia ngazi ya cheti mpaka stashahada na asilimia kubwa huenda kufanya mafunzo ya vitendo katika mashule mbalimbali katika mikoa ya Mtwara na Lindi. Mkakati uwekwe ili kuwawezesha walimu hawa kubaki katika mashule hayo. Mikakati hiyo ni kama malazi ya bure kwa walimu pamoja na posho mbalimbali za kujikimu, na pia mikakati mbalimbali ya kuwahamasisha ili waweze kuipenda kazi yao. Mfano Uwezo wa kupunguziwa gharama za usafiri kwa ndege kama ilivyokuwa enzi za Mwalimu na miakati mingine mingi. 

Kuelekea uchaguzi mkuu 2015. Ni vyema wadau wa mikoa ya Mtwara na Lindi wakaweka mikakati ya kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2015. Ni vizuri wale waliopewa dhamana wakajitathmini mazuri yao na mapungufu yao katika dhamira zao kabla ya kuamua ama kugombea ama kutokugombea. Kila mhusika atatakiwa aainishe kwa ufupi maeneo aliyofanikiwa pamoja na changamoto binafsi pamoja na zile za ujumla ambazo zitapatiwa ufumbuzi. Kuhusiana na changamoto binafsi ni vyema wanasiasa husika wakatoa tathmini ya nini kilichowakwamisha ili hatua zichukuliwe dhidi ya waliokwamisha ama dhidi yao wenyewe kwa uzembe wao.

Ujenzi wa Vivuko kwa mikoa ya Mtwara na Lindi. Serikali imeanza kuonyesha jitihada za ujenzi wa kivuko cha kivuko maeneo ya kutoka Mtwara kuelekea Msanga mkuu. Ni vyema pia wakaangalia na vivuko vingine vilivyoko mpakani wa Tanzania na Msumbiji ambavyo kama vitaweza kutengenezwa vitaweza kufungua fursa kubwa ya kibiashara kati ya Tanzania na Msumbiji.

Mkakati wa kuwawezesha wakina mama wauza samaki. Kila siku mfano Mtwara wakina mama wamekuwa wakipita na mabeseni yao ya kuuza samaki wakienda na kutoka ferry. Biashara hii ni nzuri lakini ili iweze kuleta faida yahitaji kuendelezwa na kukuzwa kwa kuweka miundo mbinu mizuri ya kuweza kuwasaidia si hao akina mama pekee, bali hata na wavuvi. Kijengwe kiwanda kitakachojihusisha na utengenezaji wa minofu ya samaki na majiko na mwalo mkubwa ujengwe kwa ajili ya biashara hiyo. Jitihada zimeonekana ila Wanawake hawa wanahitaji kuwezeshwa kwa namna moja ama nyingine.

Mwisho masuala ya Ulinzi na Usalama. Suala la ulinzi na usalama ni muhimu katika kudumisha amani na endapo amani inatoweka katika sehemu husika basi shughuli na utendaji wa kila siku ama huyumba na kusimama kabisa. Suala la ulinzi na usalama si jukumu la Polisi ama Mwanajeshi bali ni jukumu la kila mmoja wetu. Isipokuwa kila mtu ana mipaka ya wajibu wake. Sasa hivi imejitokeza dhana ya Vyombo vya ulinzi na Usalama kutumika kama wanasesere wa wanasiasa na kuwaacha waliowapa dhamana kama watoto wakiwa. Iwekwe mikakati ya kuwaweka karibu wananchi na wenye dhamana ya vyombo hivi. Naweza kuona jitihada za IGP Mwema nadhani hizi ni jitihada za kisayansi zinatakiwa ziende zaidi ya hapo ili imani iweze kujengeka miongoni mwa wananchi. Ili kutibu majeraha ya vugu vugu la gesi na mambo mengine utaratibu huu ni vizuri ungetumika na miradi mbalimbali iletwe mikoa ya Mtwara na Lindi ambayo itawawezesha wananchi kushiriki katika zoezi la ulinzi na usalama katika nchi yao.

No comments: