Tuesday, October 1, 2013

ASASI 50 ZAPINGA MWANANCHI NA MTANZANIA KUFUNGIWA

Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu unaowakilishwa na mashirika zaidi ya 50 yasiyo ya kiserikali, yameungana kulaani kitendo cha Serikali kuyafungia magazeti ya Mwananchi na Mtanzania.

Taasisi hizo zimeungana na Umoja wa Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania (Moat), Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika-Tawi la Tanzania (Misa-Tan), na Baraza la Habari Tanzania (MCT) kupinga kitendo hicho kilichofanywa na Serikali, Jumamosi iliyopita.
Serikali ilitangaza kulifungia Gazeti la Mwananchi kwa wiki mbili na Mtanzania kwa siku 90 kuanzia Jumamosi iliyopita kwa kile ilichoeleza ni kuandika habari za uchochezi.
Akisoma tamko hilo leo, Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu ambao ni mkusanyiko wa asasi  za kiraia zinazotetea haki za binadamu (THIRD-Coalition), Onesmo ole Ngurumwa alisema kitendo cha Serikali ni cha kutishia na kuzua hofu kwa jamii na kurudisha nyuma harakati za kukabiliana na haki za binadamu.
“Taasisi hizi kwa umoja wake zimeona kufungiwa kwa magazeti haya ya wananchi kuna lengo la kutisha watu wake,” alisema.
Alisema pia uamuzi huo wa Serikali una lengo la kuwanyamazisha wapigania na watetezi wa haki za binadamu na vyombo vya habari nchini.
"Uamuzi huo wa Serikali kuwa ni kinyume cha Katiba ya nchi. Ni wazi kwamba hatua hii ya Serikali ni ukiukwaji mkubwa wa Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Ibara ya 18(1)(2) ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, Toleo la mwaka 2010,” alisema ole Ngurumwa.
Alisema hatua hiyo ni mwendelezo wa matumizi ya sheria kandamizi ya Magazeti ya mwaka 1976 na ile ya Usalama wa Taifa ya mwaka 1970 ambazo zinavunja uhuru wa vyombo vya habari na haki ya kupata habari.
"Sheria hizo ndizo zilizotoa madaraka kwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo kuyafungia magazeti haya. Kutokana na hali hiyo, tumependekeza mambo tisa muhimu ya kuchukuliwa ili kukomesha uvunjaji huo wa haki za binadamu.
Alitaja baadhi ya mambo hayo kuwa ni Serikali kuyafungulia magazeti yote yaliyoyafungiwa na kufuta na kuzifanyia marekebisho sheria hizo kandamizi. Katiba iheshimiwe kwa sababu ndiyo sheria mama ili kuondoa sheria zinazokinzana nazo.
“Ipo haja kwa yeyote anayelalamikia habari iliyotolewa na vyombo vya habari basi apeleka malalamiko kwenye Baraza la Habari Tanzania (MCT)."


MWANANCHI

No comments: