Sunday, August 4, 2013

MKAZI WA NEWALA AJILIPUA KWA MOTO


 
MKAZI wa Kijiji cha Mtungulu, wilayani Newala, mkoani Mtwara, Kibwana Mpeme (60), amejiua kwa kuchoma moto nyumba aliyokuwamo kwa kile kinachodaiwa kuchoshwa na maradhi ya moyo.
  
Taarifa zilizothibitishwa na Mwenyekiti wa kijiji hicho, Rashidi Uledi, zimeeleza Mpeme aliyekuwa akisumbuliwa na maradhi hayo kwa muda mrefu, siku moja kabla ya tukio hilo aligombana na mkewe na kumpiga hadi kumjeruhi, hali iliyosababisha apelekwe hospitali.

Akizungumza kwa njia ya simu kutoka kijijini hapo, Mohammed Mkupuni, ambaye ni mpwa wake, Ismail Rajabu, aliyejeruhiwa akiwa katika harakati za kumuokoa Mpeme, alisema mke wa marehemu alipotoka hospitali alikwenda kwa ndugu yake akihofu madhara zaidi.

Mkupuni aliiambia Tanzania Daima kuwa baada ya Mpeme kuwa peke yake aliichoma moto nyumba aliyokuwamo na majirani walipoona moshi huku wakijua kuna mtu ndani walianza harakati za kumuokoa.
“Ismail akiwa na wenzake waliuvunja mlango wa nyumba ili kuingia ndani kumuokoa mzee Mpeme, lakini wakashaangaa kuona akiwalenga kwa mshale na kumfyatulia Ismail kifuani na kumjeruhi vibaya,” alisema Mkupuni.

Aliongeza kuwa baada ya Ismail kujeruhiwa na marehemu, waokoaji wengine wakahofia usalama wao na kususia zoezi hilo, na mzee huyo kufa kwa kuteketea kwa moto.

Mkupuni alisema Ismail alikimbizwa hospitali kwa matibabu na polisi kutoka Newala walifika na kuchukua maelezo ya tukio hilo na kuruhusu mwili wa marehemu kuzikwa.

No comments: