Thursday, July 25, 2013

BEI DIRA: CHANZO CHA KUYUMBA ZAO LA KOROSHO


Na Abdallah Bakari,
Upangaji wa bei dira ya zao la korosho usiozingatia utaalamu ni kiini cha kuyumba kwa bei na soko la korosho nchini hasa katika Mkoa wa Mtwara na kusababisha vurugu kutoka kwa wakulima wa zao hilo.
Uchunguzi unabainisha kwamba katika wilaya za Masasi, Tandahimba, Nanyumbu na Newala mkoani Mtwara kumekuwa na ongezeko la bei dira katika misimu miwili iliyopita na kuyumbisha soko la zao hilo.
Bei ya kurosho haieleweki
Kumbukumbu zinaonyesha kwamba msimu wa ununuzi wa zao hilo 2012/13 na 2011/12 bei dira ilikuwa Sh1,200 kwa kilo moja ya korosho, wakati msimu wa 2010/11 na 2009/10 ilishuka na kufikia Sh850 tu kwa kilo.
Msimu wa 2008/9 bei dira ilikuwa Sh800 na msimu wa 2007/8 ambao utaratibu wa stakabadhi ghalani ulianza kutumika na bei dira ilikuwa Sh700 tu kwa kilo.
Uchunguzi umebaini kuwa tangu bei dira ilipopanda na kilo moja ya korosho kufikia Sh1,200, mwenendo wa soko na bei ya korosho umekuwa ukiyumba kila msimu wa zao hilo. Bei dira ya juu ya misimu ya awali ilifikia Sh850 kwa kilo na kusababisha vurugu baada ya wakulima kulalamika kwamba bei hiyo ilikuwa ndogo.
Wakulima wamepokea na kutafsiri kwamba bei dira ndiyo bei ya chini ambayo wanapaswa kuitumia wakati wa kuuza mazao yao kwa wanunuzi. Tafsiri hiyo imesababisha vurugu kutoka kwa wakulima dhidi ya viongozi wa vyama vya ushirika wakati bei ya kuuza zao hilo inapokuwa chini ya bei dira.
Hivi karibuni katika Wilaya ya Tandahimba mkoani Mtwara katika msimu 2011/12 kuliibuka vurugu na kusababisha uvunjifu wa amani na ubadhiribifu wa mali za viongozi wanaotuhumiwa.
Katibu wa Chama cha Msingi cha Ushirika cha Mnanje wilayani Nanyumbu mkoani Mtwara, Baraka Mrope anasema chama chake kimeshindwa kulipa bei dira ya Sh1,200, badala yake wamewalipa wakulima Sh1,115 kwa kilo moja ya korosho.
Anasema hali hiyo ilizua malumbano kati ya chama hicho na wakulima kwa hisia kwamba uongozi wa chama hicho umeiba Sh85 zilizosalia.
“Mimi nilidhani ingekuwa vizuri kama suala la bei dira likaachwa mikononi mwa wataalamu badala ya wadau ili pale matarajio yanaposhindwa kufikiwa basi wawajibishwe, tusiwe kisiasa zaidi, biashara na siasa haviendi pamoja,” alifafanua Mrope.
Katibu huyo anabainisha kwamba wajumbe wanaopanga bei dira wamekuwa wakitawaliwana na wanasiasa ambao wanazima sauti za wataalam na kusababisha kwenda kinyume na soko la korosho.
Mkulima wa Korosho wa Kijiji Cha Mnanje anasema: “Bora stakabadhi ghalani ifutwe, bei inayopangwa haitufikii, ubabaishaji ni mwingi.”
Diwani wa Viti Maalum wa Wilaya ya Newala, Halima Malolo anasema tatizo ni wakulima kwa kuwa hawakubaliani na ushauri wa wataalam, kwenye mkutano wa wadau wa kupanga bei dira, msimu uliopita wataalam walishauri bei dira iwe Sh950, lakini walipinga na kupanga Sh1,200.
Mkulima wa korosho wa Kijiji cha Mbuyuni, wilayani Masasi, Jafari Mkata anasema kuyumba kwa soko katika misimu miwili iliyopita kumechangiwa na kupanda kwa bei dira.
“Bei dira inapokuwa kubwa kuliko hali halisi ya soko, wanunuzi hawaingii sokoni, korosho zinachelewa kuuzwa.
“Kutokana na bei dira kuwa kubwa hata ushuru wa asilimia tano kwa halmashauri za wilaya unakuwa mkubwa, kwa mfano miaka hii miwili, ushuru umekuwa Sh60 kwa kilo, hayo yote yanamuumiza mkulima anayelipa,” anasema.
Mtafiti wa zao la korosho katika Kituo cha Utafiti Naliendele, mkoani Mtwara, Dk Louis Kasuga anasema wataalam hawajapewa fursa ya kusikilizwa wakati wahusika wakipanga bei dira ya zao hilo.
“Sisi wataalam tulipendekeza bei dira kwa msimu 2012/13 iwe kati ya Sh900 au Sh1,000, lakini wadau walipinga hilo,”anafafanua Dk Kasuga.
Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika Mtwara, Masasi (MAMCU), Fikili Makarani anasema ni muhimu kuwa na bei dira ili kutoa taswira halisi ya mwenendo wa soko.
Fanyeni tathimini
Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT), Mfaume Mkanachapa anasema wataalam wanakabiliwa na changamoto kubwa ya mapendekezo yao ya bei dira zao kukubalika.
“Mkutano wa wadau upo kisheria na ndiyo wenye mamlaka ya kupitisha bei dira, kimsingi kunatakiwa kufanyika kwa tathimini kwa kuwa unapoweka bei dira kubwa, wanunuzi wanapungua sokoni,” anasema Mkanachapa.


MWANANCHI

No comments: