Monday, October 21, 2013

MTAMA WA BABA NI NINI? MTAMA WA BABA WALIWA.
"  We are in favour of a democratic republic as the best form of state for the proletariat under capitalism. But we have no right to forget that wage slavery is the lot of the people  even in the most democratic bourgeois republic. Furthermore, every state is a "special force" for the suppression of the oppressed class. Consequently, every state is not "free" " and not a people's state"  "

 (Lenin, V.I (1963), Selected Works, State and Revolution, PG 251, Progress Publishers, Moscow). Na Baraka Mfunguo,

Ni majira ya saa tatu asubuhi mwaka wa 1984 naamka taratibu na kujikongoja kitoto mpaka sebuleni na ninafungulia redio ya R.T.D nasikiliza kipindi cha "Tuimbe Sote". Kipindi cha Tuimbe sote kilikuwa ni mkusanyiko na mjumuiko  wa vikundi mbali mbali vya kwaya nchini Tanzania (wakati huo) vilivyopeleka kazi zao R.T.D na maudhui yake yalilenga kuelimisha, kuonya, kuburudisha, kuweka utayari wa wananchi "self awareness" lakini kikubwa kilikuwa ni utajiri wa utamaduni wetu kama Watanzania wasio na misingi iliyofungamana kidini, kikabila, kikanda ama kibara na visiwani. Hivi leo nadhani limebaki kundi moja la kwaya ambalo linafanya kazi ya kusifia , kuabudu na kusujudia chama tawala na mfumo wake huku likisahau ama kufumbia macho masuala mengi ya msingi.

Kwaya iliendelea kuimba huku kibwagizo kikiwa " Mtama wa baba ni nini?, Mtama wa baba waliwa" Niliendelea kusikiliza kwa makini na shauku kutokana na upeo wangu wa kitoto wa kutoweza kuling'a,mua fumbo lile mpaka mwisho wa wimbo ambapo waimbaji wanatanabaisha kwamba " Mtama wa baba ni mali ya umma". Ghafla macho yanafunguka ama! Kumbe mtama wa baba ni mali ya umma.

Zamani na mpaka sasa mtama ni zao muhimu sana ni zao linalostahimili ukame na ni zao ambalo ni chakula kizuri kwani waweza kupata ugali wa mtama, uji wa mtama, wali wa mtama na hata togwa linalotokana  na mtama. Pia mtama ni chakula kinachopendwa sana na ndege wa aina karibia zote. Hivyo huwalazimu wakulima kulinda mashamba yao ili mtama usiliwe na ndege. Hivyo  mtama ni zao muhimu sana na linaloheshimika kwani liliweza kupambana na njaa ipasavyo. Mkulima asipokuwa makini, mtama wake waweza kuliwa na kumalizwa na ndege hata asipate chakula cha kuweza kuilisha familia yake, mbegu za kupanda na kile kitakachohifadhiwa katika ghala.

 Dhana nzima na maudhui ya wimbo huu " Mtama wa baba ni nini?, Mtama wa baba waliwa", imejikita katika ubadhirifu wa rasilimali za umma unaotokana na ukwasi, ubinafsi, tamaa za viongozi ambao wamepewa dhamana na wananchi. Wananchi wameweka matarakio kama alivyo mkulima anayehifadhi mbegu zake ili akazipande shambani ili avune mazao kwa ufanisi. Matokeo yake mazao yake kuliwa na ndege. Wananchi ama mwananchi wa kawaida ni rasilimali na anawajibika kwa serikali  katika uzalishaji mali ili kukuza uchumi na kuongeza kipato, kulipa kodi , kushiriki katika maamuzi kuanzia ngazi ya shina, kutiii na kuheshimu sheria pamoja na mamlaka zinazotambulika. Haya yanatekelezeka kwa miadi ya viongozi kutimiza wajibu wao. Matokeo yake ni viongozi kushindwa kutimiza wajibu wao kwa njia ya tamaa zao kwa kujilimbikizia  posho kubwa, mishahara minono isiyoendana na uhalisia wake, maisha  ya kifahari na anasa ambayo yanatokana na kodi za wananchi huku mambo ya msingi mfano huduma za kijamii kama vile afya, elimu, haki za msingi anazostahili raia zikihodhiwa na viongozi wenyewe. "Mtama wa baba ni nini?, Mtama wa baba waliwa".

Masuala mbalimbali ya utendaji ya serikali kufanywa kama masuala binafsi na ya kifamilia. Na kupelekea wananchi wa kawaida kukosa hata fursa. Hata kama mwananchi huyo wa kawaida atakuwa na kipaji cha hali ya juu . Haki zake zitahodhiwa na kufanywa kama mali ya kiongozi fulani ama kipaji hicho kitatafsirika na kumhusisha mtu anayehusiana na kiongozi "Mtama wa baba ni nini?, Mtama wa baba waliwa"

Tukiwa tunaelekea uchaguzi mkuu mwaka 2015, takriban miaka 10 kashfa za EPA, Meremeta, Tangold, Richmond na Rada zimeunguruma masikioni mwetu zikikaribua kupasua ngoma na sasa kashfa ya mabilioni ya Uswizi haina majibu. Pamoja na kupigwa kelele kwa kashfa hizo, kiasi cha fedha kilichochotwa hakijarejeshwa kwa asilimia 100% serikalini na wahusika wakuu hawajatiwa hatiani. "Mtama wa baba ni nini? Mtama wa baba waliwa"

Uharamia baharini, Nyara za serikali kama vile pembe za ndovu, pembe za faru, ngozi za chui, simba na wizi wa wanyama wa mwituni wakisafirishwa mchana kweupee huku viongozi wa serikali wakijifanya  ama hawaoni na kutokujua na kupelekea kuunda tume zisizokuwa na tija na wasio hatia kutolewa kafara kwa kisingizio cha uzembe. Turejee kashfa ya Loliondo iliyoutoa uhai wa Katabalo.
"Mtama wa baba ni nini? Mtama wa baba waliwa".

Viongozi wa serikali kupenyeza mianya ya kisiasa katika dini na kupelekea ufa mkubwa unaohatarisha amani ya nchi. Huku viongozi wengine wa kisiasa wakijitapa katika sehemu za ibada kwa kuendekeza udini wao. "Mtama wa baba ni nini? Mtama wa baba waliwa"

Migogoro ya wakulima na wafugaji inayogharamiwa na kufadhiliwa na wanasiasa ambao wanafaidika na biashara ya mifugo na wengine wanafaidika na mashamba wakiwatumia wakulima na wafugaji kama chambo ili kufikisha  ujumbe wao kwa serikali. "Mtama wa baba ni nini? Mtama wa baba waliwa"

Serikali kuwabana wakulima kutokuuza mazao yao nje na kuwaruhusu wafanyabiashara kuagiza mazao na kuyauza  kwa bei inayopishana na soko la ndani na kupelekea mkulima kukosa soko la mazao yake na hivyo kuyauza kwa hasara na kuua uchumi wa nchi kwa kupoteza kodi. "Mtama wa baba ni nini? Mtama wa baba waliwa"

Kumomonyoka kwa maadili ya uongozi, Utumishi wa umma. Kwa viongozi kuendekeza rushwa, upendeleo wa makusudi, rushwa ya ngono, ubadhirifu na ubinafsi. Hali hii imepelekea hata kuweka maslahi binafsi katika kandarasi mbalimbali ama utaratibu wa kupata kandarasi mbalimbali kutoka serikalini.. Leo hii hata ukiwa mjasiriamali wa aina gani ni lazima utoe walau asilimia kidogo ili upate kandarasi ama uingie ubia na watendaji ili kinachopatikana kigawiwe nusu kwa nusu. Na hutashangaa sana kuwapo utitiri wa wafanyabiashara katika siasa. Kubwa na baya zaidi ni ile kauli ya "Usipokuwa tayari kuliwa nawe huli" kauli inayouhalalisha wizi na ubadhirifu wa mali ya umma kupitia rushwa. "Mtama wa baba ni nini? Mtama wa baba waliwa"

Tumeshuhudia kifo cha mashirika ya umma na yaliyobakia, yanasuasua ama yako mahututi yote hii ni matokeo ya kuendekeza siasa badala ya kazi, siasa badala ya weledi na kupelekea kupoteza dira, ubunifu, malengo na stratejia. Mashirika ya umma, kabla ya mfumo wa vyama vingi yalikuwa na utaratibu wa kuwapo kwa tawi la CCM ambapo alikuwapo mwambata wa chama ama Kada ambaye alisaidia kuainisha misingi ya chama ama aidiolojia iliyorandana ama kushabihiana na kuchapa kazi kwa malengo ili kukuza uchumi wa nchi na serikali yake.  Leo hii baada ya kupiga marufuku siasa maofisini, kila mtu ni mwanasiasa, kila mtu ni mjuaji, kila mtu ana ndoto ya kuwa mbunge baada ya kufilisi maana amewaona wakubwa zake wako katika mkondo huo huo tena kwa chama tawala na wanapita kwa kupitia rushwa wasivyo na haya. Ni wanasiasa hawa hawa leo wanaoenziwa waliofilisi mashirika kufikia wafanyakazi wa kawaida wa kima cha chini wasio hatia kupigwa ridandansi. Hakuna atakayesahau kadhia ya ridandansi katika hii nchi watu kupoteza ajira zao, mateso kwa familia zao na watoto kukosa huduma za msingi na kuwa wa mitaani. Haya ni matokeo ya kuendekeza siasa badala ya kazi kunakoendekezwa na viongozi wetu hata uteuzi wa watendaji hauzingatii vigezo bali siasa yatangulizwa mbele. "Mtama wa baba ni nini? Mtama wa baba waliwa"

Wafanyabiashara wa usafirishaji kuivimbia serikali kwa ongezeko la tozo la asilimia  5% la kodi ya mizigo katika mizani za wakala wa barabara ni matokeo ya ulafi wa serikali ambao ni matokeo yake ya kuua mfumo mzima wa reli. Kuanzia reli ya kati, reli ya Tanga, Moshi , Arusha na reli ya Tazara. Hii imetokana na nadharia hila "conspiracy theories" baina ya watendaji wa mashirika ya reli wanasiasa kwa kushirikiana na wafanyabiashara na serikali ikakazania ujenzi wa barabara pekee na wanasiasa kutumia kama ngazi ya kujipatia umaarufu na matokeo yake uchumi wa nchi unadumaa kwa kukosa mapato yatokanayo na uchukuzi. Nchi ambazo hazina bahati ya kuwa na bahari kwa ajili ya kufanikisha usafirishaji na uchukuzi wa bidhaaa zao nchi za mbalimbali za kigeni zingeweza kuunganishwa vizuri kwa kupitia mfumo wa reli. "Mtama wa baba ni nini? Mtama wa baba waliwa"

Ulanguzi, uhujumu uchumi kwa kuua mazao ya biashara mathalan Pamba, Pareto, Kahawa, Korosho, Mawese, Katani na tumbaku. Hii inaanzia vyama vya ushirika vya msingi mpaka taasisi mbalimbali zinazotokana na mazao hayo mfano bodi mbalimbali ambazo zimeweka urasimu wa makusudi na utaratibu ambao si rafiki kwa mzalishaji ama mkulima. Leo hii kwa mfano hata tufaa"Apple" linaagizwa kutoka Afrika ya Kusini, Shayiri ya ngano kwa ajili ya kimea cha pombe inaagizwa Afrika ya Kusini, nguzo za umeme Afrika ya Kusini, Karatasi Afrika ya Kusini. Viwanda ambavyo vingetakiwa kutumika kuzalisha bidhaa zinazotokana na mazao mbalimbali ya chakula na biashara vimegeuzwa kuwa maghala, mapagala ya wanyang'anyi na wahuni. Bado Serikali inakaa na kujaribu kutafuta mwarobaini wa kupambana na omba omba mijini, watoto wa mitaani, uchangudoa , utapeli na ujambazi. "Mtama wa baba ni nini? Mtama wa baba waliwa"

Gesi ya Mtwara, Madini ya Tanzania, rasilimali za Tanzania zinapigwa mnada kwenye masoko ya hisa Ulaya kwa bei ya kutupa kupitia uwekezaji huku Watanzania na waliomo pembezoni mwa amali hiyo waking'aa macho na mabwanyenye wakipita na magari yao sigareti mdomoni wakiwatimulia vumbi. Na ukasema upite njia hata pembezoni jirani mwa uzio wa mwekezaji unapigwa risasi na makorokoro wao. Ukenda kudai haki yako unaambiwa si haki yako, umevunja sheria , shauri lako, Umejitakia mwenyewe. Katika nchi yako. Unadhani tuko huru? "Mtama wa baba ni nini? Mtama wa baba waliwa"

Kuvuja kwa mitihani ya taifa, siasa na udini kujipenyeza katika elimu inayopelekea uvunjifu wa amani. Nani atakayesahau mlolongo wa uchomwaji shule moto miaka ya tisini? Elimu ya Tanzania kushuka, vipaji vya vijana kufa. Ukitafuta ajira unaambiwa huna vigezo kwa sababu hujakidhi ushindani wa soko kutokana na elimu yako. Wanaokuambia ni wanasiasa uliowapa dhamana . Wanakuambia hivyo wakijua watoto wao wako Ulaya wanasoma ili waje kushikilia vitengo, ili watutawale na kutuzimia sigara kwenye paji za nyuso zetu. Tukiwa katika hali ya kukatishwa tamaa tunaamua kukimbilia na kubahatisha kubanana kwenye bongofleva, kucheza sinema, kucheza ngoma na ndombolo inayoambatana na kukata mauno. Ndiyo! Hiyo ndiyo ajenda ya Bepari angalia Utitiri wa wasanii kwa Mwamerika na Kongo iliyokuwa Zaire huo ni mfumo mahsusi ambao ni ngumu kugundua kwa macho ya kawaida. Akili zetu zimeegemea katika ngono, zinaa, udaku na kuota kuishi maisha ya kwenye tamthilia za maigizo ya Televisheni badala ya ubunifu na kufanya kazi. Naam hiyo ndio njia waliyotuchagulia viongozi wetu huku wakitupa suluhisho la muda mfupi "Shule za Kata". Mabepari watabaki na mbinu ubunifu, ujuzi ili waweze kubeba rasilimali zetu. Na kutulazimisha hata kilicho kinyume na maadili yetu, kwa  kigezo cha haki, misaada na usawa. Kama wanataka Usawa, kwanza watupe fursa ya kujifunza miundombinu mbalimbali ya kukua kiteknolojia na utaalam kama wao ili tuweze kujitatulia matatizo yetu sisi wenyewe. Hawatakubali! Kwa sababu wanataka tuwe wajinga na viongozi wetu wakichekelea kufanywa vibaraka wao. "Mtama wa baba ni nini? Mtama wa baba waliwa".

Biashara ya madawa ya kulevya, mihadarati, fedha haramu pamoja na ile ya silaha. Najua hili la silaha wapo watakao likataa ila lipo. Suala hili la Silaha linatokana na Tanzania kuwa kitovu cha Ukombozi kusini mwa Afrika ambapo stratejia pamoja na mbinu mbalimbali za kiintelijensia za mapambano zilianzia hapa. Baada ya harakati za ukombozi na baada ya kuporomoka kwa dola ya Sovieti, nchi karibia nyingi zilikwisha kombolewa. Wajanja walipata mwanya wa kukomba kiporo cha silaha kilichobakia na kuunza kwenye nchi zilizo na migogoro katika ukanda wa ziwa. Hatuelewi na hatujapata taarifa rasmi za maghala yetu kulipuka ambazo zitaweza kutuaminisha kitaalamu labda kwa sababu ya umbumbumbu wetu na kukosa umuhimu katika masuala ya usalama wa nchi. Nirudi kwenye madawa ya kulevya, wanasiasa kwa viongozi wa dini, wakurugenzi kwa maofisa wa polisi, wapelelezi kwa wakaguzi wa forodha wote wakitumika kufanikisha biashara hii huku Mtanzania akiteketea kama mshumaa. Maghorofa ya vioo Darisalama yanaota kama uyoga wenye kuyajenga haijulikani pesa wanaitoa wapi mwishowe tutayaita "Cocaine Towers" kama hawatatuthibitishia uhalali wake. "Mtama wa baba ni nini? Mtama wa baba waliwa"

Ngoja nimalizie, nisionekane mchochezi naandika bila ushahidi na utafiti, habari zangu za vijiweni hazina chanzo. Kwa hao wanaotapatapa na kuhaha kupitia makasuku wao ili waonekane safi pamoja na kutoa vitisho lukuki na hatua kazli za kisheria. Ipo siku watajulikana na wataumbuka. Mwisho wa ubaya ni fedheha na aibu.

"MTAMA WA BABA NI NINI? MTAMA WA BABA WALIWA"

No comments: