Friday, May 31, 2013

TULIONYA NA TUNAONYA TENA, BILA AKILI GESI ITATULIPUKIA


 Dr. Kitilla Mkumbo,
LILIANZA kama kero, lakini sasa suala la faida za gesi linalowakang’anya wananchi wa Mtwara na serikali limeanza kuwa tatizo kubwa la kitaifa, linalotishia kubomoa kabisa utamaduni wa kutatua matatizo kwa amani kulikozoeleka miongoni wa Watanzania. Kuna wanaolaumu wananchi wa Mtwara, na wapo pia wanaoilaumu serikali.

Kulaumu ni sehemu muhimu katika kujua chanzo cha tatizo ili uweze kulitatua. Mimi niseme moja kwa moja bila kujiuma kuwa si walaumu wananchi wa Mtwara, sio kwa sababu hawana makosa au wapo sawa katika madai yao. Siwalaumu wananchi kwa sababu wao wametekeleza wajibu wao wa kulalamika, lakini wakakosa mtu wa kubeba lawama zao sawa sawa na kuzijibu.
Nailaumu sana serikali na hasa wizara husika ya nishati na madini kwa kutumia muda mwingi na rasilimali nyingi za taifa kutengeneza majibu kwa maswali ambayo hayakuulizwa na wananchi wa Mtwara.

Tunaweza kujifanya hatuelewi au kupotosha madai ya wananchi wa Mtwara, lakini hii haiondoi ukweli kwamba hatujajibu maswali yanayoulizwa na wananchi wa Mtwara. Wananchi wa Mtwara wanauliza swali moja tu la msingi ambalo halijajibiwa na serikali, na loni: kwa nini viwanda vya kufua gesi visijengwe Mtwara ili gesi isafirishwe ikiwa imeshakwifuliwa?
Kwa maana nyingine wanachouliza wananchi wa Mtwara ni kwa nini viwanda au mitambo ya kufua gesi itengenezwa Dar es Salaam na sio Mtwara? Wananchi wanataka viwanda vijengwe kwao ili vijana wao wapate ajira na mji wao ukue.

Sasa badala ya kujibu swali hili kwa utulivu na kujaribu kuwaelimisha wananchi au kukubaliana nao Wizara ya Nishati na Madini imeingiza propaganda kwa kudai kwamba wananchi wa Mtwara hawataki gesi itumike na Watanzania wengine na kwamba rasilimali za nchi ni za taifa zima bila kujali zilipo, kana kwamba hiyo Mtwara sio sehemu ya Taifa.

Wajibu wa wananchi ni kuuliza maswali na wajibu wa serikali ni kujibu na kuelimisha bila kuchoka hadi wananchi watakapoelewa. Wananchi wasipoelewa sio kosa lao bali ni kosa la huyu anayeelimisha. Sasa serikali imeshindwa kuwaelimisha wananchi wa Mtwara wakaelewa inaanza kuwalaumu na kuwazushia propaganda za kizamani kabisa za kudai kwamba hawataki Watanzania wote wafaidike na gesi.
Propaganda hizi za hatari zinajaribu kutengeneza mazingira ya Watanzania wengine wawachukie wenzao wa Mtwara kwa uchoyo. Huu ni uhochezi na uchonganishi mbaya kabisa hata kama wanaofanya hivyo hawajui kama wanafanya uchochezi.

Pengine kinachokera zaidi katika sakata hili ni pale serikali inapotaka kutuaminisha kwamba wananchi hawawezi kufikiri hadi watumwe na watu wengine. Kwamba kinachoendelea Mtwara sio bure bali kuna mkono wa mtu, na mkono wenyewe unaweza kuwa vyama vya siasa au hata mataifa na kampuni za nje. Huu ni utamaduni mbaya sana ambao inabidi tuukemee kabisa. Kuamini kwamba wananchi hawawezi kufikiri hadi watumwe ni dharau kwa uwezo wa asili wa kufikiri aliyopewa kila mwanadamu.
Tofauti kubwa ya maana iliyopo kati ya binadamu na wanyama wengine kama punda na ng’ombe ni kwamba binadamu ana uwezo wa kufikiri. Hivyo kujaribu kujiaminisha au kuaminisha watu wengine kwamba binadamu hawezi kufikiri au kutenda jambo hadi atumwe ni kumdharau binadamu na ni kujaribu kumvua ubinadamu wake.

Kwa maoni yangu hili ni moja ya jambo ambalo limechochea wananchi kupaza zaidi sauti na kufikia hatua ya kufanya matendo ambayo kimsingi sio utamaduni wa kitanzania katika kudai haki au kutafuta majibu.
Sababu ya pili iliyotufikisha hapo tulipo katika suala la Mtwara ni utamaduni wa viongozi wa serikali za kiafrika wa kutoogopa wananchi wanaowaongoza. Katika utamaduni wa kidemokrasia serikali huogopa wananchi kwa sababu ndio wenye mamlaka na siku zote serikali hujitahidi kujinyenyekeza kwa wananchi. Hata hivyo, pamoja na kwamba nchi yetu kinadharia ipo katika mfumo wa kidemokrasia, viongozi wetu wengi wamekulia katika mfumo hodhi na wa kiimla.

Huu ni mfumo ambao wananchi kawaida huiogopa serikali n aviongozi wa serikali wamezoea kuogopwa. Na hivi ndivyo viongozi wetu wengi walivyo. Wanataka waogopwe kwa sababu ndivyo walivyokuzwa na kuzoeshwa, na ndio maana wanakuwa mbogo kabisa pale ambapo wananchi wanawauliza maswali badala ya kutii. Hawa ni viongozi ambao sio zao la mfumo wa kidemokrasia. Ndio maana viongozi wetu wa nishati na madini lugha zao zimejaa kebehi, ubabe na kiburi. Badala ya kutumia lugha ya kiuongozi yenye kutoa matumaini, viongozi wa nishati na madini wanajibizana na wananchi kibabe: wananchi wanasema ‘gesi haitoki, kiongozi wa serikali anajibu, gesi lazima itoke. Hizi ni lugha za kibabe ambazo zinaeleweka zikitolewa na wananchi lakini kamwe haziwezi kueleweka zikitolewa na kiongozi mwenye dhamana aliyeteuliwa na mkuu wa nchi na tena akitumia jukwaa rasmi kama Bunge.

Tatizo la gesi ni Mtwara ni taswira ya jinsi tulivyoshindwa kuzimudu rasilimali zetu za asili. Yote hii ni kwa sababu serikali imeamua kufanya mambo bila wananchi kujua. Hadi leo hakuna anayejua kilichopo katika mikataba waliyoingia serikali na kampuni za kigeni za kibepari zilizopewa mikataba ya kutafuta hiyo gesi. Kwa hiyo wananchi pamoja na wawakilishi wao (wabunge) wapo katika giza. Ni utamaduni wa ajabu katika utawala ambapo serikali haiwezi hata kuwaamini wabunge.

Sasa mtu akishakuwa kwenye giza atalazimika kupapasa, na akipapasa anaweza kushika chochote na ndicho kinachotokea huko Mtwara. Inabidi tukumbushane tena kwamba rasilimali bila akili hazina maana yoyote. Kinachofanya nchi ziendelee cha kwanza sio rasilimali bali akili, na hasa akili za kiuongozi. Nimewahi kutoa mfano wa Israel mara kadhaa. Kwamba Taifa la Israel halina rasilimali za maana. Nchi yao ni ndogo yenye ukubwa sawa na Mkoa wa Tanga pekee. Karibu nusu ya nchi hii ni jangwa. Lakini Israel ni Taifa lenye nguvu kubwa za kiuchumi, kiinteligenisia, na kisayansi kwa sababu waliamua kuwekeza kwenye rasilimali akili, na hasa kuhakikisha kwamba kila mara wanachagua viongozi wenye akili na upeo wa kuona mbali zaidi ya mipaka ya Israel.

Bila kuwekeza kwenye akili gesi haitatusaidia na badala yake itatulipukia. Tayari tuna mifano hai. Madini yetu yanaelekea kwisha na hayajatusaidia sana. Wananchi wa Mtwara wanajua kilichowapata wenzao wa Geita ambao ardhi waliomo imejaliwa madini tele lakini hadi leo ni miongoni mwa mikoa masikini kabisa Tanzania.
Viongozi wetu wajifunze kujadiliana na kuwaamini wananchi kwamba wanaweza kujitegemea kifikra bila kutumwa na mtu yeyote.

Tatizo la Mtwara kuhusu gesi linatatulika kwa viongozi wetu kuwekeza muda wa kujaribu kuelewa hoja ya wananchi hao na kuwapa muda tulivu wa kuwasikiliza. Kuwasema na kuchapisha lundo la maelezo kwenye magazeti halitasaidia sana. Hili ni jambo linalohitaji akili ya kiuongozi na sio ubabe wa kitaaluma katika kulitatua. Namtakia kila la heri Waziri Mkuu katika ziara yake huko Mtwara, na juhudi zake za kujaribu kurudisha maelewano kati ya serikali na wananchi. RAIA MWEMA

1 comment:

Chinang'o mwiro said...

well Nadhani nimekuelewa vizuri and naomba unielewe pia. wananchi wa mtwara wanatakiwa kujua kwamba mradi wa gesi unatoa bidhaa za aina tatu : kwanza ni umeme baada yakuwa imebadilishwa pili ni gesi ya majumbani na viwandani kwamaana badala ya viwanda na majumba kutumia umeme kwa kupigia na kuzalishia bidhaa watatumia gesi ambayo tafika kwanjia ya bomba na kila nyumba au kiwanda kitakuwa na meter kwa ajili ya bili kama vile maji. la tatu ni mabaki ya gesi ghafi ambayo yatatumika kuzalisha mbole.
kwahiyo basi, kuondoa gharama katika kufanikisha haya yote kwapamoja njia pekee sahihi ni bomba na sio nguzo za umeme. ukisema ujenge nguzo na umeme kupelekwa kwenye grid itakuwa umesolve bidhaa moja tu ya umeme na kulazimika kujenga bomba kwa bidhaa gesi ya majumbani na viwandani.

so nakuomba kwakuwa wewe umeelewa then tumia muda wako kama nilivyotumia mimi kuwaelimisha wengine katika kukidhi maslahi ya taifa letu sote.

wabillah tawfiq, mwenyezi mungu akujaalie uadilifu na ukweli.