Wednesday, October 23, 2013

ZANZIBAR HAIPIKI,HAIPAKUI,INASUBIRI KULETEWA.Zanzibar.  Kwa muundo wa Muungano wa Serikali mbili Zanzibar haipiki wala haipakui, yenyewe inasubiri ukumbuni kitakachopikwa ndicho itakachokula.

Hii ndio falsafa ya baadhi ya wanasiasa Zanzibar ambao kwa hofu tu ya kupoteza ulwa wanajiweka katika nafasi ya ‘mgeni mwalikwa’ wakati yenyewe ndio mwenye shughuli. 

Zanzibar kwa asili yake, kwa maumbile yake haistahiki kuwa ilivyo, haifurahishi kuona inapoteza mila, silka, utamaduni wala historia yake iliyotukuka.

 Cha ajabu leo miaka 49 ya Muungano, kuelekea jubilee ya miaka hamsini mwakani, umaarufu wa Zanzibar unazikwa na wanasiasa wa kambi ya kihafidhina kwa kisingizio cha kupambana na wapinga mapinduzi!

 Ni ukweli uliowazi kwamba Wazanzibari wengi wanauona mfumo wa serikali mbili kama ni jakamoyo, wanajiuliza kwani wao wana nafasi gani katika Muungano huu?

Je wamenufaika vipi na ushirikiano huu wa kisiasa kwa miaka 49 au ndio maneno yale yale ya udugu na historia ambayo hayawezi kufutika.

Nani aliyepoteza au kunufaika katika maumbile ya sasa ya Muungano – Tanganyika au Zanzibar? Kwa haraka haraka naweza kusema ni Zanzibar iliyopoteza kila kitu. Imepoteza nguvu za nchi, imepoteza mamlaka yake sio tu ya kimataifa bali hata ya ndani maana kuna mambo mpaka ‘kaka mkubwa’ atake, apendezwe na jambo fulani.

Kiti kinachokaliwa na Balozi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Umoja wa Mataifa ni cha Tanganyika iliyojiunga na UN Desemba 14 mwaka 1961, kilichohaulishwa kwa Muungano na si cha Zanzibar iliyojiunga na UN Desemba 16, mwaka 1963.


Kumbukumbu za maandishi ya Umoja wa Mataifa zinaonesha kwamba Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilijiunga na UN siku ambayo Tanganyika ilijiunga na umoja huo, jawabu unayo mwenyewe.

Tukiwa na mfumo wa muundo wa Muungano ambao utaifanya Zanzibar na Tanganyika kujiunga na mashirika na taasisi za kimataifa kama UN, ICC, WTO, IMF, WB na mengine bila shaka utatuondoshea jakamoyo walilonalo wananchi.

Mara baada ya mapinduzi ya Januari 12 mwaka 1964, Zanzibar ilianza kazi ya kujenga uchumi madhubuti, wakoloni wakibezwa, ari ya kujitawala ilikuwa kubwa, maadui watatu wakatangazwa – umaskini, ujinga na maradhi.

Tumekuwa tukijiuliza Zanzibar ina nafasi gani, ubavu gani wa kupambana na maadui hao ambao kwa maumbile, hulka zao wanahitaji kushughulikiwa kwa kiasi kikubwa na mashirika kama Benki ya Dunia, Umoja wa Mataifa, Shirika la Fedha Duniani, Shirika la Sayansi, elimu na utamaduni na Shirika la Afya ulimwenguni.

Waziri wa Afya wa Zanzibar pamoja na ukakamavu, uhodari wake hawezi kutia saini mkataba wa kimataifa bila ya kuomba ruhusa wala kupata kibali cha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe.
Kibali chenyewe inategemea na siku yenyewe, akiamka na mazonge ya Jimbo la Mtama, itabidi usubiri maana hakuna nguvu za kisheria za kumshurutisha kutekeleza suala hilo, huku wananchi wako wa Mtende, Kitope, Pongwe wakisubiri kuona utekelezaji wa ilani ya uchaguzi uliyoinadi.
Kwa sababu ya umaskini uliokothiri, wananchi wengi hawapati chakula bora na kwa hivyo, utapiamlo nao ni tatizo kubwa hapa Zanzibar, hasa kwa shamba nyingi za hapa Zanzibar ambapo kikawaida chakula chao ni cha aina moja tu kila uchao kwa sababu ya kutokuwa na kipato cha fedha cha kutosha. 
 Tatizo la ajira ni maumivu mengine hasa kwa vijana ambao licha ya kupata elimu kwa mazabe mazabe, mashaka, lakini wamalizapo mafunzo yao wanaselelea vijiweni kuhesabu ndege zituazo na zinazo paa pale Kisauni.
Maisha ya Wazanzibari wengi ni magumu, lakini kwa sehemu za mashamba maisha yanakuwa magumu zaidi na kwa hivyo idadi kubwa ya watoto wanaomaliza masomo darasa la kumi hulazimika kukimbilia mjini Unguja ambako nako pia hakuna ajira na kusababisha ongezeko la idadi ya watoto wa mitaani na wazururaji katika Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja.
Tunaambiwa takwimu za sense ya watu na makazi iliyofanyika mwaka 2012 Mkoa  wa  Mjini Magharibi Unguja una watu 593,678 sawa na asilimia 46 ya watu wote wa Zanzibar.
Idadi ya watu Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeongezeka zaidi ya mara tatu kutoka watu milioni 12.3 mwaka 1967 hadi watu milioni 44.9 mwaka 2012. Kati yao 43,625,354 wapo Tanzania Bara na 1,303,569 wapo Tanzania Zanzibar.
Tunaambiwa kuwa taarifa za Sensa ya mwaka 2012 zitatumika kutathmini Dira ya Maendeleo ya Mwaka 2025 kwa Tanzania Bara na Dira ya Maendeleo ya Mwaka 2020 ya Zanzibar.
Pia, itatumika kutathmini Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2011/12 – 2015/16, Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini (Mkukuta) kwa Tanzania Bara (Tanganyika) na Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini Zanzibar (Mkuza) pamoja na Malengo ya Milenia ya Mwaka 2015.
Je, Zanzibar imetimiza vipi vigezo vya malengo ya milenia 2015 ilhali ikiwa ni ‘mgeni mwalikwa’ kwenye ukumbi unaopanga masuala hayo?
Kwanini hatufikiri kwa makini zaidi kutanguliza maslahi ya umma mbele, hasa tukitazama ongezeko la watu mwaka 1967 na mwaka 2012 kuwa kunahitajika mabadiliko ya mfumo wa muundo wa Muungano kwa kuwa mahitaji ya watu yameongezeka?
Ongezeko la vibaka, wezi na kukithiri kwa vitendo vya baadhi ya wanawake kujiuza mijini ni ushahidi wa kuporomoka kwa maadili, lakini kwa kiwango kikubwa hali hiyo inasababishwa pia na umaskini uliokithiri katika jamii.  

Na jambo hili ni hatari kwa amani na utulivu wa nchi yetu.  Bado Wazanzibari wanaishi chini ya mstari mwekundu wa umaskini huku wakitegemea pato la chini ya dola moja.
Jamani, wakati umefika kuchagua historia nzuri ya nchi yetu, tuacheni ubabaishaji, undumilakuwili na upopo wa leo kuwa ndege, kesho mnyama. Tuchague historia bora kwa maisha yetu.


MWANANCHI

No comments: