Monday, May 20, 2013

UBINAFSI,ULAFI NA UFISADI VIMEMUUA DR. MASAU

NI kifo cha heri na baraka alichokipata ndugu yetu, kaka na baba yetu Dk. Ferdinand Massau. Ni shujaa wa kuokoa maisha ya watu aliyetangulia mbele ya haki, alitaka kuokoa ‘akapigwa’ yeye. Dk. Masau alikuwa mtaalamu wa upasuaji wa moyo nchini, aliyejaribu kuanzisha Taasisi ya Moyo (THI) ya kuwahudumia wagonjwa wote wenye matatizo ya moyo na kuwafanyia upasuaji bila kupelekwa nchi za nje.

Daktari huyu amenyanyasika kwa sababu ya uzalendo na huruma yake kwa Watanzania masikini, hadi yamemfika na amepoteza uhai wake. Pengine kwa ‘kupigwa kwake sisi tutapona’.

Dk. Masau alikuwa mmoja wa wataalamu wachache wa upasuaji wa moyo, kujitoa kufanya kazi ya kuhudumia wagonjwa wa moyo hapa nchini, tena masikini bila malipo, akijitahidi kwa kushirikiana na marafiki zake kutoka Ujerumani, Marekani na Uingereza kutoa huduma za matibabu ndani ya nchi yetu badala ya kuingia gharama kubwa kwenda nchini India. Baadhi ya viongozi wa serikali na wahudumu wa Wizara ya Afya hawakufurahishwa na
mpango wa kuhudumia wagonjwa hapa nchini na kuokoa mabilioni ya fedha zilizokuwa zikipelekwa nchini India kwa sababu gawio la asilimia 10 halitapatikana tena.

Kwanini nasema ni baadhi ya watu walioko serikalini? Ni kwa sababu serikali haikutaka kujihusisha au kujali mgogoro uliokuwa ukiendelea kati ya THI na NSSF, hata siku ambayo wagonjwa walitakiwa kutolewa nje pale THI serikali ilikaa kimya.

Hatutakiwi kulalamikia uamuzi wa mahakama, lakini inapotokea utu umekosekana dhamira zinatuuma. Asiyeumwa na dhamira ana tatizo kiroho au kinafsi.

Tujiulize ni Watanzania wangapi masikini ambao wakienda Wizara ya Afya kuomba msaada wa kupelekwa India kwa matibabu wanapata? Je, ni wafanyakazi wangapi wa serikali wa kada za chini au kati ambao wakiugua wanapelekwa India? Lakini kama kuna matibabu ya bei nafuu hapa Tanzania ambayo serikali imetoa msamaha wa kodi kwa vifaa vyake au inatoa ruzuku wananchi wanaweza kutibiwa na kuokoa maisha yao.

Kifo cha Dk. Masau si kwamba kimetushtua Watanzania tu bali hata wageni. Ni mtu aliyeona mbali, aliyefikiri juu ya kulisaidia taifa lake na kurudisha fedha ndani kwa ajili ya kukuza uchumi na ustawi wa afya za jamii. Lakini wale waliopewa dhamana wameamua kummaliza ili wafaidi asilimia 10. Hii ni laana na damu za wagonjwa waliokuwa wakipata matibabu katika Taasisi ya Moyo nchini itawalilia wao na kizazi chao. Kwanini tunakosa utu, huruma? Tunafikiri kuwa fedha za duniani zitatufikisha mahali? Watu wangapi wameondoka duniani wameacha matrilioni ya fedha? Yuko wapi bilionea aliyekuwa Rais wa Libya Hayati, Muammar Gaddafi? Wako wapi matajiri wa Kitanzania masikini walioishi kama miungu watu hapa duniani? Si kwamba hata magari au ndege zao zinawageuka na kuwaua? Tumuogope Mungu mwenye nguvu.

Malengo ya Dk. Masau katika taasisi ya THI yalikuwa kuwafanyia uchunguzi na upasuaji wa moyo walengwa, hasa watu masikini wa Tanzania. Kama alivyoandika kwenye tovuti ya THI; “Overall diagnosis as well as surgery of heart related disease are our targets, especially to poor people.” Inasikitisha kuwa lengo hili lilipigwa vita na Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) wakakubali kutumika vibaya kumfukuza katika taasisi hiyo huku wakilazimisha wagonjwa waliokuwa wamelazwa na dripu zao kutolewa nje.

Mara kadhaa kesi zimeendelea mahakamani, huku Dk. Masau akiwa ameshalazwa rumande kwa kesi yenye mahusiano na THI, lakini mwishowe Julai 10, 2012 taasisi ilifungwa rasmi na mali zake zote kupigwa mnada na Mahakama Kuu kitengo cha Ardhi. Tunajiuliza wanaopiga mnada mali za kuhudumia wagonjwa wanawatumikia Watanzania gani? Je, wanastahili kuendelea kuitwa Watanzania? Je, kama Shirika la Hifadhi ya Jamii ambalo Watanzania wameweka fedha zao linashindwa kutafakari umuhimu wa ustawi wa afya za watu wake linawatumikia kina nani? Si kwamba fedha hizo ni bora zingechelewa kutoka THI kuliko kuwekeza kwenye majengo ya watu binafsi na wafanyabiashara? Ona sasa kazi waliyoianzisha ya kukwamisha utaalamu wa Dk. Masau imekamilika.

Huyu Dk. Masau ni Mtanzania masikini aliyethubutu kujaribu kitu kipya kwa ajili ya Watanzania wenzake, akapigwa vita hadi kupoteza uhai wake kwa msongo wa mawazo. Je, wataalamu wengine wazawa watakubali kurudi nchini? Si kwamba kila mtu akikumbuka yaliyomkuta Dk. huyu atabaki huko?

Sote tunajua kuwa matibabu ni gharama, hususani ya upasuaji wa moyo, misuli na mifupa. Lakini gharama za safari na kuishi nchi jirani, kutafuta hati ya kusafiria na visa zinamuongezea mgonjwa mzigo mkubwa. Kwa sasa ukitaka kupata matibabu ya bei nafuu kabisa nchini India si chini ya dola za kimarekani 10,000 sawa na sh mil. 16.3, pamoja na kulala na kula kwa siku 14 utakazokaa hospitalini. Je, Watanzania wangapi wanamudu gharama hizi?

Kosa kubwa la Dk. Masau ni kuthubutu kwa mafanikio kiasi kutibu ugonjwa wa moyo kwa upasuaji nchini, lakini tutamkumbuka na bila shaka, ipo siku tutajenga THI nyingine na itaitwa kwa jina lake. Buriani Dk. Masau Watanzania masikini watakukumbuka daima.

Lakini ufisadi wa aina hii nao utafikia mwisho pale Mwenyezi Mungu atakapoamua na kusema HAPANA! Tuonane wiki ijayo.

----
Deogratius Temba
via Tanzania Daima

No comments: