Monday, October 21, 2013

BURIANI JULIUS NURU YA BURUDANI REDIONI.

 Na Baraka Mfunguo,

Kama taa inayowaka,
Sauti yako iliwaka na kumulika,
Taifa likaburudika nasi tukajumuika,
Buriani Julius nuru ya burudani redioni.

Ghafla nasikia ati umetutoka,
Duniani umeondoka, yaani umetoweka,
Moyo unaniruka, nakaribia wehuka,
Buriani Julius , nuru ya burudani redioni.

Sauti yako hakika,
Ilileta hamasa Afrika, nasi tukahamasika,
Huyu ndiye Julius , ubunifu asiyefilisika,
Aliyajua maadili, uongozi akasifika,
Buriani Julius, nuru ya burudani redioni.

Klab raha leo show, misakato ukasikika
Nyuzid' Nyuzid', RTD tukaburudika
Leo Julius umekauka
Umelala hutaki amka
Buriani Julius, nuru ya burudani redioni.

Najiuliza Baraka, mbona walalamika,
Julius unayemlilia, yuko na malaika,
Lau siku yako ikifika, nawe huko utafika,
Ama kweli katika kifo, hakuna atakayesalimika,
Buriani Julius, nuru ya burudani redioni.

Machozi yazidi kunitiririka,
Kila ninapokukumbuka,
Sauti yako na burudani, redioni hazitasikika,
Wema hawana maisha, Balisidya alinung'unika,
Buriani Julius, nuru ya burudani redioni


PUMZIKA KWA AMANI ANKO J. JULIUS NYAISANGAH.

No comments: