Friday, October 18, 2013

TUSIMAMIE MALENGO YA NYERERE KUJENGA TAIFA LA HAKI, HESHIMA.
Mwalimu Julius Nyerere akimpa moja ya nyaraka za kiserikali, Rais wa kwanza wa Zanzibar, Abeid Aman Karume.

 Na Ibrahim Kaduma,

Tunaposema tunamkumbuka Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere sharti iwe ni kwa lengo la kulinda, kudumisha na kuimarisha uhuru wetu na kujenga heshima ya Taifa letu. Viginevyo tutakuwa tunamdhihaki jambo ambalo litatuletea laana.
Hivyo, kwa maoni yangu, kumbukumbu zetu ziwe zaidi ni zile zinazolenga kumuenzi Mwalimu kwa misingi mizuri ya utawala bora aliyotuwekea ili iwe shule kwa vizazi vipya katika kuweka sera za maendeleo ya nchi yetu.
Kwa msingi huo, ninayo furaha na heshima kuwakumbusha Watanzania wenzangu na hata watu wa mataifa mengine malengo makuu yaliyowekwa na Mwalimu Nyerere kwa ajili ya kujenga taifa linalosimamia haki na kujijengea heshima mbele ya mataifa mengine ambayo ni:-
•Kujenga nchi ya watu huru na sawa; watu ambao wana fursa sawa katika jamii na ambao mapato yao hayapishani sana.
•Kujenga nchi ya watu huru na ambao wanajitegemea. Mwalimu Nyerere alilenga kuliondolea Taifa hili na watu wake tabia ya kuombaomba kwa sababu alijua kwamba kwa kufanya hivyo tunalidhalilisha taifa.
•Kujenga nchi ya watu huru na wanaotawala uchumi wao wenyewe. Kwa kutambua rasilimali nyingi ambazo taifa hili linazo, aliamini kwamba tukiwa na uzalendo wa kutosha tutaweza kuzivuna na kulitajirisha taifa hili ama sisi wenyewe au kwa kushirikiana na wageni lakini sisi tukiwa na kauli kubwa zaidi. Kwa njia hiyo tutaweza kutimiza lengo letu la kwanza na la pili.
•Ili hayo malengo matatu yafikiwe, alidhamiria kujenga taifa la watu huru na wanaongozwa na viongozi bora kwa maana ya viongozi waaminifu na waadilifu; viongozi wasio wabinafsi bali wanaoamini katika kuwatumikia wananchi kwa faida yetu wote; viongozi ambao wako tayari kujitoa mhanga kwa faida ya wanyonge na taifa zima kwa jumla. Hivyo ndivyo alivyokuwa yeye mwenyewe – yaani kiongozi mwenye uzalendo wa hali ya juu sana na anayesimamia haki ya Mungu.
Sifa hizi ni za viongozi waliokombolewa kifikra na kuwekwa huru; viongozi wanaomcha, kumwogopa na kutafuta kumtii Mungu katika maamuzi na utendaji wa kazi zao.
Hawa ni viongozi wanaotambua kuwa Mungu hawezi kufichwa jambo lolote hata kama ni katika mawazo tu; viongozi ambao wanaheshimu mamlaka zilizopo lakini hawaziogopi; yaani viongozi walio tayari kukosoa na kukosolewa. Ni kutokana na msingi huu, Mwalimu Nyerere aliandika kitabu kijulikanacho kama “TUJISAHIHISHE”.
Hii ni tabia ya mtu aliye tayari kukiri makosa yake na kubadilika kuwa mtu mwema; jambo linalomfurahisha sana Mwenyezi Mungu. Ndio maana mara tu baada ya Uhuru, Mwalimu Nyerere alitamka katika Bunge tarehe 28/06/62 kwamba “hatimaye kinga ya haki za wananchi, uhuru wa wananchi na vitu vyote wanavyovithamini, hatimaye kinga yake ni maadili ya Taifa”.
Waliongeza kusema kwamba “Kama taifa halina maadili yatakayoiwezesha Serikali kusema ‘Hili hatuwezi kulifanya kwa sababu si u-Tanganyika’; Au wananchi kusema ‘Lile hatuwezi kulivumilia kwa maana lile si u-Tanganyika’ kama wananchi hawana maadili ya jinsi hiyo, haijalishi mnaandika Katiba ya jinsi gani…siku zote watakuwa watumwa wa maonevu” (Uhuru na Umoja, uk. 174).
Maneno haya aliyatamka kwenye kikao cha Bunge ambalo lilikuwa likiujadili Mswada wa kuandika Katiba Mpya ya kuigeuza Tanganyika kuwa Jamhuri.

Kumbukumbu hii inatoka katika muda mwafaka; muda ambao Watanzania tuko katika harakati za kuandika Katiba Mpya ya Jamhuri yetu. Malengo hayo manne aliyoyaweka Mwalimu Nyerere hapo juu, ndiyo kipimo cha “u-Tanganyika au u-Tanzania”.
Basi, hivyo ndivyo watu waliokombolewa kifikra na wanaoenzi mafundisho ya Mwalimu Nyerere yaliyotutaka, tuwaheshimu na kuwatumikia watu wote bila ubaguzi wa aina yoyote; pia kujitolea nafsi zetu ili kuondoa umaskini, ujinga, magonjwa na dhuluma; wanatakiwa kuenenda.
Mipango yetu tuichangamkie kama inalenga kutekeleza malengo hayo. Kinyume cha hayo, lazima tukemee tukitoa sababu zetu za kufanya hivyo. Kwa kufanya hivyo ndipo tutaweza kuulinda, kuudumisha na kuuimarisha uhuru wetu. Aidha, hivyo ndivyo tutaweza kudumisha upendo, mshikamano na amani katika nchi yetu. Ni vyema Katiba yetu ikazingatia misingi hiyo. 

Vyombo vyetu vya habari, kama mhimili wa nne wa uongozi wetu vitatusaidia sana kama vitaipigia debe misingi hii ya utaifa wetu. UHURU NA UMOJA; UHURU NA AMANI; A LUTA CONTINUA.
Ibrahim M. Kaduma ni mwanasiasa mkongwe aliyewahi kushika nafasi mbalimbali za juu serikalini.MWANANCHI

No comments: