Thursday, August 1, 2013

TULIKOSEA KATIKA MADINI,TUSIKOSEE KATIKA GESIHII NI MAKALA KUTOKA GAZETI LA RAIA MWEMA-JIPATIE NAKALA YAKE UJISOMEE HABARI ZA KUSISIMUA .

Na Balozi Mwanaidi Maajar,

MIAKA michache kutoka sasa, uchumi wa Tanzania utaanza kutegemea zaidi nishati ya gesi tuliyonayo. Takwimu zinaonyesha tuna akiba ya gesi ya kiasi cha futi za ujazo (cubic feet), trilioni 40 na hiki ni kiasi kikubwa sana.

Jambo la msingi kwetu kama taifa ni kuangalia ni kwa kiasi gani tutafaidika na ugunduzi huu mkubwa wa gesi. Ni wazi hatukuwa tumejiandaa vya kutosha wakati wa ugunduzi wa madini kama vile dhahabu na taifa letu halijafaidika vya kutosha.

Nafananisha hali ya sasa ya uchumi wa gesi unaokuja na treni ambayo iko stesheni inasubiri abiria. Ni lazima tuipande treni hii. Tusikubali ituache kama treni ya dhahabu ilivyotuacha. Ni treni ambayo italipeleka taifa letu kuwa miongoni mwa nchi zenye uchumi wa kati. Tusikubali ituache.

Kuna mambo ya msingi ambayo sisi kama taifa na watu ni lazima tuyafanye. Na tuyafanye kuanzia sasa ili tufaidike tunakokwenda. Jambo la kwanza ni kwamba ni lazima mambo haya ya msingi yazungumzwe na yazoeleke.

Sisi, katika taasisi ya Rex Attorney, kwa mfano, tutaanzisha kitu kinachoitwa Breakfast Debate. Katika mikutano hii, wasomi, wanaharakati, wanasiasa, watu wa serikali, wananchi wa kawaida na asasi za kiraia watakuwa wakikutana kujadili mambo anuai kuhusu nishati ya gesi na uchumi wake.

Mikutano hii itakuwa ikifanyika mara moja kwa mwezi na waalikwa watakuwa wakijadili kwa mapana masuala ya gesi. Mikutano itakuwa ikifuata kanuni maarufu zinazofahamika kwa jina la Chatham. Chini ya kanuni hizi, wazungumzaji hawataruhusiwa kutajwa majina yao au kuzungumzwa waliyosema kwenye taarifa za nje ya mkutano.

Lengo ni kuwapa wazungumzaji uhuru wa kuzungumza kila kitu kwa uwazi mkubwa. Bila ya hofu ya kunukuliwa vibaya kwenye vyombo vya habari au mahali popote. Tunahitaji kuona ule uwazi na upeo wa juu kabisa katika ujengaji wa hoja.

Ninaamini, zaidi ya mambo yote mengine, watu wanahitaji kuzungumza kuhusu mambo haya ya gesi. Hili ni jambo ambalo halikufanyika wakati tukiingia kwenye uchumi wa madini na nadhani ni mojawapo ya sababu za kwanini hatujafaidika sana na utajiri wetu wa madini.

Kuna mambo ya kuzungumza. Kwa mfano, kwenye mikataba ya kampuni za madini, kulikuwapo na vipengele vinavyoonyesha kampuni hizo zina wajibu wa kufunza (kuelimisha) wazalendo katika sekta hiyo ili wafaidike na fursa hizo.

Mpaka sasa, sijui hilo limefanyika kwa kiasi gani. Sijui ni Watanzania wangapi ambao walifaidika na mafunzo yaliyotolewa na kampuni za madini.

Kwenye uchumi wa madini au gesi kuna mambo ambayo ni muhimu yafanyike ili taifa lifaidike. Kwa mfano, ni muhimu kujua taifa limejipangaje kuhakikisha kunakuwa na mwingiliano wa sekta hiyo na sekta nyingine. Nitatoa mifano.
Wakati kampuni za madini zikija nchini, zilikuja na vitu vingi kutoka kwao. Walikuja na mitambo yao, wafanyakazi wao na wengine walikuja na vyakula vyao. Kama taifa, ni lazima tufahamu ni kwa vipi kampuni hizi zitasaidia ukuaji wa sekta nyingine za uzalishaji kama vile kilimo na viwanda vidogo vidogo.

Hatukujiandaa kwa hili kwenye madini na ni muhimu, muhimu sana, kutorudia makosa kama hayo kwenye uchumi wa gesi. Mijadala haipaswi kuwa kuhusu iwapo gesi itatoka Kusini au haitatoka bali ni kwa vipi watu wa Kusini na Tanzania kwa ujumla watanufaika na gesi hiyo.

Ndiyo maana, kupitia Breakfast Debate, tutakuwa tayari kualika watu kutoka katika nchi ambazo zimefaidika na uchumi wa gesi na zile ambazo hazikufaidika. Lengo litakuwa ni kuhakikisha tunajifunza kutokana na makosa na umahiri wa wenzetu. Lakini ni lazima watu wazungumze.

Kwenye kufaidika na gesi, ile kauli maarufu ya aliyekuwa Rais wa Marekani, John F. Kennedy; Usiulize nini taifa lako limekufanyia bali jiulize nini umelifanyia taifa lako, ina nafasi kubwa. Kama sote tukitimiza wajibu wetu sasa, kwa kizazi hiki, kizazi kijacho kitatushukuru.

Huu ni wakati wa kuhakikisha kwamba taifa letu linaingia kwenye uchumi wa gesi likiwa na sera na sheria zilizo sahihi huku wananchi wake wakiingia katika uchumi wa gesi wakiwa na akili (mentality) iliyo sawa. Watu hawatakiwi kuingia kwenye uchumi huo wakiwa na mawazo potofu.

Ziko nchi duniani ambazo zimefaidika na nishati ya gesi. Utajiri wa gesi haupaswi kabisa kuwa chanzo cha migogoro na kuleta kile kinachoitwa Resource Curse (Laana ya Utajiri). Utajiri ni jambo la baraka na Mungu alikuwa na maana yake kutupa Watanzania utajiri wote huu aliotupa.

Ninaamini, vyombo vya habari vina nafasi kubwa katika ujenzi wa taswira iliyo sahihi kuhusu uchumi wa gesi. Wakati nikiwa Balozi wa Tanzania nchini Marekani, kulikuwapo na kashfa kubwa ya Kampuni ya Shell kumwaga mafuta katika bahari za Marekani.

Bosi Mkuu wa kampuni hiyo ya mafuta alikuwa mapumziko wakati matatizo yakitokea. Vyombo vya habari vya Marekani vikampiga picha na kumsema kwamba anastarehe vipi wakati bahari za nchi yao zinateketea? Matokeo yake Marekani imelipwa fidia nzuri na kampuni hiyo.

Tunataka vyombo vya habari ambavyo ni vya kizalendo. Vyombo vilivyo tayari kupigania maslahi ya Watanzania na Tanzania. Si vyombo ambavyo vinachochea hofu na vurugu. Si vyombo ambavyo havina ajenda yake ya kitaifa kuhusu rasilimali za taifa letu.

Nimefanya kazi nyingi za kisheria. Nimetumikia taifa langu kama balozi. Lakini, nitajisikia fahari zaidi iwapo nitaweza kusaidia kufanikisha nchi yangu ifaidike na utajiri wa gesi tulionao. Ninaamini, tukifika huko, nitaangalia nyuma na kuona kwamba huo ulikuwa mchango wangu mkubwa zaidi kwa taifa hili.

Tujiandae kwa uchumi wa gesi. Tusikubali treni hii ituache.

Mwanaidi Sinare Maajar ni Mwanasheria na Mwanadiplomasia. Amewahi kuwa Balozi wa Tanzania katika nchi za Uingereza na Marekani. Kwa sasa ni mmoja wa wabia katika kampuni ya kisheria ya Rex Attorney jijini Dar es Salaam. Maelezo yake haya yamechukuliwa jijini wiki hii na Ezekiel Kamwaga. RAIA MWEMA

No comments: