Friday, August 16, 2013

NANI NI MHAMIAJI HARAMU?

KUNA watu mkoani Kagera wanaitwa ‘wahamiaji haramu’. Hawa wanaoitwa wahamiaji haramu ni wale wanaoishi miongoni mwa jamii zao zilizogawanywa na wakoloni walipoweka mipaka miongo mingi iliyopita.

Ni muhimu kutambua kuwa sehemu zote za mipakani zina matatizo ya aina hii. Kwa sehemu kubwa matatizo haya yanatokana na kutofahamu sheria za uhamiaji.

Kwa bahati mbaya sana, operesheni za kuhamisha hawa wanaoitwa wahamiaji haramu, zimekuwa zikitokea kwa vipindi tofauti, na ghafla zinatoweka baada ya wahusika wa operesheni hizi kuwa wamenufaika na mali wanazopora kutoka kwa watu hawa, hasa mifugo na wakati mwingine hongo ya fedha.

Kitu ambacho watawala wetu wamekataa kutambua ni ukweli kwamba wakati wakoloni wakiweka mipaka, hawakuangalia kama kabila moja limegawanywa na mpaka.
Walichokifanya ni kuweka hiyo mipaka na kuacha makabila tofauti ya mipakani yakiangukia pande mbili za nchi tofauti.
Isitoshe, wakati mwingine makabila haya yalikuwa chini ya himaya moja kama ilivyo Bunyoro Kitara iliyojumuisha watu wa Kagera na sehemu za nchi jirani.

Tangu kupatikana kwa uhuru wa nchi za Afrika Mashariki, suala hili limekuwa likiachwa bila msimamo unaojulikana.
Watu wakaendelea na shughuli zao hadi kunapotokea tatizo la kisiasa kati au baina ya nchi zenye mpaka mmoja, basi suala hilo huibuka na kuwataka wale wanaoshabihiana kwa sura na jamii iliyo upande wa pili, kuondoka na kurudi ‘kwao’.

Kwao ni wapi? Vurugu hizi zimekuwa zikiibuka na kutoweka. Ni ukweli kuwa kutojua sheria si utetezi, lakini je, si busara serikali yeyote makini kuwasaidia wananchi wasio na uelewa wa mambo haya ili kuondoa mzozo wa mara kwa mara?
Hawa tunaowaita wahamiaji haramu, wengi wao wanasalitiwa na maumbile yao ya kinasaba.

Mkoa wa Kagera una watu wa jamii ya wafugaji waitwao Wahima ambao wamekuwa katika mkoa huu kwa miaka mingi.
Haiyumkini watu hawa wanashabihiana zaidi na wenyeji wa nchi jirani, lakini wanaweza kuwa siyo raia wa nchi hizo.
Ni kweli kuna walio raia wa nchi jirani, lakini pia kuna walio raia wa Tanzania.

Kuna wahamiaji wachache wanaweza kuwa wameingia nchini kinyume cha sheria; hawa wanaweza kuondolewa. Lakini si aina hii ya operesheni yenye uonevu ndani yake.
Mimi ninayeandika haya, baba mzaa babu ni kutoka Nkole kule Uganda. Isitoshe, marehemu baba yangu anamiliki shamba Wilaya ya Lakai hukohuko Uganda; hata bibi yangu mzaa huyo baba amezikwa huko.

Leo utaniambia niondoke nirudi ‘kwetu’ Nkole? Kwetu wapi? Baadhi ya hawa wanaoitwa wahamiaji haramu katika Mkoa wa Kagera, hususan Wilaya ya Missenyi, kinachowaponza ni utajiri wao wa mifugo. Hapa aliye muungwana atakubaliana na ukweli huu.

Wenzetu hawa wana talanta ya ufugaji na wengi wao wamepata ng’ombe wa kuanzisha ufugaji huo kutoka kwa jamii nyingine mkoani humu.
Hii ni talanta yao kama walivyo wenzetu Wachagga katika umahiri wa uchuuzi na biashara. Sisi wakazi wa Kagera tusimame kidete kukataa uporaji huu wa mali za watu kwani uchumi wa mkoa wetu utarudi nyuma.

Tuangalie mfano wa Zimbabwe, yalinyang’anywa mashamba kutoka kwa Wazungu; wakagawiwa wazalendo ambao wameyaacha yakiwa machaka; huku Zimbabwe ikigeuka ombaomba wa chakula.
Tusijidanganye kwamba tukipora mashamba na mifugo ya hawa ndugu zetu wanaoitwa wahamiaji haramu tutafaidika na lolote.
Huu uamuzi unatokana na tofauti za viongozi wa kisiasa ambao hawaathiriki na kadhia hii. Tukubali ukweli kuwa hili ni tatizo la kikoloni.

Tanzania hatuna uhaba wa ardhi. Wale ambao tunao tayari watambuliwe kama raia wa nchi hii. Tusijidananye, hili si tatizo la Kagera tu. Ni la Kigoma, Tanga, Mara, Mtwara na kwingineko kwenye mipaka kati yetu na nchi nyingine.
Kuna wakati kiongozi mkubwa wa nchi hii alituhumiwa kuwa Mmakonde wa Msumbiji! Nina mfano wa diwani mmoja wa zamani kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambaye alihudumu kwa vipindi tofauti wilayani Missenyi, akifadhili chama wakati ni mtu wa jamii ambayo sasa ‘haitakiwi’.

Kumbuka hata Marekani imekubali kuwa maendeleo ya nchi yao yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na ‘wahamiaji haramu’. Tushikamane wana Kagera, mkoa wetu unarudi nyuma.


TANZANIA DAIMA

No comments: